Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Hasnain Gulamabbas Dewji (1 total)

MHE. HASNAIN G. DEWJI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kulipa fidia kwa Wananchi wa Kilwa Masoko waliopisha upanuzi wa eneo la Uwanja wa Ndege?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Hasnain Gulamabbas Dewji, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha zoezi la uthamini wa mali za wananchi wanaopaswa kupisha utekelezaji wa mradi wa ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kilwa Masoko. Hatua hii ni muhimu katika kuhakikisha kuwa haki na stahiki za wananchi husika zinatambuliwa ipasavyo kabla ya utekelezaji wa mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali inaendelea na taratibu za upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi hao, kwa kuzingatia taratibu na miongozo ya kisheria inayosimamia ulipaji wa fidia nchini. Serikali ina dhamira ya kuhakikisha kuwa fidia stahiki inalipwa kwa wakati kadri rasilimali zitakavyopatikana, ili kuwezesha utekelezaji wa mradi huo muhimu kwa maendeleo ya sekta ya usafiri wa anga na uchumi wa eneo husika.