Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Yumna Mmanga Omar (2 total)

MHE. YUMNA MMANGA OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na majibu mazuri ya Serikali, ningependa kujua. Je, Serikali ina mfumo gani madhubuti wa kutambua vijana hawa ambao wamepata mafunzo haya, ni wangapi ambao wamepata ajira, wamejiajiri na kuanzisha biashara endelevu? Iwapo mfumo huo upo, Serikali inaweza kutueleza matokeo halisi yaliyopatikana hadi sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza naanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Yumna kwa kuwasemea watu wenye ulemavu. Amefanya hivyo hata katika Bunge la Bajeti lililopita, ameendelea kuwasemea walemavu, ili waweze kunufaika na fursa katika nchi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanzisha mfumo rasmi wa kupata taarifa kutoka katika halmashauri zetu kote nchini, lakini pia, tunaendelea kutumia wakurugenzi wetu na maafisa maendeleo ya jamii katika halmashauri zote nchini kuwafikia vijana wenye ulemavu, kutoa elimu na kuhakikisha na wao wananufaika na ile mikopo ya 10%, zile asilimia mbili na pia, katika yale manunuzi ya umma (PPRA) nao wanaingia katika mifumo hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tumepata takwimu hii ya zaidi ya vikundi 703 na mwanzoni vilikuwa vikundi 45 tu, lakini mpaka sasa kuna vikundi 703 na tunaona matokeo. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Yumna, pamoja na walemavu wengine nchi hii ni yao na wao lazima tuwajumuishe katika kukuza uchumi wao binafsi. Ninaomba kuwasilisha.
MHE. YUMNA MMANGA OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Sambamba na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujua, miradi hii ya kimkakati inazalisha sana fursa mpya za ajira na ujuzi. Je, Serikali inahakikisha vipi wanafunzi wahitimu wenye ulemavu wanafaidika na fursa hizi za ajira mpya na ujuzi? Ni kwa namna gani inawafuatilia wao kuweza kunufaika na ajira hizo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA MAHUSIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Kwanza nachukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge, amekuwa mahiri sana katika kupigania suala la watu wenye ulemavu katika sekta hii ya ajira na muda si mrefu ametoka kuuliza swali la aina hiyohiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua kwamba, miradi ya kimkakati katika dhana ya local contexts inasisitiza ajira kwa wazawa na pia, inahusisha ajira kwa watu wenye ulemavu. Kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, katika Kitengo cha Kamishna wa Kazi, tunafanya kaguzi mbalimbali kuhakikisha uzingatiaji wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu, Sura 183, ambayo inasisitiza kwamba, kila mwajiri katika mradi huu anatakiwa kutenga nafasi, kwa ajili ya watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge, tunaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kuhakikisha watu wenye ulemavu, wakiwa ni wadau muhimu kabisa katika kutekeleza miradi hii ya kimkakati, wanapata fursa ya ajira.