MHE. REGINA H. MIKENZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninapenda kuuliza swali. Ni lini Kituo cha Afya cha Kata ya Rwamgasa kitakamilishwa na kuanza kutoa huduma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifika katika Kituo cha Afya cha Rwamgasa na kiukweli kimeanza kutoa huduma za OPD na kuna majengo yanazidi kuongezwa pale kupitia mbia wetu wa Buckreef, na majengo haya yanakwenda kukamilika ndani ya mwezi wa tatu na kuanza kutoa huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshatoa maelekezo mahususi kwa Mkurugenzi kufuatilia kwa ukaribu katika ujenzi wa majengo haya ili akina mama wetu wanaojifungua zaidi ya 200 mpaka 250 kwa mwezi waweze kupata huduma hii ya afya ya msingi. (Makofi)
MHE. REGINA H. MIKENZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili nami niulize swali la nyongeza. Wilaya ya Nyang’hwale ndiyo Wilaya pekee katika Mkoa wa Geita ambayo haina barabara yoyote ya kiwango cha lami inayounganisha Wilaya hiyo na Wilaya nyingine ikiwemo Makao Makuu ya Mkoa wa Geita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni lini Serikali itatujengea barabara kwa kiwango cha lami katika Wilaya hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Mbunge na ninatambua kwamba hili swali tumelijibu mara kadhaa kuhusu barabara ya lami aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge. Barabara hii ipo kwenye utaratibu kwa sasa wa kuisanifu kuanzia Busisi – Ngoma - Nyang’hwale hadi Nyambura na pia kutoka Nyang’hwale kwenda Geita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukamilisha usanifu, gharama zitajulikana, na sasa ndiyo tutakuja na mpango wa kuijenga kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. REGINA H. MIKENZE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi, ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri, lakini bado ninapenda kuuliza maswali yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na adha kubwa wanayopitia wananchi wa Majimbo mawili ya Katoro na Busanda. Je, Serikali haioni kuna umuhimu wa kufanya haraka sana kuwapelekea halmashauri, ili kuweza kuwanusuru na adha hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili. Kwa kuwa, katika Jimbo la Katoro tunalo jengo ambalo lipo tayari, kwa ajili ya halmashauri. Je, hatuoni kama linaweza kusaidia kuharakisha harakati hizo za kulipatia Jimbo la Katoro na Busanda halmashauri?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza, ambayo yameletwa kwa niaba ya Mheshimiwa Engineer Kija Limbu Ntemi, juu ya jambo hili. Wizara iko tayari kupokea, kujadili na kupeleka kwa uharaka maombi haya kwa mamlaka, kwa ajili ya kuridhiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kwenye jibu la msingi, kutokana na mwongozo uliotolewa mwaka 2025, Halmashauri hii ilipelekewa mwongozo ule, ili waweze kuleta kwa kuzingatia vigezo vilivyotolewa. Vigezo hivi ni idadi ya watu, ili tuweze kuanzisha halmashauri mpya ni lazima tuwe na watu wasiopungua laki tano. Kwa Katoro kwa sasa ni kweli idadi ile imezidi, tuna watu zaidi ya milioni moja, kwa hiyo kigezo hiki wamekitimiza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vigezo viwili vingine ambavyo Halmashauri ya Wilaya ya Geita inatakiwa ivitimize; cha kwanza ni ukubwa wa eneo na cha pili ni kujitegemea. Kwamba, ili halmashauri iweze kupewa kuwa halmashauri ni lazima iwe na uwezo wa kifedha wa kujitegemea usiopungua asilimia 50. Kwa leo hii Halmashauri ya Wilaya ya Geita ina uwezo wa kujitegemea kwa asilimia 26 tu. Tumewapelekea mwongozo ule waweze pia kuleta, ili jambo hili tuweze kulifanyia kazi kwa uharaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la nyongeza ni kuhusu uwepo wa utayari kwa kuwa na jengo ambalo lingeweza kutumika, kwa ajili ya kuanzisha halmashauri hii. Pindi watakapotimiza vigezo hivi tuna uhakika kwamba, Wizara yetu italichukua jambo hili na kulifanyia kazi kwa haraka, ili na jengo lile baadaye liweze kutumika. Ninakushukuru sana.