MHE. SELINA H. KINGALAME aliuliza: -
Je, Serikali haioni haja ya kuanzisha Mfumo wa Elimu ya Vitendo (Internship) kwa kada nyingine za elimu, kama ilivyo Elimu ya Utabibu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, ninaomba nijibu swali la Mheshimiwa Selina Henry Kingalame, Mbunge wa Viti Maalumu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa mafunzo kwa vitendo (internship) katika kuimarisha ubora wa wahitimu. Kwa sasa Serikali kupitia vyuo vya kati na vya elimu ya juu, imeweka utaratibu wa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi, ambapo uendeshaji wake hutofautiana kulingana na kada na mahitaji ya taaluma husika kwa kutumia mfumo wa field practical na industrial trainings.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, Serikali inaendelea kuboresha miongozo ya mafunzo kwa vitendo, ili kuongeza tija na kuhakikisha yanaendana na mahitaji ya soko la ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, katika kada ya ualimu, Serikali imeandaa Kiunzi cha Kitaifa cha Mafunzo ya Ualimu kwa Vitendo (National Teachers’ Internship Framework) cha Mwaka 2026 ambacho kitatekelezwa kwa mtindo unaofanana na kada ya utabibu na kinatarajiwa kuanza katika mwaka wa masomo 2026/2027. Hivyo, Serikali itaendelea kuboresha mfumo wa utoaji mafunzo kwa vitendo kadiri itakavyoonekana inafaa.
MHE. SELINA H. KINGALAME aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaajiri wahitimu wahadhiri wa vitendo wanaojitolea sehemu za ofisi na vyuo hasa waliojitolea kwa zaidi ya mwaka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Selina Henry Kingalame, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma, Toleo la 2 la mwaka 2008, ikisomwa pamoja na Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura 298, ajira katika utumishi wa umma hupatikana kwa ushindani na uwazi. Kwa kuzingatia kuwa kuna vijana wanaojitolea katika sekta ya elimu na sekta nyingine za umma, Serikali ilitoa mwongozo wa kujitolea wa mwaka 2025 ili kuwezesha vijana kujipatia ujuzi wa ziada pamoja na kuwapa uzoefu na uwezo wa kushindana pindi ajira zinapotangazwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa upatikanaji wa walimu wa vyuo yaani wahadhiri, Serikali na vyuo vikuu imeweka utaratibu maalum wa kuwabaini, kuwabakiza na kuwajengea uwezo vijana wanaohitimu na ufaulu mzuri unaokidhi vigezo vya kuajiriwa kama wanataaluma katika vyuo husika. Aidha, vijana hao wanajengewa utamaduni wa kufanya kazi katika mazingira ya kitaaluma kwa utaratibu wa mikataba, ahsante.