Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Josephine Joseph Kapoma (12 total)

MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Je, Wizara ina mkakati gani wa kuja na solution ya kudumu, na hata kama siyo ya kudumu japokuwa ya muda mrefu kwa zile barabara zinazozibwa viraka? Kwa mfano, kuna baadhi ya barabara unakuta zina mashimo, lakini zinazibwa mara kwa mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa ninataka kujua kama tunaweza tukapata solution ya kuziba viraka ambavyo vitakaa kwa muda mrefu kwa ajili ya ku-save pesa ambazo zinatumika. (Makofi)



NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mbunge wa Mkoa mzima wa Morogoro aliyetoka kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametupa maelekezo sisi TARURA ndani ya Serikali kwa ajili ya kuanza mkakati wa kutumia teknolojia mpya ambayo itajenga barabara zetu kwa gharama nafuu na hivyo tutaweza kuyafikia maeneo mengi na kujenga barabara zinazodumu kwa muda mrefu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa huu Mkoa wa Morogoro ambao Wabunge wake wameuliza maswali mengi hapa, Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana, tumejenga mtandao wa barabara kwa kiwango cha lami na sasa tumefikisha karibia kilometa 125. Mradi wa TACTIC ambao tulitekeleza kwa awamu ya kwanza tulipeleka zaidi ya shilingi bilioni 19. Mheshimiwa Rais lengo lake ni kutaka kuona anaufungua Mkoa huu mkubwa ambao ni muhimu kwa uchumi ndani ya nchi yetu. (Makofi)
MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nina swali dogo la nyongeza. Kama ikimpendeza Mheshimiwa Naibu Waziri atalijibu au atalichukuwa. Wilaya yetu ya Malinyi tumekuwa tuna shida ya gereza la mahabusu kwa muda mrefu sana. Eneo limepatikana lakini kumekuwa kuna ucheleweshwaji wa kukamilisha ambayo inawafanya wahusika kusafiri umbali mrefu sana kwenda Wilaya ya Ulanga. Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha suala hili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimfahamu ili niweze kujibu vizuri; amekusudia mahabusu ya polisi au ya gereza?NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge.

MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, mahabusu ya gereza.

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tunaongelea kuhusu suala la Jeshi la Polisi lakini kwa sababu Magereza na yenyewe ni sehemu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, lakini ninaomba tu nimjibu Mheshimiwa Kapoma kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli yapo baadhi ya magereza yamekuwa na changamoto ya uchakavu wa majengo. Hata hivyo, moja ya eneo ambalo amelitaja la jimbo lake kwamba wilaya nzima ya Malinyi hakuna gereza na kupeleka eneo la pili; tunakuja na mpango na tutaueleza kwenye bajeti ya mwaka huu kwamba ni mpango gani kwa upande wa Jeshi la Magereza, tutaenda kuboresha magereza katika maeneo ambayo yana uhaba likiwepo eneo lake la Malinyi.
MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakazi wa Kata ya Boma Mlimani Luhungo wa Wilaya ya Morogoro Mjini wamekuwa na mgogoro wa muda mrefu na Serikali kwa ajili ya uharibifu wa mazingira. Je, Serikali ina mpango gani wa kuja na mkakati wa kutoa elimu ya mbinu bora za kilimo zitakazozingatia uhifadhi wa mazingira?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nimthibitishie tu Mheshimiwa Josephine kwamba, moja ya mkakati wa Serikali ili kuhakikisha kwamba wananchi hawaendelei kuharibu mazingira, ni pamoja na kuhakikisha tunajenga miundombinu bora na ya kisasa, kwa maana ya mabwawa na schemes ili wananchi wale tukishawapanga na kuonesha maeneo ambayo wanafaa kufanya kilimo chao, maana yake hawatakuwa na nafasi ya kwenda kuharibu mazingira katika maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tutaendelea kupeleka timu kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kutunza mazingira, kwa sababu sisi mazingira ndiyo ambayo yanatusaidia kupata vyanzo bora vya maji ambavyo sasa miradi yetu ndiyo maeneo ambayo tumekuwa tukitekeleza.
MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, vijana wengi wamekuwa wanapata hizi fursa za mikopo na Serikali imejitahidi sana kufungua hizi fursa, lakini tumekuwa na shida kubwa sana kwa vijana kwa sababu wengi hawana nidhamu ya fedha (finance mistress), lakini sasa Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha Vyama vya Ushirika vya Kuweka na Kukopa (SACCOS) ili waweze kujengewa uwezo wa kuwa na nidhamu ya fedha? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAENDELEO YA VIJANA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, Serikali imeendelea kujitathmini kila wakati kuona namna ambavyo mikopo inayotolewa hasa kwenye kundi la vijana inakuwa na ufanisi. Kama alivyoeleza Mheshimiwa Kapoma, ni kwamba kumekuwa na changamoto kubwa sana hasa katika urejeshaji, kwa mfano tukiangalia Mfuko wa Maendeleo wa Vijana, zaidi ya shilingi bilioni 3.9 zimeshindwa kurejeshwa. Tumefanya tathmini kuangalia changamoto ni nini, ikiwepo pia na asilimia nne zinazotolewa kupitia halmashauri zetu. Moja ya changamoto tuliyoiona, ni elimu ya kifedha na ndiyo maana kupitia awamu hii ya mikopo tuliyoitoa, tumeingia utaratibu wa makubaliano rasmi na taasisi ya kifedha hasa CRDB, ambayo kabla kijana hajapata mkopo, huwa anapata fursa ya kupewa mafunzo maalum yanayohusiana na usimamizi wa kifedha, nidhamu pamoja na biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafunzo haya yanakuwa endelevu pia, ili kuhakikisha kwamba wanaendelea kupata elimu hiyo kwa namna endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea wazo lako na ushauri wako juu ya kuwa na SACCOS za vijana, na kama ambavyo Serikali imeendelea kuwezesha kwenye vikundi, tutaendelea kuifanyia kazi ili kuhakikisha kwamba vijana wanafikiwa kwa wingi. Ahsante sana.
MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali. Nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, wafanyabiashara hawa waliahidiwa soko hili kuanza tangu Julai, 2025 na mpaka sasa wanashindwa kufanya biashara zao kwa sababu hawajui hatima yao. Je, ni lini sasa Serikali inategemea kuanza mradi huu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tuna miradi kadhaa Mkoa wa Morogoro ambayo inatakiwa, iko chini ya TACTIC. Je, ni lini Serikali inajipanga kuanza kukamilisha kwa sababu mingi iliahidiwa tangu mwaka 2025?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali inatekeleza miradi hii ya TACTIC; tunayo makundi matatu. Kuna kundi la kwanza la miji 12, kundi la pili la miji 15 na kundi la tatu ambalo Ifakara imo ni miji 18.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari imeshaanza utekelezaji wa miradi hii katika makundi ya kwanza na ya pili na utekelezaji unaendelea. Ipo miradi iliyokamilika, ipo ambayo inaendelea na hatua mbalimbali. Baada ya kukamilisha usanifu wa miradi hii ya kundi la tatu, tutaanza utekelezaji wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Jimbo la Kilombero na Ifakara kwamba Serikali baada ya kukamilisha usanifu wake tutaanza mara moja utekelezaji wa mradi katika eneo la Ifakara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tunafahamu kuwa iko miji kadhaa ambayo iko kundi la tatu, la kwanza na la pili ambayo inaendelea na utekelezaji wa miradi ya TACTIC. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kama ambavyo utekelezaji unaendelea, tutahakikisha inakamilika kwa wakati. Ile ambayo haijaanza, na ambayo iko tier three tutahakikisha nayo inaanza kwa ajili ya kuhakikisha kwamba inatekelezwa kwa wakati.
MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa ninataka niulize swali dogo la nyongeza. Nchi nyingi kwa sasa zimeshapiga hatua kubwa sana katika kubadilisha taka kuwa fursa za kibiashara. Je, Serikali ina mkakati gani wa kujielekeza katika mlengo huu ili kutokomeza hili suala la uchafuzi wa mazingira? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza sana Mbunge wa Mkoa wa Morogoro kwa swali lake zuri, na amekuwa msemaji mzuri sana kuutetea Mkoa wa Morogoro pamoja na Tanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuweka jitihada kubwa katika kuhakikisha kwamba taka zinazozalishwa kwenye mazingira ya shughuli zetu za kiuchumi kwenye miji yetu, kwenye majiji na maeneo mbalimbali zinakuwa recycled, yaani zinarudishwa kutumika kwa ajili ya kuzalisha bidhaa ambazo zitatumika tena kwenye mzunguko wa uzalishaji kwenye maeneo mbalimbali ya kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, Serikali inahakikisha kwenye majiji makubwa, mathalan kama ilivyo Dar es Salaam inajenga madampo makubwa na ambayo yataambatana na miundombinu ya viwanda vitakavyoendelea kufanya recycling, yaani marejeo na marejesho ya hizo taka ili ziweze kutumika tena kwa ajili ya kuzalisha bidhaa zitakazotumika kwenye maeneo yetu.
MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Morogoro Mjini tuna Barabara ya Tungi ambayo imebakiza kipande kidogo sana, na hii barabara ni kati ya barabara za suluhisho za diversion endapo barabara kubwa ya Msamvu kuelekea Dar es Salaam ina shida. Sasa nilikuwa ninataka kujua mpango wa Serikali wa kumalizia hiki kipande kidogo cha kuunganisha Kihonda – Tungi kuelekea Dar es Salaam.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ninampongeza Mheshimiwa Josephine, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Morogoro, lakini nimhakikishie kwamba Serikali inatambua kwamba ziko barabara katika Manispaa ya Morogoro ambazo kwanza zimeharibiwa na mvua nyingi, lakini barabara nyingine ni chakavu ikiwemo barabara ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja. Lengo na dhamira ya Serikali ni kuendelea kujenga na kuboresha barabara hizo kwa awamu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Manispaa ya Morogoro kwamba tutaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizo. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI nitumie fursa hii kuwasisitiza Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuweka kipaumbele kwenye fedha za mapato ya ndani kwa mujibu wa maelekezo ya halmashauri ambazo zinakusanya zaidi ya shilingi bilioni 10, ni lazima watenge fedha kwa ajili ya matengenezo na ukarabati wa barabara.

Mheshimiwa Spika, hata halmashauri ambazo zinakusanya chini ya shilingi bilioni 10 kama barabara ni kipaumbele kikubwa katika eneo hilo, ni muhimu watenge fedha kwa ajili ya ukarabati wakati tunasubiri fedha za Serikali Kuu.
MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Sasa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Je, Serikali inasimamia vipi kuhakikisha vijiji husika vinapata magawio yao kwa usawa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Takwimu inaonesha kampuni nyingi za wanunuzi wa hewa ya ukaa ni kampuni za kigeni. Je, Serikali imeweka vigezo rafiki kuvutia kampuni za wawekezaji wazawa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge Josephine, amekuwa ni msemaji mzuri wa kuutetea mkoa mzima wa Morogoro na Watanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameuliza maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, ni kwa namna gani Serikali inahakikisha vijiji vinapata magawio sawia kwenye biashara hii ya hewa ya ukaa? Serikali imeweka utaratibu wa kikanuni na wa kimiongozo kupitia Kituo chetu cha Uratibu wa Biashara hii ya Kaboni (NCMC) kwamba, biashara inapokuwa imefanyika, kijiji hupata 50% kama biashara hii imefanyika kwa kupitia uvunaji wa hewa ya ukaa kwa kupitia misitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo, halmashauri husika, kama kampuni iliyofanya biashara ni kampuni ya kigeni, italazimika kulipa 10% kwenye halmashauri hiyo, na vilevile kampuni hiyo italazimika kulipa asilimia moja kwenye mkoa husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ni lilikuwa kwamba kampuni nyingi zinazofanya shughuli ya ununuzi wa credit zinazotokana na biashara hii ya hewa ya ukaa ni za kigeni. Ametaka kujua ni mkakati gani uliopo wa kuwafanya wazawa waweze kuwa wanunuzi kama ambavyo kampuni za kigeni zinanunua?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni biashara ambayo kwa ngazi ya ununuzi inahitaji mtaji mkubwa. Sisi kama Serikali tunaandaa mwongozo na mkakati maalumu wa namna ya kuwawezesha Watanzania wazawa ili waweze kuwa na mitaji ya kuweza kununua credits hizi za kaboni, waweze kushiriki kwenye biashara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo, kwenye miongozo hii na mikakati tunayoiandaa kupitia Kituo chetu cha NCMC tunaweka utaratibu wa kushirikisha sekta binafsi na hususan benki, ili ziweze kushiriki kuwawezesha Watanzania wazawa kimitaji. Kama ambavyo tumeona benki zikifanya kwenye maeneo mengine kama ilivyokuwa kwenye barabara, benki zimefanya kwenye infrastructure bond. Kwa hiyo, vivyo hivyo, hata kwenye eneo hilo la hewa ya ukaa Serikali itakwenda na uelekeo huo.
MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Spika, Wananchi wa Wilaya ya Gairo, Mkoani Morogoro, wanashukuru sana kwa kupatiwa Madaraja ya Chakwale na Nguyami yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 24, lakini sasa tuna Daraja dogo sana la Matare ambalo linaunganisha Idibo na kuelekea Kilindi, Tanga na kata nyingi za Gairo, ambalo tumeliomba kwa muda mrefu sana. Ni lini Serikali itatukumbuka kukamilisha ujenzi wa daraja hili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mpango wa kutengeneza yale madaraja ambayo yalikuwa changamoto miaka yote, na yale aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge, ya Chakwale na Nguyami, yamekamilika na sasa wananchi hao wanapita.

Mheshimiwa Spika, hiyo barabara tunavyoongea sasa hivi ipo kwenye mpango wa kusanifiwa, ikiwa ni pamoja na hilo daraja. Ninamwelekeza tu Meneja wa Mkoa wa Morogoro aweze kwenda kwenye hilo eneo, ili wakati tunakamilisha usanifu, basi tuweze kupata mahitaji na kuona uwezekano wa kulitengeneza hilo daraja kwa muda; kwa sababu, madaraja yale makubwa yametengenezwa, basi na hilo tuweze kuliangalia kama linaweza likatengenezwa kwa udharura, kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, ahsante.
MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, wakazi wa Morogoro Vijijini wanaendelea kuishukuru Serikali kwa kuendelea kuliongezea thamani zao la karafuu. Hivi karibuni tumefanikiwa kufungua maghala matatu; Kinole, Tawa na Kisemu. Kwa msimu wa mwaka jana tu, tumepata zaidi ya shilingi bilioni ya 41.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni upi mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba tunakuwa na Stakabadhi Ghalani ili tupate kuongeza thamani ya hili zao la karafuu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nimpongeze dada yangu Mheshimiwa Josephine Kapoma, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Morogoro kwa swali lake la msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri nipongeze Mkoa wa Morogoro kwa jitihada kubwa wanayoifanya sasa hivi ya kuzalisha karafuu kwa wingi na kutaka kuwa miongoni mwa maeneo ama mikoa itakayoongoza kwa uzalishaji hapa nchini. Ninafahamu na kwenye huo mkakati mimi mwenyewe nilikuwepo. Mkakati wa Serikali ni kwamba; cha kwanza tuongeze uzalishaji na baada ya hapo sasa tutafute masoko ya uhakika ikiwemo kuingiza hili zao katika Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, lakini baada ya kuongeza uzalishaji kwa wingi.
MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kati ya vipaumbele vikubwa vya kuongeza uchumi Mkoa wa Morogoro ikiwa kimoja wapo ni kuongeza idadi ya watalii wa ndani kutoka watalii 60,000 mpaka 300,000 na wa nje kutoka 400,000 mpaka 750,000 na Serikali ilishatuahidi kutujengea kiwanja cha ndege kwenye Hifadhi ya Mbuga ya Mikumi; je, ni lini Serikali itaanza kutekeleza suala hili? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Josephine kwa swali lake ambalo kimsingi ameliuliza. Ni kweli Serikali inayo dhamira ya dhati ya kuendeleza sekta ya utalii na uwanja wa ndege pale Mikumi ni moja ya vipaumbele vyetu kwenye ilani yetu. Nimhakikishie kwa kuwa ndiyo tunaanza utekelezaji wa ilani hiyo, aipe muda Serikali iendelee na mchakato wa ndani, tutakapokuwa tayari basi tutakwenda kuanza taratibu za kuujenga uwanja huo.
MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; ni lini Serikali itajikita katika utafiti wa kina wa maeneo ya uchimbaji wa madini hususan katika Mkoa wa Morogoro ili tuweze kuchimba kwa utaratibu na kuacha kuchimba kiholela?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Serikali ina mkakati gani wa kuzishughulikia zile leseni ambazo zimetolewa, lakini haziendelezwi kwa wakati ambazo zinachochea uchimbaji haramu na uvamizi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Josephine kwa jinsi ambavyo amekuwa mtetezi wa kweli wa wachimbaji wadogo wa madini nchini. Nitumie fursa hii kumjibu kwa swali lake la kwanza kuhusu mpango wa Serikali wa kuongeza wigo wa utafiti ili kubaini maeneo yenye madini ya aina mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba zoezi hili linaendelea na hivi sasa Serikali iko katika hatua za mwisho za kupata kampuni kubwa ya utafiti wa madini kwa kutumia ndege ya nyuki na ndege nyingine kubaini maeneo yote yenye madini kwa kumulika kutoka juu ile tunayoita high resolution aerial surveying ili kujua maeneo sahihi ya kuwapa wachimbaji wetu wadogo, wakubwa na wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, niendelee tu kusisitiza kwamba Watanzania wachangamkie fursa za kutafuta maeneo ya uchimbaji wa madini kwa sababu Serikali inaenda kuwafanyia utafiti na muda siyo mrefu tutakuwa na maeneo sahihi yenye taarifa sahihi za kuwapa wachimbaji wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la pili kuhusu leseni ambazo hazijaendelezwa, ninapenda tu kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna kaguzi zinazoendelea. Kuna zoezi linaendelea la kukagua leseni zote nchini ili kubaini maeneo ambayo hayaendelezwi na hati za makosa kutolewa na kufutwa kwa leseni hizo. Hivi sasa tupo katika hatua ya kufuta leseni 87 ambazo zikishafutwa kwa mujibu wa sheria kuna maeneo matano ambayo yatatengwa mahsusi kwa ajili ya wachimbaji wadogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nitoe rai kwa wamiliki wa leseni nchini waendeleze leseni zao kwa sababu wasipoendeleza, tutazifuta na wale ambao wako tayari kuwekeza waje wayaombe hayo maeneo baada ya kuwa yamefutwa na kutangazwa na Serikali. Ahsante sana.