Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. George Venance Lugomela (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. DKT. GEORGE V. LUGOMELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa hii fursa ili niweze kutoa mchango wangu katika hoja hii muhimu ambayo tuko nayo hapa. Kwanza, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kwa ajili ya kuchangia hoja ambayo ipo mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuleta maendeleo ya nchi hii. Tunafahamu kwamba Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiye mwanamazingira namba moja; na ameendelea kutoa miongozo ya usimamizi wa mazingira ikiwa ni pamoja na kupanda miti siku ya birthday yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Makamu wa Rais Dkt. Emmanuel John Nchimbi, tunafahamu kwamba ndiye mkuu wa ofisi hii ya hoja tunayoijadili leo. Kwa hiyo miongozo yake pamoja na maelekezo yake pia yamo kwenye hoja ambayo tunaijadili leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia nimpongeze Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kwa kazi kubwa anayoifanya. Waziri Mkuu ndiye kiongozi wa shughuli za kila siku za Serikali, kwa hiyo maana yake ni kwamba, hata tunayojadili kwenye hoja ya leo pia Waziri Mkuu ana maelekezo yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Waziri wa sekta hii Mheshimiwa Hamad Masauni kwa hotuba aliyoiwasilisha hapa na kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuhakikisha kwamba mazingira yanatunzwa, lakini pia Muungano unalindwa. Nimpongeze pia Naibu Waziri wa sekta hii, Mheshimiwa Reuben Kwagilwa kwa kazi kubwa anayoifanya kumsaidia Mheshimiwa Waziri. Niwapongeze pia watendaji wote, Katibu Mkuu, Manaibu Katibu Mkuu wawili, Wakurugenzi pamoja na watendaji wote katika sekta hii ya Muungano na Mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajielekeza zaidi katika sekta ya mazingira. Sekta ya mazingira ni pana, lakini pia sekta hii ni changa. Kwa maana ya kwamba ni kuanzia katikati ya miaka ya 90 ndipo mazingira yameanza kutiliwa mkazo. Maana yake ni kwamba kazi kubwa imefanyika. Sheria ya mazingira ilikuja 2004, kazi kubwa imefanyika; lakini bado kuna mambo mengi kwa sababu tunashuhudia uharibifu wa mazingira na mambo mengine mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzijuzi tumeona maporomoko yaliyotokea kule Kyela, lakini miaka kadhaa iliyopita tuliona maporomoko yaliyotokea kule Manyara. Ukiangalia vizuri utaona kwamba haya pia pamoja na mabadiliko ya tabianchi lakini yana uhusiano na mazingira, ukataji wa miti na uondoshaji wa uoto wa asili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajielekeza mchango wangu katika eneo la mazingira. Changamoto kubwa ninayoiona katika sekta hii ya mazingira, hatujaweza kuwa na vyanzo vya kutosha vya mapato kuwezesha sekta hii isimamiwe vizuri. Ukiangalia idara ya mazingira chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, fedha nyingi inazotegemea kwa ajili ya kuendesha shughuli zake za maendeleo ni kutoka kwa wafadhili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kutokana na changamoto ya sera za wafadhili kubadilika, wakati mwingine kuchelewa kutolewa kwa fedha hizi baadhi ya miradi haitekelezwi; kwenye taarifa ya Kamati hilo limebainishwa. Kwa hiyo maana yake tunahitaji kufikiria namna ya kuongeza mapato katika sekta hii ya mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kuwa Baraza la Usimamizi wa Mazingira linajiendesha kwa tozo na faini mbalimbali ambazo linatoza katika kutekeleza shughuli zake; lakini bado hela inayopatikana haitoshi kuendesha shughuli za mazingira kwa upana wake na ukubwa wa tatizo hili. Kwa hiyo, ninaomba nipendekeze maeneo machache ambayo tunaweza tukayatilia mkazo na kuweza kupata fedha kwa ajili ya kusimamia shughuli za mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao Mfuko wa Mazingira Environmental Trust Fund; lakini Mfuko huu bado vyanzo