Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Josephine Joseph Kapoma (1 total)

MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kufikisha elimu kwa wananchi kuhusu Biashara ya Hewa ya Ukaa kwa kuwa ni miongoni mwa biashara kubwa duniani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba uridhie kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama mahali hapa tangu Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliponiteua kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee sana, ninapenda kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuniamini kwa nafasi hii katika Wizara hii ya Makamu wa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, ninamshukuru Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Prof. Shemdoe pamoja na familia ya TAMISEMI chini ya Waziri Mkuu kwa ushirikiano mkubwa walionipa kwa nafasi ile ya Naibu Waziri wa TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo, nitumie nafasi hii nimshukuru sana Mheshimiwa Eng. Hamad Masauni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, pamoja na watumishi wote chini ya Ofisi hii ya Makamu wa Rais kwa kunipokea vyema na kunipa ushirikiano kwa majukumu haya ninayoendelea nayo kwenye Ofisi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Joseph Kapoma, Mbunge wa Mkoa wa Morogoro, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais na Kituo chetu cha Kusimamia masuala ya Kaboni, zimeweka mikakati mbalimbali ya kufikisha elimu kwa wananchi kuhusu biashara ya kaboni, ambayo ni miongoni mwa biashara kubwa duniani, kwa kupitia njia zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ni kutekeleza programu za uhamasishaji na elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari kama redio, televisheni na mitandao ya kijamii ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu dhana, faida na fursa zilizopo katika biashara ya kaboni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, njia ya pili ni kutoa mafunzo kwa viongozi wa ngazi za mikoa, halmashauri na vijiji ili waweze kuwa mabalozi wa elimu kwa jamii zao kuhusu utekelezaji wa miradi ya kaboni na manufaa yake. Hili tumelitekeleza kwa kutoa elimu kwa viongozi mbalimbali tangu kupitishwa kwa kanuni na mwongozo wa biashara ya Kaboni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, njia ya tatu na ya mwisho ni kushirikiana na wadau wa maendeleo, asasi za kiraia na sekta binafsi katika kutoa elimu na kujenga uwezo wa jamii kuhusu namna ya kuanzisha na kunufaika na miradi ya Kaboni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuimarisha juhudi hizi ili kuhakikisha wanapata uelewa wa kutosha na kushiriki kikamilifu katika biashara ya kaboni, hivyo kunufaika kiuchumi huku wakichangia katika juhudi za kuhifadhi Mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.