Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. MORRIS J. MAKOI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ninaomba nikushukuru wewe binafsi, lakini kwa vile ninaongea hapa kwa mara ya kwanza kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Moshi Vijijini, ninaomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Nimshukuru pia Makamu wa Rais, lakini na Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kazi kubwa wanayofanya kuhakikisha nchi yetu inasonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba pia nichukue nafasi hii kumshukuru Waziri wa Kilimo, Naibu Waziri, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na timu yao yote, bila kumsahau Mkurugenzi Mkuu wa COPRA na Mkurugenzi wa Wizara ya Kilimo wa Mazao Mchanganyiko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu ninalotoka la Moshi Vijijini na Vunjo, kilimo kikubwa ambacho kimesaidia wananchi miaka mingi ni kilimo cha kahawa, lakini katika miaka ya hivi karibuni kilimo kile ni kama kimepewa kisogo na ninaona hata Wizara ya Kilimo na wenyewe kama wamekaa pembeni kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaendelea ninaomba kabisa kwa ruhusa yako nimwombe Waziri wa Kilimo na timu yake ya Wizara watusaidie Wilaya ya Moshi, Jimbo la Moshi Vijijini na Vunjo, waweze kurejea tena kwenye kilimo cha kahawa kwa sababu ndiyo njia pekee ya kujipatia riziki na kipato kwa wananchi wa Majimbo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sasa pamoja na kwamba Wizara imetusaidia hivi karibuni kupata miche ya kahawa, ninawaomba waendelee kuongeza nguvu kwa sababu wananchi wale sasa wamekubali kurudi shambani ili wazalishe upya kahawa baada ya kugundua kwamba bei imekuwa kubwa na wamegundua kwamba Mheshimiwa Rais Samia ana nia ya dhati kabisa kuwezesha wakulima wote ambao wana nia ya kuzalisha mazao ya biashara hususan zao la kahawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama unavyojua kule kwetu Kilimanjaro, Chama Kikuu cha KNCU ndicho ambacho kilichochea vyama vingi vya msingi na wakulima kujiondoa kwenye kulima kahawa kutokana na madeni mengi ambayo chama kile kimeshindwa kuwalipa vyama vya msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba nimepata hakikisho la fedha zinazodaiwa kulipwa, lakini ninataka niweke kumbukumbu sawa kwenye Bunge hili kwamba, Chama Kikuu cha Ushirika KNCU wanadaiwa na vyama 40 kutoka Jimbo la Moshi Vijijini na Jimbo la Vunjo jumla ya shilingi milioni 800 na kidogo. Uhakiki uliofanyika karibuni unaonesha kwamba hizo fedha ni za msimu wa 2010/2011- 2012/2013 mpaka karibu 2016 zilikuwa hazijalipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, unaweza kuona jinsi gani hali hiyo imechochea umaskini, kukata tamaa kwa wakulima na hali nyingine ambayo kwa kweli kumshawishi mtu arudi shambani alime kahawa imekuwa ni ngumu, lakini wananchi wale sasa wapo tayari baada ya kupata hakikisho kwamba fedha zile zitalipwa kupitia Mkurugenzi wa TCB. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niongelee ushirika: ushirika nayo imekuwa ni changamoto kubwa sana katika Wilaya ya Moshi; majimbo mawili Vunjo na Moshi vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushirika wameshindwa kabisa kurekebisha sheria ambayo itawezesha wale ambao wachache wanaotumia fedha za wananchi vibaya waweze kukumbwa na mkono wa sheria. Kwa hiyo, kule Moshi SACCOS nyingi ambazo zilikuwa zimeanzishwa na wakulima ama zimefilisika, ama zimefilisiwa na wale viongozi na hakuna hatua zozote ambazo zimechukuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba Mheshimiwa Waziri, atakapokuja kufanya majumuisho, aniambie na awaambie wananchi wa Moshi Vijijini kupitia Bunge hili ni hatua gani watachukuliwa wale ambao wamekula fedha zao kutoka kwenye baadhi ya Vyama vya Msingi na SACCOS ambazo zilikuwepo na ambazo zilikuwa zimeenda vizuri na zilikuwa zinatoa tija kubwa sana kwa wale wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, niombe nizungumzie habari ya upatikanaji wa mbolea. Ninaomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mkurugenzi wa… eeh...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Makoi.
MHE. MORRIS J. MAKOI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. MORRIS J. MAKOI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Ninaomba nichangie katika eneo la uangukaji wa taaluma kwenye elimu ngazi ya chini kwa sababu, ninaona wachangiaji wengi wameongea zaidi katika ngazi ya juu, ambayo Waziri, Mheshimiwa Mkenda, anaisimamia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuwe na wanafunzi wenye elimu nzuri katika shule za sekondari na vyuo ni lazima tuangalie taaluma katika ngazi ya chini kuanzia shule ya msingi mpaka, pengine form four, form five na form six.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika shule zetu za sekondari za Kata nyingi kwa kweli taaluma inaanguka sana kutokana na ukosefu wa ufuatiliaji wa wale Waratibu Elimu na wale wengine ambao wanatakiwa kusimamia elimu katika ngazi hiyo. Kwa hiyo, ninaomba nimwambie Kaka yangu Waziri Profesa Mkenda pamoja na kazi kubwa sana ambayo anaifanya, pamoja na uwekezaji mkubwa sana ambao Rais Samia Suluhu Hassan amewekeza, bado kuna kazi kubwa sana ya kuangalia ngazi ya chini ili tuweze kwenda sambamba na malengo ambayo tunayatarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko changamoto katika upande pengine wa mitihani ya darasa la saba, ambapo wanafunzi darasa zima wanaambiwa kwamba wame-pass na wanakwenda kujiunga na form one, lakini ukifuatilia wakati mwingine ukiwakuta form two kuna mwanafunzi ambaye hajui kusoma na kuandika. Sasa, katika mazingira haya huko mbeleni tunakwenda kutengeneza watu ambao hawawezi kuleta tija na pengine kutuletea matokeo ambayo tunatarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninamwomba Waziri, pamoja na kwamba hili eneo pengine ni la TAMISEMI, lakini kama Wizara zinatakiwa zisomane, kwa sababu TAMISEMI wanamtengenezea ngazi ya chini na yeye anatengeneza ngazi ya juu, kama wanasomana wanaweza wakatengeneza wanafunzi ambao wanaweza wakaleta matokeo ambayo pengine tunayatarajia ama tunayahitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni chakula, ninapenda kuzungumza habari ya upatikanaji wa chakula kwenye shule zetu kuanzia shule ya msingi na hata sekondari zetu hasa za Kata. Kumekuwepo na utaratibu wa Serikali wa wananchi ama wazazi kuchangia mchango wa chakula katika shule zetu. Katika hili jambo maelekezo yanayotolewa na Serikali lakini yamekuwa hayana nguvu sana, kwa hiyo kumekuwa na changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa vyakula katika shule za msingi na sekondari katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile Wakurugenzi hawawajibiki kuingilia au kufuatilia, wanafunzi wengi wamekuwa wakikaa wakiteseka na njaa na mwanafunzi yeyote ambaye ana njaa hawezi kujifunza na kuweka kitu kichwani. Ninatoa ushauri, kama itampendeza Waziri na anaweza kushauriana na Waziri wa TAMISEMI, kuna baadhi ya shule ambazo zina mashamba ama ardhi ya kutosha ambayo inazunguka shule, basi, Serikali ingeweza kuweka utaratibu yale mashamba yakalimwa rasmi kwa ajili ya kusaidia uzalishaji wa chakula kwa wanafunzi wa zile shule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inaweza kusaidia kupunguza gharama ya michango kwa wazazi kwa mfano, kama mzazi alikuwa anachangisha shilingi 100,000 kwa msimu, anaweza akachanga labda shilingi 20,000 ambayo inaweza ikawa rahisi kuipata, hasa wale wananchi wa maeneo ya vijijini. Uko utaratibu ambao mwanafunzi kabla ya kujiunga anatakiwa kuchangia moja kwa moja kwenye ile fomu anapojiunga shuleni, siyo wazazi wengi ambao wana uwezo wa kuchangia moja kwa moja, wengine wanashindwa kuchanga, lakini Serikali inaelekeza kwamba wanafunzi wote wawe darasani ama awepo shuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo walimu wakuu wanatii yale maelekezo, lakini mwishoni mwa siku kunakuwa na wanafunzi waliolipa na ambao hawakulipa. Kwa hiyo, kinachotokea ni kwamba, chakula kinanunuliwa kinatumika, kikiisha wanafunzi wanabakia hawana chochote, kwa sababu wale walioshindwa kuchangia mchango wao haukupatikana, kwa hiyo, kama kuna uwezekano basi mashamba ya shule yangetumika kusaidia kupunguza tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali inaweza kuweka utaratibu maalum ambao zile fedha zinaweza zikalipwa pengine kwa control number au moja kwa moja kwa Mkurugenzi na Mkurugenzi akawajibika kuhakikisha kwamba wanafunzi wanapata chakula shuleni wakati wote, kuepusha kuunda Kamati za Vyakula za Shule ambazo na zenyewe zinasemekana kwamba zinajihusisha na uharibifu wa fedha na vyakula ambavyo vinapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo niongelee uchakavu wa miundombinu wa shule zetu za msingi na sekondari. Ninaomba nitoe shukrani nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri Profesa Mkenda kwa kazi kubwa ambayo imefanyika katika Halmashauri ya Moshi, kwa ukarabati wa shule mbalimbali za msingi na sekondari na nyingine zimejengwa upya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyojua shule nyingi za msingi na sekondari katika Wilaya ya Moshi zimejengwa miaka mingi zaidii ya miaka 50, zote zimefikia mahali zimekuwa na uchakavu wa wakati mmoja, kwa hiyo, ninaomba Waziri anapokuja kuhitimisha atuambie ni mpango gani, mkakati gani upo wa kuhakikisha shule zote za msingi au sekondari ambazo ni chakavu zinaboreshwa, kwa sababu Serikali imepeleka fedha imejenga baadhi ya madarasa na baadhi ya shule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unakuta tumekuwa kama tuna ubaguzi. Wapo wanafunzi wanaosoma kwenye vyumba vizuri na wanaosoma kwenye vyumba vya zamani ambavyo vingi vinavuja. Sasa, inakuwa kama pengine inakuwa ni ubaguzi na wale wanafunzi wengine wanaona kama wamepewa madarasa mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba wakati Waziri anakuja ninamwomba sana na ninajua anatoka Kilimanjaro, anafahamu hali ilivyo kule, atuambie Serikali inatusaidiaje kwa kweli katika hii hali kwa sababu ni jambo ambalo limekuwa sugu na tumejaribu kuangalia njia mbalimbali za wafadhili, wanatusaidia lakini bado tatizo ni kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji kabisa nguvu ya Serikali na nguvu ambayo inahitajika hasa wakati huu maeneo ya milimani mvua nyingi zilizonyesha zimesababisha uharibifu na ule uchakavu umezidi kwa sababu ya mvua ambazo zimenyesha kubwa. Kwa hiyo, ninaomba sana Waziri atakapokuja atusaidie kuangalia hilo jambo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia tuangalie utaratibu wa kuwepo na walimu. Tunajua kwamba ngazi ya sekondari walimu wako wa kutosha maeneo mengi, lakini kwenye ngazi ya elimu msingi walimu ni wachache sana. Unakuta shule moja ina walimu watatu au walimu wawili, unakuja mradi wa ujenzi wa darasa wanateuliwa kusimamia darasa, mwishoni anabakia mwalimu mmoja katika shule, sasa ufundishaji wa namna hiyo hauwezi kutoa matokeo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kama inaonekana kwamba shule ina mradi na hakuna wasimamizi, basi hakuna sababu ya kumteua mwalimu aliyeko pale, ni bora akatafutwa mtumishi kutoka halmashauri akaja kusimamia ule ujenzi ili wale walimu wachache wawili watatu waliobaki shuleni waendelee kufundisha wanafunzi badala ya kuwekwa katika mazingira yale ambapo wanafunzi wanabakia kwenda shuleni wanazunguka kuanzia asubuhi mpaka jioni, wanarudi na hakuna ambacho kinaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaomba nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Profesa Mkenda, Naibu wake na wale wote wanaomsaidia katika majukumu haya. ninamshukuru vilevile, Rais Samia pamoja na Wasaidizi wake na hata washauri wake ambao wanamshauri kwa jinsi ambavyo anatusaidia kuhakikisha kwamba suala la elimu limepata kipaumbele na wanafunzi wetu wale ambao wamekuwa katika yale madarasa mapya na shule mpya ziizojengwa wanaendelea kunufaika na mchango huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. (Makofi)