Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
| Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
|---|---|---|---|---|---|---|
| 2025-2030 | Session 3 | Sitting 43 | Works and Transport | Maswali kwa Waziri Mkuu | 1 | 2026-06-04 |
Name
Haran Nyakisa Sanga
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Kigamboni
Primary Question
MHE. HARAN N. SANGA: Mheshimiwa Spika, kwanza ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali kwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu kwanza ninakupongeza sana kwa kazi nzuri ambayo unafanya katika kutatua changamoto mbalimbali za wananchi hapa Tanzania. Hata mimi nilivyokuwa nina shida zangu za kivuko pale Kigamboni nikakwambia ukaniambia kesho nakuja, na ulifika ukaongea na wale wananchi. Ninakupongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na wimbi kubwa la kukua kwa miji mikuu kama Arusha, Mwanza, Mbeya, Dodoma na Dar es Salaam; inakua kwa kasi kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, ninataka nijue, nini kauli ya Serikali katika kuimarisha miundombinu hususani ya kiwango cha reli ili kufanya miji hii iweze kukua kwa kasi kuendana na idadi ya wananchi, lakini pia kuongeza uchumi/kuchachua uchumi katika majiji haya hususan Jiji la Dar es Salaam? (Makofi)
Name
Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Magharibi
Answer
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa nafasi hii ili niweze kujibu swali zuri la Mheshimiwa Haran Sanga, Mbunge wa Kigamboni, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kabla sijajibu swali lake ninaomba uniruhusu niseme mambo mawili; jambo la kwanza ninaomba nitumie Bunge lako Tukufu kuwapongeza vijana wetu wa Serengeti Boys kwa hatua kubwa na yenye heshima waliyofikia katika mashindano ya vijana chini ya miaka 17, kwa kucheza hatua ya fainali tena yenye ushindani na kukosa tu bahati kwa kweli ya kulileta kombe hilo hapa nyumbani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninajua Watanzania watakuwa wamesikitika, lakini ninawatoa hofu, kwa sisi wafugaji ukiona kila siku wingu kubwa linakuja na mvua hainyeshi, kuna siku mvua itanyesha hata bila kuwa na wingu kubwa.
Mheshimiwa Spika, Yanga walikosakosa wakatolewa kwa uwiano wa magoli, Simba wakakosakosa kwa kushindwa tu mbinu za nje ya uwanja, na vijana jana wamekosa. Kuna siku kombe hilo linakuja na wala siyo siku nyingi litakuja hapa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili, ninatoa rai kwa Bunge lako Tukufu, wiki ijayo tarehe 11 Juni, siku ya Alhamisi itawasilishwa Bajeti Kuu ya Serikali hapa Bungeni. Ninatoa rai kwa Waheshimiwa Mawaziri na Wabunge wote kushiriki katika siku hiyo ya kusomwa Bajeti Kuu ya Serikali, lakini pia na katika majadiliano ya Bajeti Kuu ya Serikali. Bajeti Kuu ya Serikali ni bajeti ya nchi inayogusa maisha ya kila Mtanzania na mpaka majirani zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya maeneo hayo mawili, sasa ninaomba nijibu swali la Mheshimiwa Haran Sanga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuleta swali hilo. Ni kweli kuna kasi kubwa ya kukua kwa miji yetu kama alivyoitaja na kusababisha msongamano pamoja na kupoozesha shughuli za kiuchumi na kuongeza gharama za maisha.
Mheshimiwa Spika, pendekezo alilolitoa Mheshimiwa Mbunge ni moja ya hatua zinazostahili kuchukulia ili kuweza kupata ufumbuzi wa tatizo la aina hiyo na kurahisisha shughuli za kiuchumi kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema.
Mheshimiwa Spika, tayari Serikali imeanza kuchukua hatua; moja ikiwa ni kuchukua hatua za sasa za kuondoa misongamano katika miji yetu inayokua, na hatua hizo ambazo zimeanza kuchukuliwa kwa sasa ni kuongeza idadi ya barabara za ndani na kuzijenga kwa kiwango cha lami barabara za mitaa.
Mheshimiwa Spika, hatua nyingine inayochukuliwa imekuwa ya kujenga njia za mzunguko ili magari ambayo hayana ulazima kupita katikati ya miji hiyo yasipite, bali yatumie njia za mzunguko. Tumeshafanya hivyo kwa hapa Dodoma, ujenzi unaendelea kwa Iringa, ujenzi ulishakamilika kwa Arusha. Tuna mpango huo na shughuli zinaendelea kwa Mwanza, tuna mpango kama huo na shughuli zainaendelea kwa Mbeya; tuna shughuli ya aina hiyo Mkoa wa Ruvuma na maeneo mengine mengi ambako bypass zinajengwa. Kusudi lake ni ku-decongest, kuondoa misongamano katikati ya majiji yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hatua itakayofuata ni hiyo ya kuwa na reli kwenye majiji yetu na hatua za awali zimeshaanza. Katika baadhi ya mikoa kuna hatua za upembuzi zinaendelea, katika baadhi ya mikoa maandiko yanafanyika, lakini pia wakati hatua hizo zinaendelea Serikali inajipa muda wa kukamilisha miradi mikubwa ya kimkakati ya reli ambayo na yenyewe kusudi lake kubwa ni hilo hilo la kuweza kufungua uchumi, kama ambavyo mnajua Dar es Salaam – Dodoma operations zimeshaanza, lakini bado tunakazi ya kufungua hivi vipande viwili mpaka Tabora, Dodoma – Tabora; lakini pia na vipande viwili, kimoja cha katikati cha Tabora – Isaka, Isaka – Mwanza tuko hatua nzuri tunaelekea 70% sasa, lakini pia cha Tabora – Kigoma, Kigoma kuelekea nchi za jirani ya Burundi, lakini pia tuna kipande kingine cha kutokea Kaliua kwenda mpaka kule Mpanda.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kadiri hatua za kifedha zinavyoruhusu tutarejea kuwekeza pia kwenye ujenzi wa zile reli za ndani ya majiji yetu ili kuweza kufungua uchumi ndani ya majiji yetu. Serikali iko wazi kutumia hata njia za ubia katika kujenga reli hizo, sambamba na zile za mikoa mingine ambazo zimebainishwa katika ilani ya uchaguzi.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved