Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Question to Prime Minister

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2025-2030 Session 3 Sitting 43 Regional Administration and Local Government Authorities Maswali kwa Waziri Mkuu 2 2026-06-04

Name

Agnesta Lambert Kaiza

Gender

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami siku ya leo niweze kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu swali.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa Mheshimiwa Waziri Mkuu ninaomba pia nitumie nafasi hii kukupongeza sana kwa kazi nzuri unayoifanya ya kumsaidia Mheshimiwa Rais kwa ajili ya kuwafikia wananchi na kutatua kero zao. Ninakumbuka ulikuja Mkoa wa Dar es Salaam kwa udharura, lakini hakika uliacha tabasamu na bado tunakusubiri kwa hamu uje jimbo kwa jimbo, ili wananchi waweze kupata tabasamu moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa, swali langu ni kama ifuatavyo: Mheshimiwa Waziri Mkuu, nchi yetu imekuwa ikifanya chaguzi za halmashauri katika ngazi ya Udiwani kwa namna iliyo tofauti na nafasi nyingine, kwa maana kwamba nafasi Meya na Mwenyekiti wa Halmashauri hufanyika kila baada ya miaka mitano, lakini nafasi ya Naibu Meya na Makamu Wenyeviti wa Halmashauri hufanyika kila baada ya mwaka mmoja.

Mheshimiwa Spika, uchaguzi huu wa kila mwaka haujawahi kuizacha salama halmashauri zetu pamoja na Madiwani, kwani chaguzi hizi hupelekea misuguano, migongano, na jambo ambalo linapelekea hata utendaji kazi wa Madiwani wetu katika halmashauri kuzorota sana kwa sababu kila baada ya uchaguzi mmoja wao huanza kuingia katika michakato ya kampeni na hivyo shughuli za halmashauri kuzorota. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kwa nia njema ile ile ya Serikali ambapo Mheshimiwa Waziri Mkuu, mmekuwa mkifanya marekebisho kwenye sheria mbalimbali na kanuni mbalimbali, je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuleta marekebisho kwa hati ya dharura kabisa ili chaguzi hizi za hawa viongozi ziwe zinafanyika kila baada ya miaka mitano ili kuondoa hii sintofahamu ambayo kwa kweli halmashaur zetu Mheshimiwa Waziri Mkuu haziko katika hali nzuri? Ahsante sana. (Makofi)

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kujibu swali hili la Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Agnesta ameleta swali zuri na ni ukweli alichosema, ndiyo mambo yanayotokea katika halmashauri nyingi. Nadhani siku za nyuma pengine nafasi hiyo haikuchukuliwa kama nafasi rasmi sana, kwa hiyo, ilichukuliwa tu kwamba kwenye kikao kimojawapo tu kwa urahisi hivi Madiwani watakusanyika tu, watamchukua mmoja wapo awe Makamu Mweyekiti kwa ajili ya kumsaidia Mwenyekiti au Makamu Meya kwa ajili ya kumsaidia Mstahiki Meya.

Mheshimiwa Spika, kiuhalisia ni kweli imekuwa chanzo cha migawanyiko na chanzo cha migogoro katika maeneo mengi. Sasa inageuza kwamba shughuli inakuwa uchaguzi badala ya shughuli zile ambazo zinafanywa na uongozi huo unaopatikana. Kwa sababu hiyo, pana mantiki ya kuliangalia upya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata Bunge lako Tukufu, Wenyeviti wa Kamati wanachaguliwa Kamati zinadumu, ifikapo nusu ya uhai wa Bunge ninadhani ndiyo kunakuwa na uchaguzi mwingine wa Makamu. Mwenyekiti akishachaguliwa anakaa katika kipindi hiki cha uhai wa Kamati.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeona logic hii na nimepita mahali nimesema mara kadhaa, na nimeshamwelekeza Mheshimiwa Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia mambo ya TAMISEMI na bahati nzuri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali yupo, wakae na Mwanasheria Mkuu waiangalie upya sheria hiyo ili waweze kuleta mapendekezo kwa haraka, ikiwezekana Bunge lijalo ambalo litakuwa linapitia miswada, ili tuweze kuiangalia upya sheria hiyo na Bunge lako Tukufu liweze kufanya marekebisho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa Tanzania katika kuzunguka nimekuja kugundua wana kero nyingi ambazo nyingine zinaweza zikashughulikiwa ngazi za halmashauri, kama kila kamati itatimiza wajibu wake. Haya mambo yote wanayoyatoa pale yana kamati zake. Kamati zetu zingekaa vizuri na zikafuatailia mambo ya aina hiyo na zikapendekeza, kero hizi zingetatuliwa kitaasisi ambao ndiyo msingi wa utawala bora. Kutatua kero kitaasisi badala ya kutatua kwa dharura.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hii ni hoja ya msingi na nadhani panapo uzima tutakamilisha na huenda Bunge linalokuja tukawa na mapendekezo hayo ili Bunge lako Tukufu liweze kupitisha marekebisho haya. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, na sisi kama Wajumbe kwenye halmashauri zetu twendelee kusimamia misingi hii. Kwamba, uchaguzi umepita watu wote wajikite kwenye kufanya kazi. Tusiwe na nchi na wananchi wanaowaza uchaguzi kila siku. Uchaguzi si kazi, kuna kazi tunazotakiwa kufanya ili wananchi waweze kupata maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninayasema kwa wale Makamu ambao kila wakati wanagombea, lakini wapo pia hata wale Wenyeviti, anaapishwa leo uenyekiti wa halmashauri siku hiyo hiyo anaanza kampeni ya kutafuta Ubunge. Kila mtu afanyie kwanza kazi nafasi aliyopewa na ili watu waione kazi, waione kazi. Waione hiyo kazi na kama wananchi watakuwa wameridhika na hiyo kazi, watasema ndiyo huyu alikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri, lakini kwa sasa tunahisi anaweza akawa Mbunge, lakini siyo unaapishwa tu kesho yake unaanza kila siku unatoa rushwa sasa isiyojulikana na inayojulikana ili Madiwani wakuone wewe ndiyo Mbunge wakati Mbunge yupo, au ili Madiwani wakuone wewe ndiyo Makamu Mwenyekiti wakati Makamu Mwenyekiti yupo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii si kitu kizuri kwenye nchi ambayo wananchi wake wanakiu na maendeleo na siyo kiu ya kubadilibadili Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti ama Mbunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa nafasi hii. (Makofi)

Additional Question(s) to Prime Minister