Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Rashid Mohamed Mtima (3 total)

MHE. RASHID M. MTIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza swali la nyongeza katika sekta hii ya kilimo kwamba, ni lini Serikali itakamilisha designing ya mradi wa umwagiliaji eneo la Chikwedu, Chipalang’anda na Lipeleng’inyi ambalo utawezesha wananchi wa Vijiji vya Chihanga, Mpilipili, Chiunjila na Tarafa ya Mkunya jumla, ili kutumia maji ya Mto Ruvuma kuweza kumwagilia na kuongeza kipato kupitia sekta hii ya uzalishaji ya Kilimo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu katika maswali niliyotangulia, ni kwamba miradi yote ya umwagiliaji ikiwemo hii ambayo ameitaja Chipalang’anda, (majina yake ni magumu kidogo), lakini miradi yote hii sisi kama Serikali tulishapewa maagizo na Mheshimiwa Rais kuingiza katika mipango, kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili tupate gharama halisi, na baada ya hapo tuweze kuitangaza ili iweze kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, at least kwenye suala la miradi ya umwagiliaji, kwa sababu ni ajenda kubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita, niseme tu kwamba haya ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais, na sisi jukumu letu ni kutekeleza. Kwa hiyo nimwondoe tu shaka Mheshimiwa Mbunge kwamba tunalifahamu, na kazi inaendelea.
MHE. RASHID M. MTIMA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza katika Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itatatua tatizo la upatikanaji wa simu katika maeneo yafuatayo katika Jimbo la Newala Mjini: Kata ya Nanguruwe, Kijiji cha Nanguruwe, Mnanje, na Mtawe; Kata ya Mcholi I, Kijiji cha Chikwedu na Chiunjila; Kata ya Namiyonga, Kijiji cha Nakachela na Mandumba; Kata ya Mnekachi Kijiji cha Kazamoyo; na Kata ya Mtumachi, Kijiji cha Mcholi Godauni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimekuwa nikieleza katika majibu yangu kwamba Serikali imeandaa mkakati wa miaka mitano wa kuyafikia maeneo yote nchini ambayo yana changamoto ya mawasiliano. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge katika mkakati wetu wa miaka mitano maeneo yake hayo pia tutayafikia, lakini kwa sababu ameeleza kwamba ana changamoto kubwa, tutayapa kipaumbele wakati wa kutekeleza mkakati wetu huu wa Serikali, ninakushukuru.
MHE. RASHID M. MTIMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Halmashauri ya Mji wa Newala ni miongoni mwa halmshauri ambazo mikopo hii hupitia benki ya NMB. Upatikanaji wa mikopo hii kupitia benki ya NMB umekuwa wa shida sana mpaka sasa vijana, wanawake na walemavu kutoka Halmashauri ya Newala Mji, bado kuna ugumu sana wa kupata mikopo hii.

Mheshimiwa Spika, je, Serikali haioni haja ya kufanya ufuatiliaji na kufanya marekebisho ili kupitia benki hii, basi wananchi hao waweze kupata mikopo kwa wakati? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Newala Mjini. Ni kweli Serikali imeona changamoto: kwa mfano katika mikopo hii ya 10%, tangu tumeanza utaratibu mwaka wa fedha 2024/2025, zile halmashauri 174 ambazo tumeendelea na mfumo wa ukopeshaji kupitia halmashauri, zaidi ya 85% ya fedha ambazo zilitengwa kwa ajili ya mikopo zimeshakopeshwa ukilinganisha na 22% tu ya fedha zilizopitia kwenye benki ambazo zimekopeshwa kwenye halmashauri zile kumi zinazopitia utaratibu wa benki.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni kweli kwamba kuna changamoto ya kasi ya upatikanaji wa mikopo kupitia benki kwa halmashauri zile kumi ambazo ziliwekwa kama pilot ikiwemo na Halmashauri ya Mji wa Newala. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali tayari tumeshakaa na benki husika CRDB, NMB na wadau wengine kuona namna nzuri ya kuongeza kasi ya kutoa mikopo hii. Pia kuona namna nzuri ya kupitia utaratibu ili lengo la Serikali la kuwafikia wajasiriamali wote kupata mikopo kwa wakati ili waendelee na shughuli zao liweze kutekelezwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tutalifanyia kazi na hivi karibuni tutaona matokeo makubwa na mabadiliko makubwa kwa halmashauri zote kupata fedha za mikopo mapema na wajasiriamali kunufaika mapema zaidi.