vyake vya mapato ni vidogo na haviwezi kukidhi haja ya usimamizi wa shughuli za mazingira hapa nchini. Kwa hiyo, ninashauri tuongeze wigo wa tozo kama vyanzo vya mapato kwa ajili ya Mfuko wa Mazingira na fedha zinazopatikana zitumike kwa ajili ya usimamizi wa mazingira nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao wachafuzi wengi wanaochafua mazingira yetu. Imeelezwa hapa habari ya migodi, lakini pia vipo viwanda ambavyo vinachafua mazingira. Kuna baadhi ya viwanda vina mitambo ya kutibu majitaka lakini vingine havina. Maana yake ni kwamba, wanatiririsha majitaka kwenye mazingira. Ninafahamu kwamba NEMC wamekuwa wakitoza tozo kwenye maeneo haya, lakini viwanda vingi havijafikiwa na migodi mingi bado inatiririsha majitaka na maeneo mengine hatuwezi kuyafikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, NEMC inashindwa kuwafikia kwa sababu, NEMC iko kwenye kanda peke yake, haiko kwenye mikoa na wala haiko kwenye wilaya. Kwa hiyo, wanashindwa kuweza kuwa mahali ambapo matatizo haya yametokea. Wanaweza kuwakamata wachache lakini wengi wanachoropoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili tunayo ile kanuni inasema polluter pays principle, mchafuzi lazima alipe. Ninashauri NEMC isimamie hili na fedha inayopatikana sehemu yake iende kwenye Mfuko wa Mazingira ili kuwezesha fedha kwa ajili ya usimamzi wa mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo eneo ya uchumi wa kijani (green economy), hili ni eneo ambalo tukiliboresha makampuni yanaweza yakawekeza katika kufanya uchumi wetu uwe wa kijani. Kwa hiyo, takataka zile tuanazokusanya nyingi zinaweza zikabadilishwa kuwa nishati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo miongozo isimamiwe vizuri ili tuweze kuwa na kampuni nyingi ambazo zinaweza kugeuza taka kuwa nishati au tunaita urejelezaji wa taka katika maeneo mbalimbali na hivyo taka zile zisiweze kuchafua mazingira yetu. Vilevile kampuni zile zinaweza kutoa ajira pamoja na mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo pia eneo la biashara ya kaboni. Biashara ya kaboni inazidi kukuwa duniani na nchi yetu bado haijaweza kutumia fursa ya biashara ya kaboni vizuri; kwa maana ya carbon credit. Tunayo misitu mingi katika maeneo mbalimbali nchini ambayo inafyonza ile hewa ya ukaa; na kwa mujibu wa makubaliano tunaweza tukapata fedha kwa ajili ya kutunza ile misitu. Fedha zile zikipatikana zitatoa motisha kwa wananchi wetu ili wasiharibu misitu kwa sababu wanajua kwamba wanapata kipato kwa kutunza misitu. Kwa hiyo, hili ni eneo ambalo litiliwe mkazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwamba kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri nimeona kwamba amelitaja hili. Sambamba na hilo, kile kituo cha kuratibu biashara ya kaboni, National Carbon Monitoring Centre, tunaomba kiimarishwe ili kiweze kuratibu biashara hii pamoja na kutoa elimu kwa wananchi na taasisi mbalimbali kuhusu fursa ambazo tunaweza kuzipata katika biashara ya kaboni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika biashara ya kaboni siyo misitu peke yake. Tunafahamu kwamba nishati safi inapunguza hewa ya ukaa ambayo ndiyo kaboni yenyewe. Maana yake ni kwamba, juhudi anazozifanya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha kwamba tunatumia nishati safi maana yake ni kwamba, tunaweza tukapata fedha kutoka kwenye Mifuko ya Mabadiliko ya Tabianchi kwa kupunguza hiyo hewa ya ukaa. Kwa hiyo, hili ni eneo ambalo linahitaji kutiliwa mkazo ili tuweze kuongeza mapato kwenye...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. DKT. GEORGE V. LUGOMELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho dakika moja tu, ninaomba niongee kwamba, elimu kwenye jamii inabidi itiliwe mkazo ili kuweza kudhibiti mazingira yetu vizuri. Kwa sababu wananchi wakielewa maana yake ni kwamba watatekeleza sheria bila shuruti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)