Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Kijakazi Mohamed Yunus (5 total)

MHE. KIJAKAZI Y. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Naomba kufahamu wananchi wa Kata ya Nanjirinji Wilayani Kilwa Mkoani Lindi wamekuwa wakipata adha ya kuvuka Mto Mbwemkuru kuelekea Wilaya ya Ruangwa kwa ajili ya kufuata huduma za dharura. Daraja hili lilisombwa na masika mwaka 2024. Sasa nataka kufahamu, je, ni lini Serikali itajenga daraja hili ili kuwaondolea wananchi hawa adha hususan wanawake wajawazito?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge, na bahati nzuri hilo daraja nilipita kabla na hata baada ya kusombwa. Ni barabara ambayo inaunganisha Ruagwa – Nanjirinji hadi Kiranjeranje.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ule mpango wa kujenga madaraja ya dharura, kulikuwa na madaraja matatu katika hiyo barabara. Moja, ni hilo Mbwemkuru ambayo ni daraja kubwa, mto mkubwa, na pia tuna Daraja Nakiu na Kigombo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Nakiu na Kigombo yamekamilika. Hili daraja la Mbwemkuru liko kwenye mpango wa kujengwa na mfadhili wa World Bank kwenye kuratibu mradi unaoitwa CRW; inavyosema, mkandarasi ameshapatikana kwa ajili ya kuanza kulijenga hilo daraja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni taratibu tu, zikikamilika na wenzetu wa World Bank, daraja hilo linaweza kujengwa ili kuondoa hiyo adha, ahsante.
MHE. KIJAKAZI Y. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona na kunipa nafasi ili nami niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo kwa barabara iliyoelezwa hapa, Barabara ya Ngongo – Milola – Michiga kwa muda mrefu sana imekuwa ikiahidiwa kujengwa kwa kiwango cha lami. Pamoja na jitihada za Serikali za kufanya marekebisho mara kwa mara, ningependa kufahamu, ni lini Serikali itajenga barabara hii kwa kiwango cha lami, ukizingatia kwamba barabara hii ni muhimu kwa uchumi wa Jimbo la Lindi Mjini, Mchinga na Jimbo la Ruangwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali hili. Nimuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Lindi kuwa kama alivyosema, barabara hii inaunganisha majimbo mawili; Jimbo la Mheshimiwa Salma na Mheshimiwa Mmuya. Wamekuwa pia wakifuatilia sana kuhusu ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami. Tumekwishafanyia usanifu na sasa tunatafuta fedha tuijenge kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kati ya barabara zetu ambazo sasa hivi tunatafuta teknolojia mpya ambayo ni rahisi kujenga barabara kwa kiwango cha lami. Hii ni moja ya barabara ambayo ipo kwenye mpango wa kuifanyia pia majaribio katika hiyo teknolojia mpya. Kwa hiyo, tuna uhakika wakati tunatafuta fedha, lakini pia imeingia kwenye mpango wa kufanyia majaribio, hii tunayosema teknolojia mpya ya barabara.
MHE. KIJAKAZI Y. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa usambazaji maji Liwale Mjini ambao ulianza kutekelezwa mwaka 2024 kwa ahadi ya kukamilika mwaka 2025, mpaka sasa haujakamilika kwa sababu ya uhaba wa pesa. Katika shilingi bilioni 6.9 zimekwenda shilingi milioni 400 tu. Je, ni nini mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba wanapeleka pesa ili mradi ule uweze kukamilika na kuwaondolea adha ya maji wananchi wa Liwale hususan akina mama? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, miradi hii hakuna utakaosimama. Tunachokifanya ni kuhakikisha kwamba tunaweka mkakati wa kwenda awamu kwa awamu. Tunayo miradi kama ambavyo tumekuwa tukisema, miradi ambayo imefikia hatua nzuri 90%, 85% ni lazima tuitoe itoe matokeo halafu tunakuja katika miradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua mradi huo ni muhimu sana na wa kimkakati katika eneo hilo. Nakuhakikishia Mheshimiwa Mbunge, tunaenda kuweka msukumo wa kutosha kwa kupeleka fedha katika mradi huo ili wananchi waweze kupata huduma ya maji safi na salama utakapokamilika, lakini tunafahamu kwamba hatuwezi kutoa fedha kwa miradi yote inayoendelea nchi nzima ambayo yapata miradi 867 ambapo tukaweza kutoa pesa kwa pamoja.

