MHE. ISAYA M. MOSES: Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa huu mradi utawainua sana wananchi wa Kongwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabla ya kusema hivyo nishukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali yanatupa matumaini makubwa, kwa utekelezaji wa huu mradi, maana yake ni kwamba wananchi wangu wa Vijiji vya Kata za Ngomai, Kata ya Ngomai, Mtanana, Songambele, Mkoka pamoja na Matongolo, Makawa pamoja na Njoge watanufaika zaidi katika huu mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, ni lini sasa utekelezaji wake utaanza kwa sababu tayari sasa watu walishapisha huu mradi, lakini umechukua muda mrefu, sasa familia zimeanza kurudi katika haya maeneo. Wanasema kwamba mradi hautakuwepo, tusipoangalia itatuingiza tatizo la kulipa fidia sasa tuone tutajipangaje katika eneo hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Kongwa sio mbali, nimuombe Mheshimiwa Waziri akipata nafasi twende tukatembelee pale, tukaone hali halisi na tukatembelee watu wana shida ya maji kule, twende tukakutane nao. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI K.n.y. WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Isaya Mngurumi Moses nikiwa najibu kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwanza tunampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi ambavyo ameanza kazi vizuri, anafuatilia maslahi ya wananchi wa Kongwa na kwa kweli kwa kutambua umuhimu wa mradi huu ndiyo maana Serikali kwanza ilitambua, pili ikafanya usanifu na tatu, baada ya kutazama na kutambua gharama zote, ikaamua kusaini mkataba wa zaidi ya shilingi bilioni 106 ili kazi ianze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba hii ni moja ya miradi ambayo inatarajiwa kuanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha ujao. Kwa hiyo, nimwombe awe na subira ili Serikali ikaweze kufanya mradi huu muhimu kwa wananchi wa jimbo zima la Kongwa na hili la pili, naamini Waziri wa Kilimo amesikia au Naibu Waziri, wakati ukifika watakwenda naye kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanatazama kulingana na maombi ya Mheshimiwa Mbunge.