Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
| Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date | 
|---|---|---|---|---|---|---|
| 2015-2020 | Session 3 | Sitting 49 | Justice and Constitutional Affairs | Maswali kwa Waziri Mkuu | 5 | 2016-06-23 | 
 
									Name
Mohamed Omary Mchengerwa
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Rufiji
Primary Question
						MHE.     MOHAMED     O.     MCHENGERWA: 
Mheshimiwa     Naibu     Spika, nakushukuru.  Kwa  kuwa,  Sera  na  Mifumo  ya  Kisheria  tuliyonayo  sasa  inaruhusu kuwaenzi  waasisi  pamoja  na  viongozi  wa  nchi  hii,  lakini  siku  za  hivi  karibuni Mheshimiwa  Waziri  Mkuu,  imejidhihirisha  wazi  kwamba  baadhi  ya  viongozi 
wameingia katika dimbwi la wizi, ubadhirifu  wa mali za Umma na ukiukwaji wa maadili:-
Je, ni lini Serikali itafanya mapitio ya Sera, Sheria na kubadilisha mifumo ili sasa   wale   wezi   wote   waweze   kuchukuliwa   hatua   kali   za   Kisheria   na watakaobainika  hivyo  dhidi  ya  ukiukwaji  wa  maadili  ya  nchi  hii?  Ahsante.
					
 
									Name
Kassim Majaliwa Majaliwa
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Ruangwa
Answer
						WAZIRI   MKUU: 
Mheshimiwa   Naibu   Spika,   naomba   kujibu   swali   la Mheshimiwa Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa  Naibu  Spika,  Serikali  inaendelea  kudhibiti  vitendo vya  wizi, kukosa  uadilifu,  kukosa  uaminifu  mahali  pa  kazi  na  Watumishi  wa  Sekta  ya Umma.  Serikali  inafanya  hilo  bila  kujali  ngazi  ya  mtumishi  huyo,  awe  ni  kiongozi wa  ngazi  ya  juu,  wa  kati,  hata  wale  watumishi  wa  kawaida,  ilimradi  Serikali imetoa   dhamana ya   kuwatumikia   Watanzania,   tunatarajia   kila   mtumishi atakuwa mwadilifu, mwaminifu, lakini pia atakuwa mchapakazi. 
Mheshimiwa  Naibu  Spika,  Serikali  inaendelea  kuchukua  hatua  kali  dhidi ya   wale   wote   wanaokiuka,   dhidi   ya   wale   wote   ambao   hawatumii   vizuri madaraka  yao,  dhidi  ya  wale  wote  wanaojihusisha  na  vitendo  vya  rushwa popote pale nchini. 
Mheshimiwa  Naibu  Spika,  Serikali  imeendelea  kuchukua  hatua  kadhaa, kama    ambavyo    Mheshimiwa   Mbunge    ametaka    kuona    ni    hatua    gani zinachukuliwa;  kwanza,  tunaendelea  kutoa  elimu  kwa  watumishi  ya  kwamba kila  mtumishi  anatakiwa  kufuata  maadili  ya  utumishi,  ikiwemo  na  uaminifu, uadilifu na uchapakazi. 
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Serikali inaendelea kuboresha kwa kuunda; na tumeshaunda Taasisi ya Utumishi wa Umma, Taasisi ya Maadili ya Watumishi ambayo yenyewe inajiridhisha kwamba kila mtumishi anatangaza mali zake na kuendelea kufuatilia mara kwa mara mabadiliko ya mali hizo ili tuone kama mali hizo amezipata kwa utumishi wake huu alionao. 
Mheshimiwa  Naibu Spika,  siyo  hivyo  tu,  Serikali  imeendelea  kuimarisha 
taasisi  mbalimbali  ikiwemo  na  Taasisi  ya  Kuzuia  na  Kupambana  na  Rushwa 
ambayo  pia  inafuatilia  maeneo  yote;  kwa  Watumishi  wa  Umma  na  hata  raia 
wa kawaida. 
Mheshimiwa  Naibu  Spika,  pia  tunafanya  mapitio  ya  lile  jambo  ambalo Mheshimiwa  Mbunge  amelisema  la  Sera  yetu  na  Sheria,  Kanuni  ili  ziweze kuendana na mabadiliko ya wakati. Hii pia, ili kuisaidia Serikali kudhibiti tabia hii, sasa  Serikali  kupitia  Bunge  hili,  siku  mbili  tatu  zijazo  mtapitisha  Muswada  wa kuanzisha Division ya  Mahakama  ya  Mafisadi  ili  kuweza  kupambana  nao  kwa lengo la kudhibiti vitendo vya Watumishi wa Umma wenye tabia ya kuiba fedha mahali  pa  kazi,  lakini  wale  wenye  vitendo  vya  ufisadi  ili  wote  hao  waweze 
kuchukuliwa hatua. 
Mheshimiwa  Naibu  Spika,  kwa  hiyo,  kwa  mbinu  hizi,  kwa  njia  hizi  zote, tutaweza  kuwa  na  Watumishi  wa  Umma  wenye  maadili  mema  na  wenye kutumia madaraka yao vizuri. 
Mheshimiwa  Naibu  Spika,  malengo  yetu  Serikali  ni  kuhakikisha  kwamba Watanzania   wanahudumiwa   vizuri   na   Watanzania   wawe   na   uhakika   na Watumishi waliopo kwa kutekeleza wajibu wao kwa Watanzania wote bila kuwa na vitendo ambavyo vinaweza kuathiri utendaji wa kila siku. 
					
