Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Questions to the Prime Minister from Hon. Khalid Mussa Nsekela (1 total)

MHE. KHALID M. NSEKELA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwanza ninaipongeza Serikali kwa jitihada za makusudi za kuendeleza sekta ya elimu na kuwawezesha vijana kiuchumi na jamii kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni vijana wengi ambao wako Vyuo Vikuu wamekuwa wakipata changamoto sana wanapokuwa wamemaliza, wanakuja kutafuta ajira, wamejikuta hawana ujuzi ambao unaendana na ajira inayotakiwa.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, swali langu ni je, Serikali ina mpango gani na mkakati wa kuwezesha taasisi za elimu ya juu, kushirikiana na sekta binafsi ili kuwajengea uwezo vijana ambao wako vyuo vikuu na kuwaandalia mazingira ya kuwapa ujuzi na uzoefu ili wawe tayari kwa soko la ajira?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, ninamshukuru Mheshimiwa Khalid Nsekela kwa swali zuri ambalo ameliuliza.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwepo na hiyo changamoto ya vijana kupata shida ya masuala yanayohusiana na ajira baada ya kuwa wamehitimu. Serikali tayari imeshasaini makubaliano ya ushirikiano kati ya Serikali, vyuo vikuu, pamoja na waajiri wakiwemo waajiri wa sekta binafsi, kuweza kuangalia namna nzuri ya kuwaandaa vijana wetu kuingia katika soko la ajira, na kuwa washindani katika masuala haya yanayohusu upatikanaji wa ajira.

Mheshimiwa Spika, baadhi ya masuala ambayo yapo katika yale makubaliano, na utakumbuka pia hivi majuzi tulipokea andiko moja zuri kutoka kwa Mheshimiwa Selemani Jafo, Mbunge wa Kisarawe ambalo na lenyewe lilikuwa linatoa mawazo na maoni kuhusu ni namna gani vijana wanaweza kupata ajira ndani ya Serikali, na sekta binafsi hasa wanapohitimu vyuo vikuu.

Mheshimiwa Spika, kupitia hilo ambalo nimesema Serikali imeshasaini makubaliano hayo na mawazo haya ambayo Waheshimiwa Wabunge wametoa, likiwemo hili ambalo Mheshimiwa Khalid Nsekela amelitoa kupitia swali lake zuri na mawazo mengine ambayo Waheshimiwa Wabunge wametoa ikiwemo lile alilotoa Mheshimiwa Jafo, Serikali kupitia wataalam wake wanaendelea kuangalia madirisha yote haya ambayo yatawafanya vijana waweze kupata mafunzo, waweze kutumia vizuri fursa zinazopatikana ndani ya Serikali na ndani ya sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, baadhi ya maeneo ambayo Serikali inayaangalia, mojawapo ni hilo la kupata mafunzo angali wanasoma, waendelee kupata attachment za kuweza kujifunza kinachofanyika katika ofisi mbalimbali, zikiwemo za umma na zile za sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, lingine, kama nilivyosema, Serikali inaendelea kufanyia kazi maelekezo ambayo Mheshimiwa Rais aliyatoa ya kuangalia kuwa na dirisha la wahitimu. Dirisha la wahitimu, tunaangalia kupitia hii kampuni ambayo itaanzishwa ambayo ni Export Credit Guarantee Scheme, iweze ku-guarantee vijana wetu wanaotoka vyuo vikuu ambao wako na mawazo ya kufanya uzalishaji, lakini wanakosa mitaji, ili waweze kupata mitaji, na wakipata mitaji, tuna uhakika kwamba wataweza kujiajiri na pia kuajiri na wengine.

Mheshimiwa Spika, tunawaza hatua kubwa zaidi ya kubadilisha sheria kutoka kwenye dhamana ambazo zilikuwa zinatambulika zamani, zile ambazo hazihamishiki, kwenda kwenye dhamana zinazohamishika.

Mheshimiwa Spika, chukua mfano mmoja mdogo wa mtu ambaye amepeleka kumsomesha mtoto wake kuanzia kindergarten, akaenda primary, akaenda sekondari, akaenda mpaka chuo na pengine mpaka vyuo vya nje, amemsomesha shule binafsi, gharama kubwa, mwisho anapomaliza anakuwa na cheti chake na hakitambuliki, lakini kipande cha eneo cha hati ya milioni 15 kinaweza kikadhamini mkopo.

Mheshimiwa Spika, cheti cha chuo kilichogharimu takribani milioni 200 hakiwezi kutambulika na kikatumika kama dhamana. Kwenye sheria tunayopendekeza, tunataka vyeti vya shule vikishathibitishwa na TCU viweze kutumika kama dhamana ya kukopa na mhitimu yule aweze kutumia cheti chake kuweza kupata mkopo.

Mheshimiwa Spika, msomi wetu aliyemaliza Famasia, na akapata cheti chake, msomi wetu aliyemaliza Electrical Engineering na akapata cheti chake, kukosa vitendea kazi vile vya kuweza ku-practice taaluma yake, na cheti anacho kwamba tumlazimishe naye awe na kipande cha ardhi tu ndiyo aweze kukitumia kama dhamana, hili tunaona tunabana wigo wa fursa ambazo vijana wetu wanakuwa wameshapata.

Mheshimiwa Spika, hivyo, haya ni baadhi ya maeneo ambayo wataalamu wetu wanaendelea kuyachambua na Muswada upo, unafanyiwa kazi. Tunaamini utakapokuwa umeiva tutaleta ndani ya Bunge lako Tukufu ili kuweza kuwapa fursa hiyo kubwa vijana wetu waweze kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika masuala ya ajira.