MHE. HASNAIN G. DEWJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa ahadi hii ya fidia ilitamkwa na Mheshimiwa Rais Mkoani Lindi wakati amekuja kuomba kura, na ahadi ya Rais ni kama maelekezo, na kwa kuwa Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo wananchi wangu walipwe fidia, ninamwomba Mheshimiwa Waziri aharakishe hilo jambo kwa kuwa wananchi wangu wanateseka sana, hawana mpango wowote, huku fidia hawajapata na huku mvua zinanyesha. Kwa hiyo, ninaomba sana fidia ipatikane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, ninamwomba Naibu Waziri aje Kilwa kuona, tukae nao wanateseka sana, mvua hizi ni kubwa, hawana pa kwenda huku fidia hawajapata, huku hawajijui wanakwenda wapi? Kwa hiyo, ninamwomba sasa Naibu Waziri aje aongozane na mimi, tufuatane, aone kabla...
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Dewji kwa namna ambavyo ana-sympathize na wananchi wa Kilwa Kusini kutokana na jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa Serikali inatambua umuhimu wa kuendeleza kiwanja hiki, na lazima nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba yako mambo makuu matatu ambayo tunayazingatia sana katika upangaji wa bajeti. La kwanza, tunatazama Ilani ya CCM; la pili, tunatazama dira ya 2050; na la tatu, maelekezo ya viongozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yeye mwenyewe ameshasema na amekumbushia kwa niaba ya wananchi kwamba Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameonyesha dhamira ya dhati kwa kuhakikisha kwamba uwanja huu unajengwa. Pale Kilwa siyo tu uwanja, pia alionyesha dhamira ya dhati kuhakikisha kwamba bandari ya uvuvi inajengwa na ninyi mnashuhudia bandari ya uvuvi sasa inakwenda kuzinduliwa. Nimhakikishie hata hili anakwenda kulifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge awe na subira, Serikali kupitia Wizara yetu ya Uchukuzi pamoja na Wizara ya Fedha tumeshamaliza uthamini, hatua iliyobaki ni kulipa. Tutakwenda kuharakisha kama alivyoomba ili wananchi hao wanaoteseka waweze kupata fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ameuliza kuhusiana na kuwa tayari kwenda, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi Mheshimiwa Prof. Makame Mbarawa Mnyaa, nitakuwa tayari kuambatana na Mheshimiwa Mbunge kwenda kwenye eneo kuzungumza na kuwaeleza nia dhahiri ya Serikali ili watuvumilie tunapoendelea kujipanga kwa ajili ya kulipa fidia hiyo.