Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Yumna Mmanga Omar (1 total)

MHE. YUMNA MMANGA OMAR aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani mahsusi wa kukuza vipaji na ujuzi kwa vijana wenye ulemavu, ili kuongeza ajira na ushiriki wao katika uchumi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri Mkuu, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Yumna Mmanga Omar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ilani ya CCM ya mwaka 2025 - 2030 Kifungu cha 95, imelenga kuwashirikisha na kuwawezesha watu wenye ulemavu kupata ajira zenye staha na kuwajengea uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali imeweka mkakati wa Kitaifa wa kukuza na kuendeleza vipaji na ujuzi kwa vijana unaoongozwa na Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007, Toleo la mwaka 2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, katika Dira ya Taifa ya mwaka 2050, Serikali imeweka mkakati wa kukuza Elimu Jumuishi na ujumuishwaji wa vijana wenye ulemavu katika elimu, mafunzo ya ufundi, ajira na shughuli za kiuchumi kwa kutambua kuwa, ulemavu haupaswi kuwa kikwazo cha mtu kutumia kipaji chake na uwezo wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza mikakati hiyo, jumla ya vijana wenye ulemavu 643 walijiunga na kuhitimu mafunzo ya ufundi stadi kwenye vyuo vitano vya ufundi, ikiwemo VETA, kwenye maeneo mbalimbali nchini kuanzia mwaka 2023 hadi 2025. Vijana hao, waliwezeshwa kupata ujuzi katika fani mbalimbali za umeme wa majumbani, useremala, uungaji vyuma, ushonaji wa nguo na viatu, kilimo na ufugaji na ujenzi na uashi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, Serikali imeendelea kuwawezesha vijana wenye ulemavu kwa kutenga 30% ya zabuni za umma, ambapo kufikia mwaka 2024/2025 jumla ya vikundi 703 vimesajiliwa kwenye mfumo wa NEST, ili kuhakikisha ujuzi wanaopata uweze kutumika kuwapatia ajira na kujikwamua kiuchumi kupitia shughuli za ujasiriamali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali imeendelea kutenga 10% ya makusanyo ya halmashauri, kwa ajili ya kutoa mikopo kwa makundi maalum, ambapo asilimia mbili hutengwa, kwa ajili ya watu wenye ulemavu. Katika kipindi cha mwaka 2021 hadi kufikia mwaka 2026 jumla ya kiasi cha fedha shilingi bilioni 26.87 kimetolewa, kwa ajili ya kuwawezesha watu wenye ulemavu. Ninaomba kuwasilisha.