 
											Name
Mohamed Omary Mchengerwa
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Rufiji
Question 1
MHE.     MOHAMED     O.     MCHENGERWA: 
Mheshimiwa     Naibu     Spika, 
Mheshimiwa   Waziri   Mkuu   nakushukuru   sana   kwa   majibu   mazuri   ambayo ninaamini yamekidhi kiu ya Watanzania wengi wanyonge, hususan Watanzania ambao  wamekuwa  wakikosa  maendeleo,  hususan  wa  Jimbo  langu  ya  Rufiji. 
Ninaamini  sasa Sheria  hii  itaweza  kusaidia  upatikanaji  wa  maendeleo  kwa Jimbo  langu  la  Rufiji,  hususan  ujenzi  wa  Barabara  ya  Nyamwage –
Utete. 
Mheshimiwa  Naibu  Spika,  ufafanuzi  tu  kuhusiana  na  hilo,  labda  ni  kama ombi tu  kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu  kwa sababu majibu ni mazuri, ni lini sasa Serikali  itaamua  mambo  haya  ya  maadili  yaingie  katika  Mitaala  ya  Shule  za Sekondari na Shule za Msingi ili vijana wetu wawe na maadili? Msingi wa maadili uanzie Shule za Msingi na Sekondari. 
 
											Name
Kassim Majaliwa Majaliwa
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Ruangwa
Answer
								WAZIRI MKUU: 
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza 
la Mheshimiwa Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napokea ombi lako na ni ombi zuri kwamba, ili 
tujenge  maadili  mema  tunatakiwa  tuanze  kutoka  ngazi  za  chini,  lakini  njia ambayo  tumeitumia  ni  kwamba,  watumishi  wetu  hawa  ambao  pia  wameapa kuwa  watumishi  wenye  maadili  mema,  wakiwemo  Walimu  ambao  wanafanya kazi yao kwa weledi mkubwa, ndio ngazi ya awali ambayo wanasimamia vizuri vijana  wetu  kutoka  ngazi  ya  shule,  wanawalea  watoto  wetu,  wanawasimamia kuwa  na  nidhamu,  kuwa  waadilifu,  lakini  pia,  wanadhibiti  vitendo  vya  wizi miongozi  mwao  ni  sehemu  ya  mafunzo  tosha  ikiwa  ni  sehemu  ya  malezi ambayo yanatolewa na ngazi hii.
Mheshimiwa  Naibu  Spika,  kwa  hiyo,  tutaendelea  kuimarisha  mabadiliko 
ya mitaala yetu kwa kuingiza maeneo haya ya utumishi bora, maadili mema ili tupate  Watanzania  wengi  wenye  maadili  na  hatimaye  huko  mbele  tuweze kujihakikishia  na  shughuli  zote  za  maendeleo  nchini  tukiamini  kwamba  kila mmoja  atakuwa  amelelewa  vizuri  kwenye  familia  yake  anapokwenda  shuleni na  pia  hata  kwenye  utumishi  kufuata  pia  Sheria  na  Kanuni  ili  kuleta  matokeo mazuri. Ahsante sana. 
							
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved