MHE. ISAYA M. MOSES aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza uchimbaji wa Bwawa la Chilanilizi, Kata ya Ngomai – Kongwa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI K.n.y. WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Isaya Mngurumi Moses, Mbunge wa Kongwa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ilitenga fedha katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la Maji Chilanjilizi, Kata ya Ngomai ambapo upembuzi yakinifu wa mradi huu umekamilika kwa 100%. Kwa sasa Tume imeingia mkataba wenye thamani ya shilingi bilioni 106 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi wa uchimbaji na ujenzi wa bwawa hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kukamilika kwa Mradi wa Bwawa la Chilanjilizi unatarajiwa kunufaisha vijiji vinavyozunguka eneo la mradi ikiwemo Chilanjilizi, Manyaya, Sigoni na Ngomai na maeneo mengine yanayozunguka mradi huo na hivyo kutoa fursa kwa wananchi kupata fursa ya uhakika wa maji kwa ajili ya kilimo na shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii.