MHE. MORRIS J. MAKOI aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga Barabara ya Mbokomu - Mti Mrefu kilometa 13.94 kwa kiwango cha lami ili kuchochea utalii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Morris Joseph Makoi, Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa Barabara ya Mbokomu – Mti Mrefu katika Wilaya ya Moshi. Katika mwaka wa fedha 2024/25 Serikali ilitenga bajeti ya shilingi milioni 200 kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami nzito (asphalt concrete) mita 200 na tayari zimekamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2026/2027, Serikali imetenga bajeti ya shilingi milioni 225 kwa ajili ya ujenzi ya barabara hiyo kwa urefu wa meta 200.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mahitaji makubwa ya matengenezo ya barabara kiwango cha lami, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kwa awamu, ahsante.
MHE. MORRIS J. MAKOI aliuliza: -
Je, lini Serikali itamrejesha mkandarasi wa barabara ya Moshi International School - Kibosho kwa Rafael yenye urefu wa kilometa 5.49?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Morris Joseph Makoi, Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Moshi International School – Kibosho kwa Rafael, kilometa 7.19, ni sehemu ya barabara ya Kibosho Shine – Kwa Rafael – International School yenye urefu wa kilometa 25.25 ambapo kilometa 18.06 tayari zimejengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali imesaini mkataba kwa ajili ya kazi ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa kilometa 7.19 zilizobaki ambapo taratibu za malipo ya awali kwa mkandarasi zinaendelea ili aweze kuendelea na kazi kwa mujibu wa mkataba, ahsante.