Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Question to Prime Minister

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2025-2030 Session 3 Sitting 43 Livestock , Fisheries, Agriculture, Food Security and Cooperatives Maswali kwa Waziri Mkuu 3 2026-06-04

Name

Sara Msafiri Ally

Gender

Female

Party

CCM

Constituent

Mvomero

Primary Question

MHE. SARA M. ALLY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize kwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, na mimi ninachukua nafasi hii kukupongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa unayoifanya ya kumsaidia Mheshimiwa Rais kutatua kero za wananchi na ninakushukuru sana wananchi wa Jimbo la Mvomero umewakimbilia walivyopata mafuriko, uliwaletea chakula cha kutosha na huduma za dharura.

Mheshimiwa Waziri Mkuu nina swali, kama tunavyojua Dira ya Maendeleo ya Taifa imelenga itakavyofika mwaka 2050 uchumi wetu wa Pato la Taifa ufikie dola trilioni moja.
Mheshimiwa Spika, tunajua kwamba wananchi wengi wako vijijini na wanategemea kilimo katika kuongeza tija na kuongeza ukuaji wa uchumi, lakini tunajua kwamba zipo changamoto nyingi kwenye sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, je, Serikali sasa ina mpango gani kuwekeza kikamilifu kwenye kilimo cha umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji na kuweza kuchochea ukuaji na kuongeza viwanda na masoko na kuweza kufikia dhana hiyo ya ukuaji wa uchumi kwa sababu Sekta Binafsi itachangia 70% ya ukuaji wa dira hii? (Makofi)

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa nafasi hii ili niweze kujibu swali la Mheshimiwa Sara Msafiri kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Sara Msafiri ameleta swali zuri sana, ninampogeza sana. Kimsingi Kilimo cha Umwagiliaji kwa nchi ambayo zaidi ya 65% na kuendelea ya wananchi wake wakiwa wanajishughulisha na kilimo, ni ufumbuzi wa matatizo mengi. Moja, kilimo cha umwagiliaji kinaleta dhana halisi ya kukua kwa lile pato la mtu mmoja mmoja kiuhalisia badala ya wastani.

Mheshimiwa Spika, tunapopima masuala haya ya pato la mtu tunatumia wastani. Ukisema anapata dola 1,000 kwa siku ama per capita income yake ni hii, kwa kiwango kikubwa inakuwa wastani, lakini uwekezaji katika sekta ya umwagiliaji unaenda kukuza kipato kwa uhalisia cha mtu mmoja mmoja. Serikali imeanza kuchukua hatua hizo. Nimesema mojawapo ni hilo la kipato.

Mheshimiwa Spika, la pili, umwagiliaji unaenda kutoa suluhisho, kama mkulima alikuwa akilima mara moja kwa mwaka, anaingia kwenye shida ya uhaba wa chakula anahitaji chakula cha msaada, mkulima huyo jawabu analotakiwa kupewa siyo kupewa chakula tu cha msaada kila wakati, anatakiwa awezeshwe alime mara mbili ili chakula kiweze kutosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, katika nchi yetu kumekuwa na migogoro mingi ya ardhi, migogoro mingi kati ya wakulima na wafugaji, migogoro mingi kati ya vijiji na maeneo yaliyotengwa ya hifadhi na vinginevyo.

Mheshimiwa Spika, hii na yenyewe inatuambia kwamba ongezeko la watu ni kubwa na ardhi haiongezeki. Maana yake lazima iwepo njia ya kutumia, njia ya tofauti ya matumizi ya ardhi, kwamba badala ya kila siku kuongeza mashamba ili uongeze uzalishaji inatakiwa ije njia ya kuongeza uzalishaji kwa kutumia eneo lile lile kwa sababu ardhi haiongezeki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua hilo, Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imechukua jitihada za makusudi na za vitendo kwa kuongeza bajeti ya Serikali inayokwenda kwenye kilimo kwa zaidi ya mara tano na baada ya bajeti hiyo kuongezeka, sehemu kubwa imeelekezwa kwenye miradi ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, imefufuliwa miradi ya umwagiliaji ambayo ilikuwa imejaa tope na mingineyo ikiwa imevunjika vunjika, maeneo mengi imefufuliwa miradi hiyo ambapo kwa sasa tuna zaidi ya miradi 780 ambayo imefanyiwa kazi na mingine inaendelea kufanyiwa kazi na mingine ipo hatua mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, pia, Serikali imewekeza kwenye uendelezaji wa mabonde, kama mnavyojua nchi yetu huwa imegawanywa katika mabonde ambapo mengi kati ya hayo mabonde yameingia kwenye hatua za uendelezaji.

Mheshimiwa Spika, moja kubwa ambalo ni la muda mrefu na linaendana na dira ambayo Mheshimiwa Sara ameitaja, ni kwamba Serikali katika dira na katika ilani yake hii mpya, imeelekeza kwenye kuwekeza kwenye Gridi ya Maji ya Taifa ambapo tunayatoa maji kwenye vyanzo visivyokauka, mfano wa Ziwa Victoria, Tanganyika, Nyasa, mito mikubwa, kuipeleka kwenye Gridi ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, maelekezo ya Mheshimiwa Rais na maelekezo ya ilani ni kwamba sasa tunapounganisha maji kutoka kwenye vyanzo hivyo vya kudumu, tusipeleke tu maji hayo kwa ajili ya matumizi ya majumbani, bali kuwe na matoleo kwa ajili ya umwagiliaji, lakini pia na shughuli za ufugaji katika maeneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo hili ni jambo ambalo litaenda kutekeleza hili swali na maoni makubwa aliyoyaleta Mheshimiwa Mbunge. Kutakuwa na miradi mikubwa kila ukanda ambapo kuna chanzo cha kudumu cha maji.

Mheshimiwa Spika, tutapeleka kwenye miradi ya maji ya majumbani kwa matumizi ya kila siku, lakini pia kutakuwepo na matoleo ya maji kwa ajili ya umwagiliaji na matumizi ya mifugo kwa ajili ya shughuli hizo zinazoendelea katika maeneo husika ambapo miradi hiyo mikubwa inapita.

Additional Question(s) to Prime Minister