MHE. RASHID M. MTIMA aliuliza:-
Je, lini Serikali itajenga josho la kuogeshea mifugo katika Jimbo la Newala Mjini?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ninaomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Rashid Mohamed Mtima, Mbunge wa Newala Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa ujenzi na ukarabati wa majosho katika kudhibiti magonjwa yanayoenezwa na Kupe na Mbung’o nchini. Katika kutekeleza azma hiyo Serikali ilianza kutekeleza mpango wa ujenzi wa majosho tangu mwaka wa fedha 2021/2022 ambapo hadi sasa jumla ya majosho 754 yamejengwa nchini kwa thamani ya shilingi bilioni 15.19.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali imejielekeza katika kutekeleza na kukamilisha miradi ya kimkakati ikiwemo kuendelea na mpango wa chanjo na utambuzi wa mifugo nchi nzima kwa lengo la kufikia azma ya kutokomeza magonjwa yenye athari kwa afya za wanyama na binadamu nchini kote.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuratibu ujenzi, ukarabati na uendelezaji wa miundombinu muhimu ya mifugo katika maeneo mbalimbali hapa nchini, ikiwemo majosho ya Newala Mjini, kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma za mifugo kwa wananchi kadri ya upatikanaji wa fedha. Aidha, ninatoa rai kwa Halmashauri ya Newala Mjini, kutenga fedha kutoka katika mapato yake ya ndani kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa majosho katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha.