MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: -
Je, kwa nini Serikali isiyondoe mfumo wa wanafunzi kurudi mchana kula nyumbani na kurudi tena shuleni ili kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Jimbo la Rorya, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa mitaala ya elimu msingi na sekondari, wanafunzi wanapaswa kusoma vipindi sita hadi nane kwa siku kwa shule za msingi, na saba hadi kumi kwa shule za sekondari, kutegemea na ratiba ya siku. Katika kutekeleza takwa hili, halmashauri zimekuwa na ratiba ya watoto kurudi nyumbani kupata chakula na kurudi shule kumalizia vipindi. Aidha, halmashauri nyingine wanafunzi hukamilisha idadi ya vipindi bila kurudi nyumbani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia Waraka Namba Tatu wa Mwaka 2016 kuhusu utekelezaji wa Elimu Bila Ada, Mwongozo wa Kitaifa wa Utoaji wa Huduma ya Chakula na Lishe Shuleni wa Mwaka 2021 na Mpango wa Utekelezaji wa Mwongozo wa Kitaifa wa Utoaji wa Huduma ya Chakula na Lishe Shuleni wa Mwaka 2023 Serikali kwa kushirikiana na wazazi imeweka utaratibu wa kuhakikisha kwamba kila mtoto anapata chakula shuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia kuwa hali ya upatikanaji wa huduma ya chakula shuleni inatofautiana kati ya halmashauri moja na nyingine, Makatibu Tawala wa Mikoa wanaelekezwa kufanya tathmini ya utekelezaji wa utoaji wa huduma ya chakula shuleni katika mikoa yao ili kuondoa ratiba ya wanafunzi kurudi mchana kula nyumbani na kurudi tena shuleni.