Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Aisha Msantu Mduyah (2 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. AISHA M. MDUYAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Ikiwa mara yangu ya kwanza kuchangia katika Bunge hili Tukufu, ningependa nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyeniwezesha kufika siku hii ya leo, nami jina langu limeandikwa katika Orodha ya Wabunge wa Bunge la Kumi na Tatu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ninapenda kumshukuru sana Mwenyekiti wangu wa Chama Cha Mapinduzi, ambaye ni Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na vikao vyake vyote vilivyopita vya kuniteua mimi kugombea, lakini pia kuniteua kuwa Mbunge wa Viti Maalum ninayewakilisha watu wenye mahitaji maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bila kuwasahau nipende kuwashukuru wanawake wote ambao ni Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa UWT – Taifa chini ya Mwenyekiti wetu, mama yetu kipenzi, Mary Pius Chatanda kwa kunikopesha imani yao ndani ya hii miaka mitano 2025 - 2030 na ninachoweza kuahidi kwao ni ushirikiano uliotukuka katika utekelezaji wa Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niishukuru familia yangu pamoja na marafiki zangu ambao wamehakikisha kwamba ndoto zangu haziwezi kukwama mahali popote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwa ninaelekea katika kuchangia hotuba hii, ninapenda kuipongeza Wizara ya Nishati: Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Menejimenti ya Wizara, pamoja na taasisi zote zilizoko hapo chini ya Wizara ya Nishati kwa juhudi kubwa wanazoziweka katika kuhakikisha kwamba Taifa letu linasonga mbele kwenye sekta ya nishati. Tunaona REA wanavyoweka juhudi zao kubwa katika kuhakikisha kwamba vitongojini pia tunapata umeme na wameweza kuanza na vitongoji 9,009. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona pia Serikali yetu namna ambavyo hailali usiku na mchana kuhakikisha kwamba mafuta siyo kikwazo katika nchi yetu na kuhakikisha pia masuala ya kiuchumi na kijamii hayakwami kwa kigezo cha mafuta. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda pia kuipongeza Wizara yetu kwa kuendelea kuibua vyanzo mbalimbali vya nishati. Tunaona nishati ya jua, nishati ya umeme wa maji, lakini pia gesi asilia na joto ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwa ninaelekea katika kuchangia hotuba hii nikianza na suala la nishati safi, sisi kama Taifa kwanza tunajivunia kuwa na kinara wetu wa masuala ya nishati safi ambaye ni Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hata jana tu tumeona akitoa mitungi ya gesi kwa mama lishe na baba lishe Jijini Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili ninaipongeza pia Wizara kwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi, lakini pia kutoa majiko banifu yenye bei ya ruzuku na kuhakikisha kwamba nishati safi inamfikia kila mwananchi. Ninaomba tu waendelee kutoa elimu hii na kuhakikisha kwamba kila mwananchi aliyeko mjini na pembezoni mwa mji anajua umuhimu wa kutumia nishati safi, kwani tukiongelea kuhusu masuala ya athari za mabadiliko ya tabianchi, basi wanawake, watoto, na watu wenye ulemavu huathirika zaidi. Hata takwimu zinatuambia kwamba watu wenye ulemavu wanaathirika mara mbili zaidi kukitokea athari zozote ikiwemo mafuriko, ukame na vitu vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda pia kupendekeza kwamba tuwe na National Clean Cooking Energy Coordination Framework. Leo hii unaweza ukafika ndani ya nyumba moja ya mwananchi ukakuta ana mitungi hata mitano hadi sita ambayo amepewa na watu kadhaa. Amepewa mitungi hii na Mbunge wake wa jimbo, akaja Mbunge wa Viti Maalum akampatia, wakaja STAMICO kupitia mkaa wao mbadala wakampatia na wadau wengine wa nishati safi pia wakampatia, hali ya kuwa jirani yake hana hata mtungi mmoja wa gesi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kukiwa kuna huu mfumo wa uratibu tunahakikisha kwamba wananchi wote wanapata nishati safi, lakini pia upatikanaji wake unakuwa nafuu na pia inawezesha hata wale waliopo pembezoni wanaweza kuji-coordinate kuweza kupata.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hii pia niweze kupendekeza kwamba fursa hizi kama tunavyoona Wizara ya Nishati inavyotoa mikopo, vituo vya mafuta vinajengwa pembezoni mwa miji, basi itoe pia mikopo hii kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, hasa waliopo pembezoni mwa miji waweze kupata mikopo hii na kuweza kuuza nishati hii kwa bei nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ninapenda kuongelea kwenye suala la Local Content. Sisi kama Taifa tunajivunia kuwa na sera hii, lakini pia ni Watanzania wachache sana ambao wanafahamu hivyo. Kwa hiyo, ninapendekeza Wizara iweze kuelezea zabuni ambazo ziko chini yake, ambazo ni specific kwa ajili ya Watanzania. Pia, ihakikishe kwamba wakandarasi hawa wa sekta ya nishati wanahakikisha kwamba zabuni hizo zinaenda kwa Watanzania pekee. Hali hii itafanya uchumi wetu uzidi kukua kwa Mtanzania mmoja mmoja, lakini pia Taifa kiujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwisho, ninapenda pia kuipongeza Wizara ya Nishati kwa kuhakikisha kwamba vijana wanaendelea kupata ujuzi. Tunaona vijana wengi wanaji-engage na miradi ya mikakati ikiwepo wa ECO ambapo wanaenda kupata skills kutoka kwa wakandarasi ambao wako nje. Ninatoa tu wito kwa vijana wenzangu kuendelea kupata ujuzi kwenye sekta ya nishati safi, vijana wote ikiwemo watu wenye ulemavu, kwani tunatambua kwamba mnyororo wa thamani ni mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kuwatia moyo, kwa ni mimi pia hali ya kuwa nina ulemavu, lakini nimesomea Uhandisi wa Mafuta na Gesi. Kwa maana hiyo, vyote vinawezekana kwa vijana wenzangu hasa wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mchango huu mchache nilioutoa na kwa moyo wa dhati, ninaomba niunge mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. AISHA M. MDUYAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii. Ninaanza kwa kuwapongeza Wizara, Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Manaibu Katibu Wakuu, Menejimenti ya Wizara, pamoja na Watumishi wote wa Wizara na Taasisi zake. Kubwa zaidi ninapenda kumpongeza na kumshukuru Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mageuzi makubwa sana aliyofanya katika elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata Sera ya Elimu ya Mwaka 2014, Toleo la 2023, Sera ambayo imeleta maono makubwa katika nchi yetu. Kwanza tumeona tuna Mtaala unaojumuisha masomo ya amali, lakini pia, tumeona tumeongezewa lugha; mbali ya Kiswahili na Kingereza, Lugha ya Alama pia, inatambulika kama lugha rasmi ya kujifundishia na kujifunzia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna lugha nyingine kama brail, pamoja na lugha ya mguso kwa wenzetu wenye uziwi na kutoona; hongera sana na shukrani sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mbali na hiyo tumeona pia, sera imekuja na miongozo minne, ikiwemo Mwongozo wa Shule ya Nyumbani. Ninapongeza kwa sababu, inawapa nafasi wanafunzi wenye mahitaji maalum ambao hawawezi kufika shule nao waweze kupata fursa sawia za kusoma, kama wenzao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa pendekezo katika utekelezaji huu, bado jamii kubwa sana haijaweza kuufahamu huu mwongozo. Tunao wanafunzi wengi wenye mahitaji maalum ambao wako nyumbani, lakini hawapati fursa ya kujifunza. Hivyo basi, ninashauri Wizara iweze kuangalia ni kwa namna gani uelewa unazidi kuendelezwa kwa jamii ikiwemo walimu ambao ndiyo watekelezaji, lakini pia, wazazi na walezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hiyo pia, Wizara ione ni kwa namna gani wataweza kuwawezesha walimu hawa usafiri na posho, kwani tunajua mwongozo huu unatekelezwa nje ya muda wa shule. Pia, kwa mapenzi mema ya Rais wetu ameweza kuruhusu wanafunzi kurudi shuleni, wakiwemo wale ambao walisitisha masomo kwa changamoto za ujauzito, tukapata re-entry guideline. Bado uelewa wa mwongozo huu haujafika kwa jamii kwa ukubwa wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona kwamba, kuna urasimu mkubwa sana ambao mabinti hawa wanaupata pindi wanapotamani kurudi shule. Mbali na hapo kwa wale wanaorudi shule bado mazingira ya shuleni hayapo sawa, kuna ubaguzi kutoka kwa wanafunzi wenzao, lakini pia, sehemu salama ambayo wanaweza kuwahifadhi watoto wao kipindi wao wako shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea pia, kuipongeza Wizara kwa nafasi nyingine ambazo wanaendelea kufanya. Ninaomba nichangie pia katika suala la teknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona kwamba, Wizara ya Mawasiliano inafanya kwa ukubwa wake kuendeleza huduma ya internet katika jamii, lakini ninaishauri Wizara ione ni kwa namna gani teknolojia inafika shuleni. Hii itapunguza gharama za uchapaji wa vitabu, wanafunzi watapa vitabu kwa njia ya E-books na pia, itaharakisha upatikanaji wa vitabu hivi, hasa kwa wale ambao wako pembezoni mwa miji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la elimu jumuishi, ninajivunia tumepiga hatua kubwa sana, hasa katika masuala ya miundombinu. Tumeona ni kwa namna gani Serikali inaboresha miundombinu, ninaomba bajeti iweze kuongezwa katika elimu jumuishi, hasa kwenye vifaa saidizi vya kujifunzia na kufundishia. Tuone ni kwa namna gani wanafunzi hawa wanapata vifaa hivi ambavyo vinaendana na uhitaji wao, vifaa ambavyo havitowaongezea wenyewe ulemavu, bali vitawasaidia katika kupata elimu yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa ninahitimisha ninaiomba Serikali, pamoja na kushukuru kwamba, Mheshimiwa Rais ametoa ajira mpya za walimu, lakini pia, ione ni kwa namna gani walimu hawa wanakwenda kuongezwa, hasa walimu wa masomo ya sayansi, masomo ya amali na masomo jumuishi. Hii inaenda sambamba na kuona ni kwa namna gani walimu hawa wanapatiwa mafunzo ya elimu jumuishi ili waweze kwenda kufundisha wanafunzi hawa ambao wengi wao hawana changamoto na wale ambao wana changamoto katika shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia ninaomba kuunga mkono hoja. Ninawatakia Wizara kila la kheri katika utekelezaji wake. Ahsante. (Makofi)