MHE. GRACE E. MKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Je, ni lini mchakato rasmi utakamilika ili uwanja wa ndege wa Mkoa wa Singida uweze kujengwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, nini mkakati wa Serikali kufungua anga ili sasa ndege yetu ya Air Tanzania ili iweze kusafiri mfano katika nchi za Morocco, Uturuki na Vietnam kwa sababu nchi hizo zina fursa za kiuchumi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Uchuzi napenda kujibu maswali ya nyongeza mawili ya Mheshimiwa Grace Elias Mkoma, Mbunge wa Viti Maalum kama ambavyo ameulizia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza nampongeza Mheshimiwa Grace Mkoma kwa kutambua umuhimu wa Uwanja wa Ndege wa Mkoa wa Singida na kuendelea kuwa sauti makini ya wanawake na viongozi na wananchi na hii ni kutokana na ukweli kwamba Mheshimiwa Grace anatambua kwamba Mkoa wa Singida kwanza uwanja wake ni mbadala na ni sehemu ya jirani kutoka Dar es Salaam, lakini pia kuna fursa za madini, kilimo, ufungaji pamoja na mambo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Grace Mkoma na wananchi wote wa Mkoa wa Singida kwamba Serikali kwa kutambua umuhimu wa uwanja huu wa Singida imekwishaanza kwanza kwa kutambua eneo kama nilivyosema na hatua inayofuatia sasa ni kukamilisha taratibu za utwaaji wa ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na hivi navyozungumza katika bajeti iliyosomwa hapa Bungeni mwezi huu wa tano na Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Mbarawa Makame Mnyaa amewahakikishia Wana-Singida katika mwaka wa fedha 2026/2027 tunakwenda kuanza taratibu mbalimbali kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi huo. Nimuombe Mheshimiwa Grace awe na uvumilivu wakati Serikali inafanyia kazi jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; pia nampongeza kwa kuendelea kupigania ndege yetu Shirika letu la Air Tanzania ambalo ndiyo shirika kubwa kwa nchi yetu na la Serikali ameuliza ni mkakati gani uliowekwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza kabisa mkakati wa kwanza ni kuingiza kwenye Ilani ya CCM, Serikali ya CCM kupitia aliyekuwa mgombea ambaye ndiye Rais wa nchi, aliwaambia Watanzania anakwenda kuongeza ndege zilizokuwepo na zitakazokuwepo ili ziweze kuwa nyingi zaidi; zaidi ya ndege nane katika kipindi cha miaka mitano hii ijayo hii ni kuongeza uwezo wetu wa kutoa huduma, lakini pia ili kuhakikisha kwamba jambo hili linakwenda kutekelezeka mwaka wa fedha wa 2026/2027 Serikali imejipangia kwenda kuongeza mtandao huo kutoka safari za ndani na nje na za kimataifa 33 zilizopo mpaka kufika 47.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ambapo ukiangalia hadhi iliyokuwepo miaka kumi iliyopita na sasa unaona kabisa vituo vingi vinaongezeka na hapa Bungeni mmesikia matamko ya Wizara jinsi ambavyo tunaongeza ndani ya nchi, tunakwenda Geita tunaunganisha Mwanza na Dodoma na maeneo mengine, pamoja na maeneo mengine ya nje ya nchi ikiwemo visiwa Sychelles na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inayo mpango wa kwenda mahali pengi zaidi ili kuhakikisha kwamba tunanufaika na fursa ambazo ziko kwenye nchi yetu, lakini mwisho tutaendelea kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha kwamba shirika letu linakwenda kuongeza mtandao zaidi ndani na nje ya nchi yetu.