Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Salome Wyckiffe Makamba (5 total)

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, sijafurahishwa sana na majibu ya Serikali kwa sababu shida tunapata sisi. Leo hii kila anayesimama anazungumzia athari zinazotokana na uhaba wa mafuta na bei kupanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu niliuliza, Serikali haioni haja? Angeniambia kama Serikali haioni haja, kwa sababu uwepo wa refinery Tanzania utaongeza ajira, utatupunguzia matumizi ya fedha za nje kununua mafuta, utatuhakikishia usalama wa upatikanaji wa mafuta na kadhalika. Sasa swali langu, angalau angesema watauweka mpango huu katika Mpango wa Maendeleo ya Taifa ili kuweza kuangalia uwezekano.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Je, ni kwa nini hawataki kufanya feasibility study ambayo itaweza kuainisha umuhimu wa uwepo wa refinery, ama isiwepo refinery?
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, tunaielewa concern ya Mheshimiwa Mbunge na tunamshukuru kwa mchango wake katika sekta hii ya mafuta.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la msingi lilikuwa linahusiana na ujenzi wa refinery kwa ajili ya mradi wa bomba la mafuta linalotoka Uganda kuja Tanzania. Nimwambie Mheshimiwa Mbunge, mipango kwa ajili ya kutafuta na kutafiti mafuta na ujenzi wa refinery katika Wizara yetu ipo na utafiti unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi zipo timu ambazo zinafanya utafiti katika maeneo mbalimbali nchini; na mara tutakapopata mafuta ya kutosha na gesi ya kutosha, basi Serikali ipo tayari kwa ajili ya kujenga refinery ili kuweza kuwahudumia Watanzania, kama alivyosema kwamba refinery inatoa ajira, lakini inaleta uhakika wa mafuta ndani ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Kumekuwa na changamoto ya kukatikakatika umeme katika Mkoa wa Simiyu, na Serikali iliahidi kutoa fedha kwa ajili ya kujenga kituo cha kupozea umeme. Je, ujenzi huu umefikia hatua gani? Lini utakamilika ili kuondoa changamoto hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuendelea kufuatilia namna ambavyo Wizara ya Nishati inaendelea kutekeleza majukumu ya ujenzi wa substation katika eneo la Simiyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi inaendelea na mpaka sasa ujenzi wa substation umefika zaidi ya 30%. Ninamwomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira. Ninamhakikishia mara baada ya substation hiyo kukamilika, Mkoa wa Simiyu utakuwa umeondokana na changamoto ya kukatikakatika kwa umeme. Ahsante.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Mosi, je, katika mikataba iliyoingia Wizara ya Nishati, mmezingatia vipi maslahi ya nchi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kupitia mradi huo, Tanzania tutanufaika nini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti ninakushukuru. Kwanza, ninampongeza dada yangu, Mheshimiwa Ester Bulaya kwa kufuatilia kwa karibu juu ya faida za Mradi huu wa Bomba la EACOP kwetu sisi Tanzania. Yako manufaa mengi ambayo Watanzania wameshayapata mpaka sasa hivi. Hivi tunavyozungumza, kipindi cha ujenzi wa bomba hili la mafuta, Watanzania zaidi ya 10,000 wamenufaika kwa ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya Mkoa wa Tanga ambako kimsingi ndiyo bomba hili linapoishia kwa ajili ya kutoa mafuta kupeleka nje, wananchi wale wamejengewa miradi ya maji, wamejengewa miradi ya barabara, wamechimbiwa visima na kama haitoshi, wamefanyiwa mafunzo mbalimbali kwa ajili ya upandaji wa miti na utunzaji wa mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiachana na hilo, Tanzania itanufaika na uwepo wa bomba hili kwa sababu kuna asilimia ambayo nchi yetu itanufaika kama sehemu ya mradi wa bomba la mafuta. Ukiachana na hilo, sisi Watanzania tutapata faida ya kuuziwa sehemu ya mafuta hayo ghafi ambayo yakiwa yameshasafishwa tutayapata kwa ajili ya matumizi ya ndani ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako manufaa makubwa ambayo tunamshukuru Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kukubaliana na Mheshimiwa Rais wa Uganda, waliamua kufanya mradi huu wa kimapinduzi ambao unaenda kutatua changamoto ya mafuta na ya kiuchumi katika nchi yetu.
MHE. KIJAKAZI Y. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini tulimsikia pia jana Mheshimiwa Waziri Mkuu akitoa maelezo yanayofanana na haya. Ningependa kufahamu, au ningependa kuuliza maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mosi, kama ilivyoeleza Serikali kwamba wako kwenye majadiliano ambayo yanaelekea ukingoni kwenda kusainiwa kwa mkataba, je, Serikali imeweka mkakati gani wa kuhakikisha kwamba wanatoa elimu, sambamba na uwezeshaji kwa wananchi wa Tanzania hususan wanawake wa Mkoa wa Lindi pamoja na vijana ili kuhakikisha kwamba wanaweza kuzipata fursa, hususan zile zinahusiana na sheria ya local content ili waweze kunufaika na mradi huu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Mwaka 2023/2024 Wizara ya Nishati iliingia makubaliano na Wizara ya Elimu kupitia Arusha Technical College kwa ajili ya ujenzi wa chuo kitakachofundisha masuala ya nishati na mafuta; na Halmashauri ya Manispaa ya Lindi ilitoa eneo lenye ukubwa wa square meter 256,000 katika eneo la Kikwetu pale Lindi. Kwa mujibu wa makubaliano, ilikuwa ujenzi wa chuo kile ujengwe haraka iwezekanavyo ...

