MHE. GRACE E. MKOMA aliuliza:-
Je, lini Serikali itajenga uwanja mkubwa wa ndege Singida?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Grace Elias Mkoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza utekelezaji wa hatua za awali za uthamini wa mali za wananchi wanaozunguka eneo la Kiwanja cha Ndege cha Singida, kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa eneo stahiki kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo. Zoezi hili linafanyika kwa kuzingatia kikamilifu matakwa ya sheria, kanuni na taratibu za nchi, ili kulinda haki na stahiki za wananchi husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara baada ya kukamilika kwa taratibu za utwaaji wa eneo hilo, Serikali itaanza hatua zinazofuata za maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kiwanja hicho, ikiwemo upatikanaji wa rasilimali fedha kwa lengo la kuboresha huduma za usafiri wa anga, kuongeza fursa za kiuchumi na kuimarisha maendeleo ya Mkoa wa Singida na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.