Kwa hiyo, ni lazima tukibaliane tuwe na subira kidogo, tutaenda awamu kwa awamu, tutapeleka fedha awamu kwa awamu na mradi utaweza kukamilika bila kuwa na changamoto yoyote. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. KIJAKAZI Y. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi, ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Tunafahamu kwamba, hakuna mpango wa Serikali ambao hauna timeframe kwa hiyo, na mimi ningependa kuuliza swali, kama ilivyo kwa Jimbo la Mheshimiwa Magembe kule Wilaya ya Kilwa, hususan eneo la Kilwa Masoko, wanakabiliana na changamoto ya namna hii.

Mheshimiwa Spika, upanuzi wa airport umeahidiwa kwa muda mrefu sana, maeneo ya watu yamechukuliwa na mpaka sasa hawajalipwa fidia, wananchi wale wanaendelea kuteseka. Napenda kufahamu, ni lini wananchi wa Kilwa Masoko watalipwa fidia ili waweze kuendelea na maisha yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo Mheshimiwa Kijakazi amezungumza, ni kweli kabisa. Serikali kwa kutambua umuhimu wa eneo la Kilwa Masoko kuendeleza kiwanja kile, tulishatazama takribani wananchi karibu 600, na fedha tuliainisha. Siyo eneo hilo tu moja peke yake, tayari na maeneo mengine ya viwanja vya ndege nchini ambayo tumeona ni muhimu kwenda kuyaendeleza tumekamilisha kufahamu mahitaji, tumepeleka Wizara ya Fedha.
Mheshimiwa Spika, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge, kulingana na upatikanaji wa fedha, tunakwenda kulipa fidia katika eneo hili.
MHE. KIJAKAZI Y. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini tulimsikia pia jana Mheshimiwa Waziri Mkuu akitoa maelezo yanayofanana na haya. Ningependa kufahamu, au ningependa kuuliza maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mosi, kama ilivyoeleza Serikali kwamba wako kwenye majadiliano ambayo yanaelekea ukingoni kwenda kusainiwa kwa mkataba, je, Serikali imeweka mkakati gani wa kuhakikisha kwamba wanatoa elimu, sambamba na uwezeshaji kwa wananchi wa Tanzania hususan wanawake wa Mkoa wa Lindi pamoja na vijana ili kuhakikisha kwamba wanaweza kuzipata fursa, hususan zile zinahusiana na sheria ya local content ili waweze kunufaika na mradi huu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Mwaka 2023/2024 Wizara ya Nishati iliingia makubaliano na Wizara ya Elimu kupitia Arusha Technical College kwa ajili ya ujenzi wa chuo kitakachofundisha masuala ya nishati na mafuta; na Halmashauri ya Manispaa ya Lindi ilitoa eneo lenye ukubwa wa square meter 256,000 katika eneo la Kikwetu pale Lindi. Kwa mujibu wa makubaliano, ilikuwa ujenzi wa chuo kile ujengwe haraka iwezekanavyo ...

SPIKA: Mheshimiwa twende kwenye swali lako.

MHE. KIJAKAZI Y. MOHAMED: ...lakini mpaka sasa bado ujenzi haujaanza, ningependa kufahamu, je, ni lini ujenzi wa chuo kile utaanza? La, kama Serikali haipo tayari, kwa nini, isirejeshe eneo lile kwa manispaa ili waendelee na shughuli nyingine, ikiwemo kuuza maeneo yale ili manispaa iweze kupata mapato?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Kijakazi Mohamed, almaarufu Binti Lindi kwa kazi kubwa anayoifanya ya kufutilia mradi huu wa LNG. Ninajua kuwa anafanya hivyo kwa sababu anajua kuwa huu ni mradi wa kihistoria ambao ukifanikiwa kuanza mikoa ya kusini itabadilika sana kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza, linahusiana na kuwajengea uwezo wanawake na wananchi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara. Sasa Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, inaendelea kutoa elimu kupitia VETA, SIDO na vyuo vingine, lakini pia kuna ujenzi mkubwa wa shule ya amali unaendelea kwa ajili ya kutoa elimu juu ya namna ambavyo wananchi wanaweza kuchangamkia fursa zitokanazo na mradi huu wa LNG ambao utaanza hivi karibuni.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na chuo cha elimu ya juu ambacho Mheshimiwa Mbunge amekitaja, ni kweli. Kwanza tunawashukuru Wanalindi kwa kutoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa chuo hiki; na hii ni kwamba elimu juu ya uchakataji wa mafuta na gesi bado ni jambo geni kidogo katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, ninawapongeza kwa hilo, na Serikali ina nia ya dhati ya kuhakikisha kwamba chuo hiki kinajengwa ili wananchi waweze kupata ujuzi na kushiriki katika mradi huu wa kimkakati na tutafanya hivyo kwa kadri ambavyo upatikanaji wa fedha utakavyowezekana. Ninaomba kuwasilisha.