Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Ester Edwin Malleko (5 total)

MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha fedha za TASAF zinawafikia walengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu. Kipekee nimshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani yake kubwa kwangu kwa kuniamini na kuniteua kuwa Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Ahadi yangu kwake ni kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa kujituma, na kwa uzalendo, ili malengo yaliyopangwa yafikiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, sasa naomba nijibu swali la Mheshimiwa Esther Malleko, Mbunge wa Viti Maalum.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia program ya TASAF, imeweka mkakati mahususi wa kuhakikisha fedha/ruzuku zinawafikia walengwa kupitia matumizi ya mfumo wa malipo ya kielektroniki (e-payments) unaolenga kuongeza uwazi, usalama na ufanisi katika utoaji wa ruzuku kwa walengwa. Mkakati huo unatekelezwa kwa kutumia watoa huduma za kifedha walioidhinishwa ambao hulipa fedha moja kwa moja kwenda kwa walengwa kupitia akaunti zao za benki na mitandao ya simu.

Mheshimiwa Spika, mfumo huu huondoa utaratibu wa kutuma fedha taslimu, na hivyo kupunguza mianya ya upotevu, ucheleweshaji au matumizi yasiyo sahihi ya fedha. Pili, malipo yote hufanyika kwa kuzingatia taarifa za walengwa zilizohakikiwa katika mfumo wa usimamizi wa walengwa, Management Information System (MIS), ambapo kila mlengwa hulipwa kulingana na utambulisho wake wa kipekee, ahsante.
MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa hoteli katika Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha uandaaji wa pembuzi yakinifu ya ujenzi wa Hoteli ya Nyota Nne katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro. Kwa sasa taratibu za kutafuta mwekezaji wa ujenzi wa hoteli zinaendelea.
MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza upatikanaji wa mbegu bora na kwa bei nafuu nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Edwin Malleko, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuongeza uzalishaji wa mbegu nchini kwa kutenga maeneo kwa ajili ya kuanzisha mashamba mapya ya kuzalisha mbegu, kuhamasisha kampuni binafsi za mbegu kuingia mikataba maalum na ASA ili kuzalisha mbegu bora kwa kutumia mashamba ya Serikali, na kuhamasisha uzalishaji wa mbegu za daraja la kuazimiwa ubora kwa maana ya Quality Declared Seeds – QDS kwa wakulima wadogo ili kuwaruhusu wakulima kuzalisha na kuuza mbegu zinazofaa kwenye maeneo husika kwa bei nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuimarika kwa uzalishaji wa mbegu nchini kutasababisha kupungua kwa ongezeko la bei linalotokana na uagizaji wa mbegu nje ya nchi. Vilevile, Wizara inaendelea kutekeleza azma ya Serikali ya kutoa ruzuku ya mbegu bora ya mazao ya kimkakati.
MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza skimu za umwagiliaji katika Mkoa wa Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Edwin Maleko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuchukua jitihada mbalimbali za kuendeleza sekta ya umwagiliaji nchini ikiwemo katika Mkoa wa Kilimanjaro. Katika kutekeleza hilo, mwaka 2025/2026, miradi 42 ya umwagiliaji inatekelezwa katika Mkoa wa Kilimanjaro ikijumuisha ujenzi na ukarabati wa skimu 15 zenye jumla ya hekta 18,154.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya skimu hizo, skimu nane ni za ujenzi zenye jumla ya hekta 9,514 ambapo utekelazaji wake umefikia wastani wa 28%. Aidha, miradi ya ukarabati ni saba ambapo utekelezaji wake umefikia wastani wa 45%. Kukamilika kwa ujenzi na ukarabati wa miradi hiyo kutawezesha kumwagilia eneo lenye ukubwa wa hekta 18,154 na kunufaisha wakulima 283,877.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa miradi ikiwemo Bonde la Mtambo lenye miradi ya Kikavu chini, Mapacha, Mtambo, Ismail na Ngosero (Mpenda Roho na Longoi) yenye jumla ya hekta 8,500. Aidha, miradi 18 ya skimu zenye zaidi ya hekta 29,000 usanifu wake unaendelea.
MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha miundombinu ya Masoko ya Mwika na Makuyuni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA
SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Edwin Malleko, Mbunge wa Viti Maalam, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa Masoko ya Mwika na Makuyuni. Kutokana na umuhimu huo Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Moshi inaendelea na mpango wa kuboresha masoko hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Soko la Makuyuni,
halmashauri imeanza kwa kutenga shilingi milioni 50 katika mwaka
2025/2026 ambapo hadi Machi, 2026 shilingi milioni 20 zimetolewa
kwa ajili ya kuzibua mifereji ya maji na kusakafia baadhi ya mifereji iliyokuwa imebomoka ili kudhibiti matope kipindi cha mvua. Aidha, halmashauri ikishirikiana na Wizara ya Kilimo itajenga soko la kisasa katika eneo la Makuyuni ambapo hadi sasa halmashauri imekamilisha kuandaa hati pacha ambayo ipo kwenye utaratibu wa kukabidhiwa Wizara ya Kilimo. Zoezi hili litafuatiwa na Wizara ya Kilimo kutangaza zabuni ili kumpata mkandarasi atakayejenga soko hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Soko la Mwika, Halmashauri ya Wilaya ya Moshi katika mwaka wa fedha 2025/2026 imetenga bajeti ya shilingi 16,000,000 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya soko hilo na hadi kufikia Machi, 2026 shilingi 15,000,000 zimetolewa na kutumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Soko la Mwika lina eneo dogo la kufanyia biashara ambapo inawalazimu wafanyabiashara kufanya shughuli zao katika eneo la barabara kuu kwa kupanga bidhaa zao barabarani. Hivyo, Serikali kupitia halmashauri katika bajeti ya mwaka 2026/2027 imetenga shilingi 70,000,000 kwa ajili ya kununua eneo la ekari moja kwa ujenzi wa miundombinu muhimu katika eneo la Mwika. Hatua hii itapunguza msongamano uliopo kwenye soko hilo na kuboresha mazingira ya kufanyia biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)