SPIKA: Mheshimiwa twende kwenye swali lako.

MHE. KIJAKAZI Y. MOHAMED: ...lakini mpaka sasa bado ujenzi haujaanza, ningependa kufahamu, je, ni lini ujenzi wa chuo kile utaanza? La, kama Serikali haipo tayari, kwa nini, isirejeshe eneo lile kwa manispaa ili waendelee na shughuli nyingine, ikiwemo kuuza maeneo yale ili manispaa iweze kupata mapato?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Kijakazi Mohamed, almaarufu Binti Lindi kwa kazi kubwa anayoifanya ya kufutilia mradi huu wa LNG. Ninajua kuwa anafanya hivyo kwa sababu anajua kuwa huu ni mradi wa kihistoria ambao ukifanikiwa kuanza mikoa ya kusini itabadilika sana kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza, linahusiana na kuwajengea uwezo wanawake na wananchi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara. Sasa Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, inaendelea kutoa elimu kupitia VETA, SIDO na vyuo vingine, lakini pia kuna ujenzi mkubwa wa shule ya amali unaendelea kwa ajili ya kutoa elimu juu ya namna ambavyo wananchi wanaweza kuchangamkia fursa zitokanazo na mradi huu wa LNG ambao utaanza hivi karibuni.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na chuo cha elimu ya juu ambacho Mheshimiwa Mbunge amekitaja, ni kweli. Kwanza tunawashukuru Wanalindi kwa kutoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa chuo hiki; na hii ni kwamba elimu juu ya uchakataji wa mafuta na gesi bado ni jambo geni kidogo katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, ninawapongeza kwa hilo, na Serikali ina nia ya dhati ya kuhakikisha kwamba chuo hiki kinajengwa ili wananchi waweze kupata ujuzi na kushiriki katika mradi huu wa kimkakati na tutafanya hivyo kwa kadri ambavyo upatikanaji wa fedha utakavyowezekana. Ninaomba kuwasilisha.
MHE. ARIF S. PREMJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Tunaongelea Mradi wa LNG wa shilingi trilioni 100. Chombo cha habari cha Citizen na Reuters ya London vilichapisha habari tarehe 27 mwezi wa kwanza mwaka huu; na kwenye habari hiyo ilimnukuu mmoja wa Waziri akisema kwamba mkataba utasainiwa mwisho wa mwezi wa Sita. Jana tumesikia kwamba kuna majadiliano bado. Je, ni ipi kauli rasmi ya Serikali kuhusiana na kusainisha mkataba huo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa swali zuri la Mheshimiwa Mbunge. Kama ambavyo Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa kauli jana, na kama ambavyo majibu yangu ya msingi ya swali hili nimeyaeleza hapa leo mbele ya Bunge hili Tukufu, mradi wa LNG upo katika hatua za mwisho za kukamilisha makubaliano ya kisheria na ya kimkataba ili waweze kusaini mikataba na kuanza mradi huu.

Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha.