Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Yannick Ikayo Ndoinyo (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. YANNICK I. NDOINYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami nichangie hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu inayoendelea. Nianze kwa kweli kwa kuipongeza sana Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuiletea maendeleo nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza pia, Makamu wetu wa Rais, Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, pamoja na Waziri Mkuu ambaye hotuba yake leo tunaijadili. Kwa kweli, mimi naanza kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu, ameiletea nchi yetu, siyo maendeleo peke yake, bali utulivu na amani ambapo kwa kweli, tunaihitaji na tunaitumia na kwa viwango vyovyote Tanzania ni nchi bora. Binafsi najivunia sana kuwa Mtanzania na kwa kanda hii yote ya Afrika Tanzania ni nchi ambayo inatamaniwa sana na wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaanza, na kwa bahati nzuri, juzi tumepata nafasi ya kuhabarishwa kuhusu kazi za CAG. Mimi nagusia kidogo kabla sijaingia Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba, hiyo ndiyo dalili, ripoti zake zinaonesha uimara wa taasisi zetu za Tanzania na uhuru wa taasisi zinazofanya kazi na ndiyo maana haiingiliwi na anatoa ripoti yake kulingana na maoni yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli, mimi ninataka kuitumia hiyo na Watanzania wafahamu kwamba, taasisi zetu ziko huru kama hiyo na zinafanya kazi kwa uhuru. Tukipata nafasi ya kuchangia tutachangia, lakini hiyo ndiyo sura halisi ya taasisi zetu, ziko huru kwa kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza pia ofisi ya Waziri Mkuu na hotuba yake pamoja na taasisi zote ambazo ziko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, kama TAMISEMI ikiongozwa na Mheshimiwa Prof. Riziki Shemdoe na wasaidizi wake wengine wote, tunawashukuru. Hongereni sana kwa hotuba na plan hiyo ambayo mnayo kwa kweli, ni nzuri. Imeonesha maono, kazi zilizofanyika na maono ya mbeleni kwa mwaka huu tunaouendea na mimi nataka ni-narrow down kwa Wilaya yangu ya Ngorongoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Ngorongoro ni kubwa kushinda mikoa mingi Tanzania, ina kilomita 14,030. Ni wilaya kubwa sana na kwa mgawanyo, inawalazimu watu kutoka tarafa moja kwenda hadi karibu kilomita 300 kufuata huduma makao makuu ya wilaya, ni eneo kubwa sana. Inatakiwa itafakariwe sasa namna ya kugawanya ile wilaya, zipatikane halmashauri angalau mbili, ili watu waweze kupata huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasemea hii kwa sababu, ile wilaya iko pembezoni sana na wilaya nyingine. Ni wilaya peke ambayo haiunganishwi na barabara ya lami na Mkoa wa Arusha. Kwa hiyo, ukichukua hiyo na umbali wa kufikia huduma, kwa kweli, inastahili tuwe na halmashauri pamoja na maeneo mengine mapya ya utawala, ili kurahisisha huduma yetu kwa wananchi. Wananchi wanapotaka kwenda kutafuta vitambulisho vya NIDA, vyeti vya kuzaliwa na vyeti vingine wanalazimika kusafiri umbali mkubwa sana kwenda wilayani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri wewe unaifahamu ile Wilaya, ni ya utalii, lakini kiuchumi pamoja na kwamba, tumegawanyika kiutawala na kiuchumi, ile wilaya imeganyika sehemu kuu mbili; Kusini, ambayo ni ufugaji na utalii na Kaskazini, ambayo ni kilimo, ufugaji na utalii. Mgawanyo huu wa kiuchumi hautumiki ipasavyo kuinufaisha nchi na watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utalii bado ni mdogo sana. Pamoja na kwamba tuna taarifa kwamba makusanyo yake ni makubwa sana kuanzia shilingi bilioni 260 na kuendelea, lakini ukilinganisha na potential ya utalii, bado ni kidogo sana. Mapato yale yanayotokana na utalii. Kwa hiyo, ni rai yangu kwa Serikali kuhakikisha kwamba, inaboresha utalii ulioko ndani ya Wilaya ya Ngorongoro, ili iweze kunufaisha nchi na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, pamoja na kwamba, tunachangia na kuipongeza Hotuba ya Waziri Mkuu na taasisi zake, ni muhimu pia mkazo utolewe zaidi kwa zile sekta ambazo ni za uzalishaji, kilimo na ufugaji kwa maeneo ambayo bado hayajawekewa mkazo wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Wilaya hii ya kwangu ya Ngorongoro ufugaji ni uchumi, lakini pia, ni mila; na kwa sababu, ni mila na Uchumi, ni vizuri kuweka mkazo wa kutosha kuhakikisha kwamba, sekta ya ufugaji inainuliwa, ili kuweza kunufaisha watu. Kwanza yapatikane malisho ya kutosha kwa wafugaji kwa nyakati zote, masika na kiangazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli, Serikali inatakiwa iweke mkakati wa kuhakikisha kwamba, hakuna mifugo ya wafugaji inayokufa kwa kukosa malisho. Mifugo mingi sana inakufa kwa sababu hakuna malisho wakati wa kiangazi, na ni kweli majani huwa yanaisha, lakini uwezekanao wa kuwa na malisho mbadala hatujaufikiria vya kutosha, ili kuhakikisha kwamba, wafugaji hawapotezi uchumi wao wakati wa kiangazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, sisi ni wafugaji naisihi Serikali, na hasa zile sekta zinazohusika, Wizara hii tunayoijadili sasa na ile mifugo ihakikishe kwamba inaweka mikakati ya kupata lishe na vyakula mbadala, kwa ajili ya mifugo, ili wasife wakati wa kiangazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwangu Wilaya ya Ngorongoro tuna wakulima karibu 13,000 wanaojishughulisha na kilimo. Naipongeza sana Serikali, imefanikiwa kusambaza mbegu za ruzuku na mbolea kwa wakati za kutosheleza, tunaishukuru sana Serikali kwa hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto yetu ni masoko. Wakulima wanapopata mazao mengi sana hupotea shambani na mengine hupotea barabarani wakiyapeleka sokoni. Ni muhimu sana Serikali iweke miundombinu ya uhifadhi wa mazao baada ya kuvuna, ili wakulima wasipoteze mazao na uchumi wao ambao wanautarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, ile wilaya yangu inatakiwa ifunguliwe. Kama Mama, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anavyofungua nchi, ile wilaya yangu inatakiwa ifunguliwe zaidi. Tunazo kilomita 49 za lami ambayo inatokea pale Wilayani Loliondo na kuishia katikati ya njia, kweli inasaidia kupunguza mwendo, lakini haisaidii kutimiza mahitaji tunayohitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muda muafaka sasa wa kutuwekea barabara ya lami kutoka Mto wa Mbu kwenda Loliondo, ili zile saa 11.00 tunazosafiri zipungue ziwe saa tatu au mbili. Tunaiomba Serikali iweke huo mkazo na msisitizo wa kutujengea hiyo barabara ya lami, ili iweze kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwa suala la mifugo. Tunayo changamoto kidogo, mara nyingi sana mifugo inapoingia maeneo yaliyohifadhiwa, kuna wakati mifugo ile inataifishwa kwa kusingizia kwamba haina wenyewe. Ninaiomba Serikali, hasa hizi sekta zinazohusika, tuache kutaifisha mifugo ya wananchi eti kwa sababu, haijatambuliwa. Mifugo mingi ina wenyewe…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umeisha. Malizia hiyo sentensi ya mwisho.

MHE. YANNICK I. NDOINYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mifugo inayotambuliwa, ina wenyewe isitaifishwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)