Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Ali Hassan Omar King (3 total)

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kutupa zawadi hii ya uhai na pamoja na kupata nafasi hii ya kusimama hapa kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe shukurani kwanza kwa Serikali, Serikali imefanya vizuri sana na kwa mimi kama ni Mbunge wa kutoka Zanzibar basi ninaishukuru sana Serikali. Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini pia na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar wamefanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajaribu kutaja sekta moja ambayo hii kwa kule kwetu itakuwa imekusanya vitu vingi sana ni sekta ya fedha za nje. Katika sekta hii ya fedha za nje, ninakushukuru sana Waziri, Mheshimiwa Dkt. Madelu hapa pamoja na ndugu yangu Mheshimiwa Hamad Hassan Chande wamefanya jambo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2021 tulianza na mkopo ule wa RCF (Rapid Credit Facility) ilifanya mambo makubwa sana kule Zanzibar, lakini tukaja na ECF tumefanya mambo makubwa sana kule Zanzibar, lakini kuna Boosting Primary Education tumefanya mambo makubwa sana. Isitoshe tokea kimeanza kipindi hicho tukitazama katika GBS (General Budget Support) hakuna mwaka ambao imesita na imekwenda kwa wakati na hiyo imefanyika kwa wakati na imeenda katika kiwango kamili. Kwa hiyo, Mheshimiwa ninakushukuru sana Mheshimiwa Dkt. Madelu na uongozi wote katika kufanikisha mambo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine niipongeze TRA, TRA imekusanya mapato mazuri kama trend inavyoonesha kwamba ilikuwa ikiongezeka hata kuvunja record ya quarter kwamba ziko quarter ambazo zimekusanya vizuri sana katika TRA. Nikushukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Serikali, lakini pia na ndugu yangu Yusuph Juma yuko pale amekusanya na amefanya kazi nzuri sana, ndugu yangu Mwenda. Kwa hiyo, tunawapongeza sana TRA kwa makusanyo mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nitoe shukurani kwa wale watu ambao sasa hivi wananisikiliza ndiyo walionileta hapa, shukurani zangu kwa wananchi wa Jang’ombe (Wapigakura wenzangu wa Jang’ombe) kwa kuniamini kwa kunileta hapa katika Bunge hili nafanya mambo ambao yanaifanya nchi yetu isonge mbele, ninawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru pia, kwa kauli yao ambayo sasa wanasema mzungu wa nne tunaurejesha palepale. Kwa maana ya hiyo huu mzungu wa nne watakuja kuukuta tena katika meza hii kwenye hii mbao utakuwepo kwa mujibu wa maoni ya watu wa Jang’ombe ndiyo yako hivyo. Ninajua inawezekana ikawa wapo wanaopita kunusanusa, lakini tahadhari ninatoa tu kwamba usinusenuse kila kitu unaweza ukaja ukanusa sumu. Sasa ninawashukuru sana watu wangu wa Jang’ombe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ila wamenipa salamu, watu wa Jang’ombe wamenipa salamu hii hapa ambayo nimeiandika na hata ukipata kwenye Mitandao yote ya Jang’ombe utaikuta hii salamu wanasema: “Oktoba Tunatiki”, ila wameniambia nifafanue. Kufafanua kwamba Oktoba Tunatiki, kuna Msemo wa Kiarabu unasema: “Khalif tuarraf”, wewe ukitaka ujulikane upate umaarufu nenda kinyume, khalif tuarraf.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna watu wana khaalif hiki kitu ili wapate umaarufu, natoa kisa kimoja, kuna mtu mmoja aliona mwezi alipoona ule mwezi magharibi ndipo unapoandama akasema mwezi ule umeandama, kwa hiyo yule mtu alipewa sifa na watu wote wakaenda kushangilia pale, sasa pembeni kuna mtu anaitwa Hababel na yeye akaona kwa nini huyu anapewa sifa, akaona na yeye aseme kaona mwezi, mwezi unaandama mmoja tu, akasema na yeye kaona mwezi, lakini kaonesha upande wa kaskazini, anaambiwa Hababel mwezi unakuwa mmoja tu huku kwa nini unatuonesha mwezi, anasema huu mwezi kumbe Hababel alikuwa anataka ule umaarufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umaarufu huu unapelekea kumbe kuna watu wengine inawezekana wakawa hawaoni vizuri, kuna watu wengine wanakuwa wana tongotongo kwenye kope hizi, sasa anapogeukia yeye huwa anaona mwezi, mwezi ni mmoja tu Oktoba, tarehe 25 Oktoba ndiyo mwezi. Sasa kama kuna Hababel ana mwezi unaoandama kaskazini yeye huyo ni mwingine, au hawa waliotaja mwezi kwamba utakuwepo mwezi mwingine, naona labda tongotongo zao, kwa hiyo wananchi wawaone hawa watu ambao wana tongotongo hakuna mwezi mwingine, mwezi ni Oktoba na Oktoba tunatiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa ushauri kwa Serikali. Jana Balozi Mulamula hapa jirani yangu alizungumzia athari ya fedha za nje kutokana na uhusiano ambao tunao wa kimataifa. Sasa alisema kwamba zimeleta athari kwamba fedha hazikuingia, lakini tukakosa tukapata upungufu wa ajira watu 1,200 kutokana na fedha ya USAID.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali yangu au niishauri ikajaribu kufanya utafiti, kuna baadhi ya fedha tunaweza tukaziona kwamba multilateral, lakini kumbe zikawa ni bilateral. Kwa maana gani? Tuna uhusiano na nchi fulani lakini zile fedha zipo katika mifuko mikubwa ya dunia, lakini ule mfuko wenyewe ukawa unachangiwa na nchi moja au ukawa unachangiwa na nchi mbili tu peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tatizo litakalotokea katika ile nchi au kubadilika kwa sera ya ile nchi, au kubadilika kwa uongozi katika ile nchi unaweza ukaja ukatuletea shoti kama hii ambayo tuliyokuja kuiona. Kwa hiyo, ninaishauri Serikali ikajaribu kutizama vile vitu ambavyo tunaweza tukaviona ni multilateral, lakini kumbe ni bilateral kwa sababu mchangiaji ni mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana ukaona kwamba ni international organization, multinational organization, lakini ikaja ikazusha hili tatizo. Kwa hiyo ili kuepuka tusiende huko kwenye kupata shoti za namna hiyo ninaishauri Serikali kufanya jambo hilo, huo ushauri wangu wa kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili, tuna ndugu zetu hawa wa OSHA ambao wanashughulikia usalama na afya katika maeneo ya kazi, hivi sasa hivi mara nyingi sisi Wabunge hupiga makofi sana tukisema tumeondosha kodi ya OSHA, lakini kumbe wakati mwingine tunaikosesha haki ya binadamu kutopatikana. Kuwa na usalama na kuwa na afya katika maeneo ya kazi ni haki ya kibinadamu, kwa sababu pale anaweza mtu akafariki kutokana na mazingira yale ya kazi hapana usalama na wala hapana mazingira ya afya nzuri, pia panaweza pakatokezea jambo lingine likampa mtu ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaishauri Serikali tunasema kwamba Dkt. Kitila Mkumbo akitaja atakwambia investment imeongezeka katika nchi hii, ile huge of investment iliyoongezeka hivyo zile fedha zinazokwenda kule OSHA zinatosha kuja ku-cover haya mazingira? Au wanakuja wawekezaji wanawekeza sisi tunazuia kutoa kodi za OSHA tunasema kwamba tumepunguza halafu tunabakiwa na walemavu na vifo na mayatima au tunapata watu wenye magonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwenda kukagua katika hayo maeneo, hii kodi au hii tozo tuichukulie kama ni haki au niishauri Serikali, basi tuweke percentage ya income tax ambayo inakusanywa iende katika OSHA ili iende ikaondeshe haya matatizo kwa sababu hii ni sawasawa na haki ya binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ninazungumzia suala la kukuza ujuzi lipo kwa Ndugu yangu Mheshimiwa Ridhiwan pia. Suala la kukuza ujuzi kwa soko la nje. Leo Tanzania tuna diplomasia nzuri na nchi nyingine na ile nchi inatamani itoe watu kwetu waende wakafanye kazi kule, lakini hatuna ujuzi wa kwenda kufanya kazi kule. Ninatoa mfano kesi moja, kesi ambayo aliizungumza Waziri wa Mambo ya Nje, tumepeleka watu, lakini watu waliofaa ni watatu katika watu mia na zaidi. Sasa hii tunaondosha fursa, tujaribu kuangalia, kukuza ujuzi kwa ajili ya soko la nje, kwa sababu tumejijenga vizuri kidiplomasia tuitumie hii fursa hata katika kufundisha Kiswahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo bidhaa moja adimu Kiswahili lakini pengine inawezekana uwezo au ujuzi wa kwenda kuifundisha nje haipo vizuri. Sasa tujaribu kuangalia katika sekta hizi ili tuweze kuingiza mapato kwa wingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni upotevu wa mazao na hili ninakusudia kwa Dkt. Kitila Mkumbo ni la kilimo hili. Tumewekeza matrilioni ya pesa kwa pamoja katika miaka michache. Tumetoka kwenye bilioni 200 tumekwenda mpaka kwenye trilioni, inafika wakati wa mavuno tunaweza tukapata majanga tunaita ya mvua na wavunaji inawezekana sasa wasipate mazao, kwa nini tusiwekeze watu waweze kuvuna hata kama kuna mvua, Serikali yetu inaweza kwa sababu tulishawekeza kwenye kilimo, tulishawahamasisha watu walime, lakini je, tunayo mipango endapo yanatokezea maafa, pamoja na maafa hayo lakini wakulima wetu waweze kulima wapate kile kitu, vinginevyo tukiweka mbadala wa kulipa ruzuku kwa majanga kama haya itakuwa siyo vizuri kuliko tukamwezesha huyu mkulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ninazungumzia ajira kwenye michezo. Michezo inaajiri sana, turudi kule zamani, uwekezaji sasa umepungua katika taaluma ya michezo. Zamani ukimgusa kocha utaambiwa kasoma Ujerumani, kasoma Brazil, kasoma wapi, kwa hiyo hata timu zetu za Taifa zikiongozwa ingawaje sasa hivi zinaongozwa na watu wa hapa si wageni, lakini tujaribu kuangalia kwamba sisi timu zetu hizi kubwa kubwa tuna-import makocha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa je, hatuwezi kupata makocha wa kwetu? Kwa hiyo, taaluma kwenye michezo imepungua. Tujaribu kufanya kwa makusudi watu wapate taaluma ya michezo ili tusi-import hawa makocha na watatusaidia kuzalisha vipaji vingine. Pamoja na yote niseme kitu kimoja ambacho ninaishauri Serikali Kuu, kwamba wajaribu kuangalia wataalam wa michezo. Wataalam wa michezo wakapokee ushauri wao kwenye biashara kuna Baraza la Biashara moja kwa moja linakutana mpaka na Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huku tunajua lipo Baraza la Michezo lakini lipo zaidi kama baraza lenyewe, sasa tunataka hawa wataalam wa michezo wapo wataalam wa michezo wamehusika mpaka kwenda kupata ule uwanja wa Arena wa Rwanda, baadhi ya washauri wametokea hapa hapa kwetu Tanzania. Kwa hiyo, ninaishauri Serikali, ijaribu kukaa na wataalam wa michezo wapate ushauri, hawa wataalam wana mambo mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja na ninasema kwamba ninaunga mkono mia kwa mia, ninashukuru sana kwa nafasi. (Makofi)
Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kupata hii nafasi, pia ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniweka hai na kunijalia siku ya leo kusimama katika Bunge hili Tukufu kuweza kuandika mipango au kutoa ushauri na maoni juu ya uandikaji wa mipango ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila Mbunge aliyesimama hapa, wengi miongoni mwao walikuwa wanaonesha wasiwasi juu ya utekelezaji wa mipango hii au mpango huu, mwisho amesimama Mheshimiwa Waitara naye pia ameonesha wasiwasi juu ya utekelezaji wa mpango huu. Kamati ilishauri na mimi ninaongezea kushauri, kwa nini tusiweke sheria ya kutekeleza huu mpango?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tunapopitisha bajeti tunakuwa tuna The Appropriation Act na tunakuja tunaihoji Serikali juu ya utekelezaji, tunakuja hapa baada ya miezi sita kwa mujibu wa sheria ya bajeti tunakuja kufanya, kama kunafanyika mid-review basi Serikali inatupa habari kwamba kitu gani kimefanyika. Kwa hiyo, ninaunga mkono kwanza wazo hilo la Kamati, lakini ninatia mkono zaidi kwamba huu mpango basi tugeuze iwe sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nichangie katika ugharamiaji wa mpango, katika ugharamiaji huo tumesema kwamba sekta binafsi itachangia 70%, nilitamani zaidi Wabunge tungejadili huko kwenye hizo 70%, niseme tu Serikali wajiandae kuwa na vivutio vizuri kwa sekta binafsi za ndani na nje ili mpango huu utekelezeke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa ushauri huo tu sitaki kwenda mbali katika hizi 70%, sekta ya umma ambapo Serikali yenyewe itagharamia mpango huu kwa 22%, lakini ugharamiaji mzima wa mpango ni sawasawa na dola trilioni 3.6 approximately. Sasa nitachangia juu ya uchangiaji wa Serikali katika mpango huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango huu Waziri amesema kuwa Tanzania kupitia Benki Kuu tutaendelea kununua dhahabu, sasa nami hapa hapa katika kugharamia mpango huu tunaweza kupitia hii kwenye kugharamia dhahabu tukapata fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhahabu huwa tunaitumia kuweka reserve (federal reserve) ya nchi, kwa hiyo inatusaidia sometimes percentages tunayoamua kuiweka inatusaidia kuingiza katika reserve kwa sababu Serikali yetu au Benki Kuu huwa inafanya portfolio ambayo wenyewe wanaita strategic reserve allocation. Inawezekana wakaweka katika Dola asilimia fulani, katika Euro asilimia fulani, katika Yuan asilimia fulani na katika dhahabu tumeweka asilimia fulani. Tumeanza kuweka kwenye dhahabu ambayo ndiyo ninaizungumzia asilimia tano, lakini tukawa tunaendelea tunaanza kuweka 10% na huenda tukazidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoweka vizuri tukizidi kwenye reserve, yale matumizi yetu ya miezi minne ambayo sasa hivi tuna miezi 4.9 tunapata kuwa na special drawing rise kubwa ambayo supplementary au ziada ya kile kilichowekwa tunapata kukopa kitu ambacho kinaitwa concessional loans. Mikopo ambayo pengine unaweza ukaipata hata chini ya asilimia moja hiyo ni financing ya kwanza, ni kwa sababu tumeweka dhahabu, hiyo ni financing ya kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Financing ya pili, tunaweza tukaweka hiyo dhahabu ambayo ziada yake dhahabu hiyo ambayo tukiisha kuweka tunaweza ikiwa nyingi, tunaweza tu tukasema kwamba tuweke dhamana tukapata fedha kwa kuweka ile dhamana, fedha zile zinaweza zikaja kwenye miradi na huu utaratibu siyo wa kigeni, siyo mgeni duniani utaratibu huu, utaratibu huu upo na uko katika mfumo wa international bullion system.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wanaojua waangalie wataona, sasa tukiweka dhamana dhahabu zetu katika kiwango ambacho kinakubalika tutapata fedha. Jambo la tatu, tunaweza tukaweka dhahabu nyingi na kiwango kile ambacho kitakachozidi tunao uwezo wa kuziuza dhahabu zile, au tunao uwezo wa kuweka dhamana tukanunua bond ya Marekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bond ya Marekani sasa hivi ya miaka miwili, sasa imefikia asilimia 3.5. Asilimia 3.5 ni kiwango kikubwa wakati fedha zako ziko palepale zitakuja kutekeleza hii miradi. Pia katika kuweka dhamana wanaku-charge asilimia mbili, utakapokuwa-charged asilimia mbili kwa dhamana ina maana ukipata 3.5, 1.5 ni faida na fedha zako ziko palepale, lakini umepata faida. Kwa hiyo, kila tukiweka dhahabu kwa wingi tunapata faida zaidi pia kiwango cha dhahabu kinachozidi tunaweza hata tukauza halafu tukanunua tena, si tunayo wenyewe hii? Kwa kuwa, tunayo wenyewe leo kitu chako kikikusaidia inakuwa nongwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze ndugu zangu, kuna mtu mmoja kule kwetu, jina lake anaitwa Mbu, Baba yake anaitwa Mbu na Babu yake Mbu, kiufupi ukimtaja majina yake yote anaitwa Mbu Mbu Mbu, alijaribu kujadili mambo haya! Huyo Mbu Mbu Mbu alitaka kujaribu mambo haya, kwa hiyo hawezi kuelewa. Huu utaratibu upo duniani unatumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika ushauri wangu katika sehemu nyingine, ushauri wa Kamati page namba 13 walisema kwamba Serikali iimarishe matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi; lakini wakaeleza kwamba TRA aliomba bilioni 480 kwa ajili ya kuimarisha mifumo. TRA amepewa bilioni 120 ambayo ni sawa 25% kwa ajili ya kuimarisha mifumo. Ina maana hii mifumo inayotumika imeboreshwa kwa 25% bado kwa 75%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishauri Serikali kwamba hebu watoe na hizo shilingi bilioni 360 ili tupate mfumo kamili; kwa sababu kati ya mifumo ilipoimarishwa mfumo mmoja ulioimarishwa ulikuwa huu ni wa IDRAS ambao unashughulikia mapato ya ndani. Mfumo huu umerekebishwa kwa 25% bado ziko modules ambazo zinatakiwa ziingizwe katika mfumo huu ili uweze kufanya kazi kikamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walipotumia fedha hizo 25% pia walirekebisha mfumo ya TANCIS, lakini bado ziko modules zinahitajika ndani ya mfumo huu ili mfumo huu uweze kwenda sawa; na kwa sababu inashindikana hata kufanya comparability, kwa sababu Mfumo wa TANCIS tunatumia kwa East Africa. Sisi hatuwezi kuona ule ulinganifu kama wanavyofanya watu wetu wengine. Huwezi kujua kama umepigwa au umepiga wewe. Tukiuboresha mfumo huu unaweza ukaja ukatufanyia mambo mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tuna mfumo hapa unaitwa ETS (Electronic Tax Stamps) ambao ulikuwa vender wake ni SICPA. Mfumo huu ilikuwa tayari uwe umekwishakabidhiwa Serikalini. Mwaka 2017 wakati mfumo huu anapewa SCPA ilikuwa a-run kwa muda wa miaka mitatu arithishe elimu kwa watu wetu ili uweze kufanya kazi. Sasa hivi bado tunahangaika na kumlipa vender, bado mfumo huu sisi hatujauchukua tunaanzisha na mifumo mingine. Kwa nini mfumo huu usije huku? Ambapo serving yake tutatekelezea miradi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, isitoshe tunakosa mapato kutokana na maeneo tofauti katika nchi katika mipaka. Upande wa nchi jirani wanazo scanners, lakini ukija kwa upande wetu hakuna scanners. Watu wamefanya research wamepita Horohoro hakuna scanners, wamepita Holili hakuna scanner, Tunduma ipo lakini foleni kubwa. Kwa hiyo, inahitajika scanner ziwe nyingi. Pia Namanga kulikuwa bado hakuna scanner na kama itakuwa imechukuliwa ni ndani ya wiki mbili hizi. Niiombe Serikali iangalie utaratibu wa kukusanya mapato. Tukiweka scanners ina maana kwamba mapato yetu hayataweza kuondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine tupime ardhi. Tunayo ardhi nzuri sana. Tutakapopima na kutoa hati tutapokea pango la ardhi. Makisio yanasema tuna uwezo wa kupata trilioni mbili kwa mwaka kwa sababu ya kodi ya ardhi tu. Sasa kwa nini hili Serikali hatuingii tukafanya hivyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo ardhi peke yake; tumetoa mfano, Mji wa Mtumba ule pale. Ninauchukulia ule ni mji wa mfano. Kila kitu chake kimepimwa. Barabara ziko pale. Kila kitu kiko pale majengo yamekaa ukipita unaona raha. Hivyo katika mpango wetu huu wa miaka 25 kutoka 2025 mpaka 2050 tutakaa kwenye makazi hayahaya Mbagala na kwingine huko? Tutakuwa hivi hivi? Ninaomba Mheshimiwa Waziri atuelezee na mpango wa makazi. Tupime ardhi lakini na mpango wa makazi uwepo. Kama hatutakuwa na mpango wa makazi kwamba hii itakuwa siyo nchi inayokua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilizungumzie, tunakua kwa kasi kiteknolojia na kila sekta imetajwa huku inatakiwa ikue; na kwa kuwa kila sekta inatakiwa ikue ina maana tunahitaji elimu ya ufundi. Tunahitaji kuwa na skills ili tuwe na kilimo kizuri. Kila mmoja aliyelalamika hapa kuhusiana na mbegu zile ni skills. Watu waliolalamika hapa kutokana na viwanda, tunakosa skills. Tumesema kwamba foreign direct investment itakuwa 57%. Watakuja watu wa nje lakini je; raw materials tutakuwa nayo, sawa; lakini watakaoajiriwa pale ni akina nani? Kama wasipoajiriwa watu wenye skills ina maana kwamba tutapoteza na huu uchumi wetu pato lile tutaingia wasiwasi kulipata. Ninazungumzia kwenye skills, mfano China watu wanafuata skills, raw materials zipo, ukitaka za viwanda zipo, ukitaka za kilimo zipo, lakini wanafuata skills. Skills zinazopatikana pale ndiyo maana wanakuwa wako competitive katika dunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimechukua muda wako mwingi unisamehe, lakini huu ni ushauri. Huu mpango unawezekana kabisa kutekelezeka na unatekelezeka, GDP iliyokusudiwa inapatikana, per capita inapatikana. Ikiwa tutawekeza kwenye ujuzi tuwekeze mapema maana ni wa miaka 25. Kwa hiyo, tusije kuwekeza mwaka wa mwisho. Tuwekeze mwanzo; tukiwekeza mwanzo productivity itakuwa ni kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka, 2025
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza, shukrani za dhati nitoe kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ametupa uhai na leo hii kuja kujadiliana kuhusiana na maslahi na uendeshaji wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru wewe kwa kunipa hii nafasi ili niweze kuchangia mchango wangu huu. Nitachangia katika hoja ambayo ameizungumzia Mheshimiwa Kakoso, ambayo ni Treasury Register Act, Chapter 370 ambayo inazungumzia remittance of fifteen to sixty percent to the consolidate fund.

Mheshimiwa Spika, katika mchango wangu kwanza ninaunga mkono maoni ya Kamati yote ambayo wameyatoa katika sehemu hii, ambapo Kamati wameeleza kwamba hii haitakuwa sawa kuwepo hapa au kufanyika hivi na ninasema vilevile haitakuwa sawa kufanyika hili, kwa sababu ukitoka fifteen to sixty percent ina maana kwamba ni four hundred percent umeongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haidhuru kwamba tumesema between, sasa hatujui nani atakuwa yuko kati, nani yuko mwanzo, nani yuko mwisho na hofu yangu tukiiacha hivi tukiondoka tulishawahi kupitisha kitu hivi in blanket, sasa huko mbele hiyo Kanuni hatujui nani atakuja kupigwa kwenye sixty, nani atakwenda kwenye fifty, nani anatakwenda kwenye forty, ingawaje kwamba kuna neno limesemwa kule mwisho as determined by Public Finance Act. Sasa kule kwenye Public Finance Act sijaona kama kuna kifungu labda kimeelezea kitaendaje endaje, hilo moja.

Mheshimiwa Spika, wasiwasi wangu ni upi? Wasiwasi wangu ni kwamba tutazinyima kampuni hizi ukwasi na ukwasi wenyewe hapa kwa sababu imesema monthly remittance, kwa kuwa ni monthly remittance ina maana kwamba hizi kampuni zitakosa kufanya zile short term obligation zao. Sasa tukiwanyima ukwasi maana yake hapa hatuzungumzii mikopo mikubwa ambao wanatazama solvency ya company, lakini hapa tunazungumzia kwamba short term obligations zinaweza zikaja zika-fail. Kwa maana hiyo, ile smooth operations za hizi taasisi itakuja kuwa ngumu. Sasa hilo mimi nalisema ili tujaribu kuangalia na tutazame Kamati ilipotushauri ili tuende na ushauri wa Kamati.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Shamsi pia alisema hapa kwamba je, hizi kampuni zilivyowekwa kwamba ziwe zinaongozwa ziwe public companies, Je, tulikuwa tunaangalia mapato au tuangalia maslahi mapana ya Taifa? Katika bidhaa kuna vitu vinaitwa public goods, public goods nyingine huwezi ukazipeleka katika private sector, ni lazima ziendeshwe na public sector inavyofanya zile kazi zake wakati mwingine kwamba wanaangalia maslahi mapana ya Taifa, kwamba nini kitatokezea kule, hili ninaona kwamba tuliweke katika kipaumbele ambayo yalikuwa ni maoni ya Mheshimiwa Shamsi Vuai. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tujifunze Waswahili tunao msemo tunasema, ukupigao ndiyo ukufunzao, maana kama haujakupiga hauwezi kukufunza, lakini hebu tujifunze. Bunge la Kumi na Moja tulisema hapa TANAPA, Ngorongoro wanapata mapato makubwa wana matumizi mabaya, pesa zao ziende Mfuko Mkuu, tukapeleka malalamiko tumeona, leo sheria imekuja imefanya nini? Inapunguza.

Mheshimiwa Spika, tulikuwa hapa tuna-export levy ya korosho tulisema yote iende Mfuko Mkuu wa Serikali, ndugu zangu hapa wa Kimakonde wakasema sana kwa korosho yao, iende Mfuko Mkuu wa Serikali, badala yake leo hii tunatoa tunasema kwa miaka minne Kamishna akikusanya apeleke wapi, katika Bodi ya Korosho. Kwa sababu umetupiga, Je, hatujifunzi huu uliotupiga? Maana ukupigao ndiyo ukufunzao.

Mheshimiwa Spika, sheria hii ya leo tunayotaka kuipitisha imepunguza hayo makali, lakini imekuja kuongeza makali katika hizi kampuni nyingine. Kwa hiyo ninaomba tujifunze na hili, tusipojifunza maana yake ni kwamba tunaweza tukapata kama haya ambayo yalitutokea.

Mheshimiwa Spika, tufanye nini basi? Kama tunahisi hayo mapato yanavuja, hayapatikani ipasavyo, zipo kule bodi na bodi uteuzi wao ni Rais. Waziri, hizi bodi basi tuweke watu competent waweze kusimamia, watakavyosimamia haya yatakwenda vizuri kwa sababu ndiyo tayari zile bodi tumeziamini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine, kwa kuwa Kamati hapa sasa imeleta schedule of amendment, ninaomba Serikali ikubali hii schedule of amendment ya Kamati kwa sababu Kamati imeona na haya kihistoria yametokezea hapa. Kuna theory ya pesa za mtoto kukamatwa na mzee, zote tunajua hapa. Theory ya pesa za mtoto kukamatwa na mzee; mzee mara nyingi sana akikamata pesa za mtoto akimwambia nitakupa kila baada ya mwisho wa mwezi, sio rahisi mzee yule kila mwisho wa mwezi zile pesa akazitoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulishafanya kwenye property tax hapa na hazikwenda. Mzee akifika tu siku atakuja kusema hizi nisubiri kidogo, nisubiri; tutaua mashirika maana Consolidated Fund ndiyo mzee, lakini hii Mifuko ya huku ndiyo mtoto. Zikikamatwa pesa huku tutakuja kuua.

Mheshimiwa Spika, pamoja na yote ninatoa shukrani; hii changamoto isingetokea bila kwamba haya makusanyo yameongezeka. Kwa hiyo, niipongeze Serikali kwamba mapato kumbe yameongezeka sasa tunatafuta njia ya kudhibiti. Sisi kama Wabunge njia ya kudhibiti tunaona sio hiyo, tupite hii njia ambayo Kamati imetushauri. Hii njia iliyotushauri Kamati itakuwa ni salama kuliko njia hii kwa sababu hapa tayari tunazo reference ya sheria tulizozipitisha hapa hapa kwenye Finance Act, lakini badala yake tukaja tuka-review tukarejea.

Mheshimiwa Spika, ninaunga mkono hoja mia kwa mia na ninashukuru kwa nafasi. (Makofi)