Supplementary Questions from Hon. Khalid Mussa Nsekela (5 total)
MHE. KHALID M. NSEKELA: Mheshimiwa Spika, kwanza ninaungana na wenzangu kumtakia heri ya kuzaliwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ninaishukuru Serikali kwa kutuletea mkandarasi wa kujenga Barabara ya lami kutoka Kyerwa kwenda Omurushaka, kilometa 50. Hata hivyo, speed yake ni ndogo sana. Je, Serikali ina mkakati na maelekezo gani ya kumsimamia mkandarasi huyu ili amalize barabara hii ili kukidhi kilio cha wananchi wa Kyerwa? Ninakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli mkandarasi huyu anakichofanya ni sanifu jenga Barabara ya Kyerwa kwenda Omurushaka. Nimwagize Meneja na Mhandisi Mshauri anayemsimamia ahakikishe kwamba huyu mkandarasi, kwa sababu alikwishalipwa fedha ya awali, aweze kwenda kwa kasi inayotakiwa kulingana na mpango wake wa kazi ambao ameupanga na tumeukubali. (Makofi)
MHE. KHALID M. NSEKELA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi ya kuuliza swali hili la nyongeza. Kwanza naishukuru Serikali sikivu ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia wahudumu 58 katika dirisha hili la ajira za afya kwa Wilaya ya Kyerwa.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, Kituo cha Afya cha Nkwenda ni kikubwa na kinatoa huduma zaidi ya Kata 19 na sometime kinatoa huduma nje ya Wilaya ya Kyerwa, lakini kituo hiki hakina gari ya uhakika ya wagonjwa (ambulance), je, ni lini Serikali itatupatia gari la uhakika kwa ajili ya kutoa huduma safi kwa kituo hicho? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT.JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, tunakumbuka sote humu ndani katika kipindi cha miaka mitano Serikali imenunua jumla ya magari ya kubebea wagonjwa 316, pamoja na magari ya wakaguzi 212 na ambulance za awamu ya kwanza tumeshazigawa katika Halmashauri ambazo ziliainishwa. Nimhakikishie kuwa, awamu ya pili kituo hiki kitakuwa wanufaika wa gari la ambulance.
MHE. KHALID M. NSEKELA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, je, kwa kuwa Wilaya ya Kyerwa imekuwa na changamoto ya muda mrefu ya huduma ya maji, Serikali haioni haja ya kuifanya Wilaya ya Kyerwa kuwa kanda maalum ya usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya maji?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuambatana na mimi na kufika Kyerwa kujionea changamoto ya maji iliyokuwa? Ahsante sana.
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge. Kwa kweli moja ya ajenda yake katika Bunge hili ni kuhusu suala zima la Wanakyerwa kuweza kupata huduma ya majisafi na salama. Sisi kama Wizara ya Maji ni wilaya ambayo tumeiangalia kwa kina sana. Ni moja ya wilaya tulizoifanyia tathmini, hasa katika kipindi hiki kwamba ni wilaya ambayo ina vijiji takribani 99, tumeshafikisha zaidi ya vijiji 55. Ipo miradi ya kimkakati ambayo tunaitekeleza katika kuhakikisha wananchi wa Kyerwa wanapata huduma ya majisafi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunao mradi wa Runyinya-Chanya zaidi ya shilingi bilioni 3.7, Kimuli-Nyanga zaidi ya shilingi bilioni mbili, Kaisho-Isingiro zaidi ya shilingi bilioni 1.9. Ninataka niwahakikishie, tutaisimamia Wanakyerwa waweze kupata huduma ya majisafi na salama, na mimi baada ya Bunge nipo tayari kuongozana na wewe kufika katika jimbo lako la Kyerwa. Ahsante sana.
MHE. KHALID M. NSEKELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ninashukuru kwa majibu mazuri kutoka kwa Naibu Waziri. Kwa kuwa, Wilaya ya Kyerwa inaongoza kwa uzalishaji mkubwa wa zao la kahawa, na ni zao ambalo linaongoza kwa kuingiza fedha za kigeni, je, Serikali haioni kwamba, ni muda muafaka sasa kuifanya Kyerwa iwe sehemu ya kipaumbele na kimkakati kwa ajili ya uzalishaji wa zao hili la kahawa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninampongeza kaka yangu Khalid Mussa Nsekela, Mbunge wa Kyerwa, kwa swali lake la msingi. Namthibitishia tu kwamba, Kyerwa ni miongoni mwa halmashauri ambazo sisi Wizara ya Kilimo tunaziangalia kwa jicho la karibu. Ndiyo maana utaona katika miaka hii miwili tu ya fedha, tumepeleka miche mingi, na bado tutaongeza, lakini siyo katika halmashauri yake tu, yaani ni katika ule Mkoa mzima wa Kagera. Ni moja ya mikoa ambayo sasa tunafufua kabisa zao la kahawa kwa sababu, ni zao ambalo linatuletea fedha nyingi za kigeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hilo lipo ndani ya mipango, na tunaendelea kutekeleza kwa kuongeza hizo pembejeo, miche pamoja na Maafisa Ugani katika eneo lake. Ahsante sana.
MHE. KHALID M. NSEKELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru. Barabara ya Nkwenda, Kakanja, Kimuli hadi Mabira ni barabara kiungo kikubwa sana katika shughuli za uchumi kwa Jimbo la Kyerwa. Je, Serikali ina mpango gani wa kuikarabati na kuijenga ili shughuli hizo ziendelee?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo barabara ambazo orodha yake tumeshazipokea kwa ajili ya ukarabati na ujenzi katika halmashauri mbalimbali, likiwemo Jimbo la Kyerwa. Pia zipo barabara ambazo tunaendelea kuzifanyia tathmini kwa ajili ya kuzifungua kwa maana ya barabara mpya kulingana na mahitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, barabara hizo ambazo tayari zipo kwenye jimbo letu na zipo kwenye mtandao huo unaohudumiwa na TARURA, tutaendelea kuzitengea fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa Serikali inaendelea na tathmini za mwisho za athari ya mvua kwenye barabara hizo ili fedha ianze kutengwa na kupelekwa kwa awamu kwa ajili ya kufanya marekebisho; na tutahakikisha pia barabara hiyo ya Mheshimiwa Mbunge tunaipa kipaumbele.