Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
| Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
|---|---|---|---|---|---|---|
| 2025-2030 | Session 3 | Sitting 43 | Other Sectors | Maswali kwa Waziri Mkuu | 4 | 2026-06-04 |
Name
Asha Salum Motto
Gender
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ASHA S. MOTTO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi ya kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, ninakupongeza sana kwa kazi kubwa unayoendelea kuifanya ya kutatua changamoto mbalimbali kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia, niipongeze sana Serikali kwa kuboresha miundombinu ya afya na uhakika wa dawa na vifaa tiba nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri Mkuu, hivi karibuni kumeibuka na taarifa za kuenea kwa ugonjwa wa ebola kwa baadhi ya nchi za jirani na kwa kuwa nchi yetu inamahusiano mazuri sana na nchi hizi za jirani, kwa maana ya kibiashara na mahusiano ya kijamii.
Mheshimiwa Spika, je, Serikali imejipangaje kudhibiti na kukabiliana na janga hili la ebola? Ahsante. (Makofi)
Name
Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Magharibi
Answer
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa nafasi hii na nijibu swali la Mheshimiwa Asha Motto, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kulileta swali hili kwa wakati, ni jambo ambalo linaendelea katika maeneo mbalimbali hapa Afrika.
Mheshimiwa Spika, kwanza nitumie Bunge lako Tukufu kusema mpaka sasa tupo salama, nchi yetu ipo salama, ni jambo la kumshukuru Mungu, tupo salama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, nchi yetu inamahusiano mema na siyo tu ya Kiserikali, ya watu na watu mipakani na pia Tanzania siyo kisiwa na jambo hili ni jambo la mlipuko inayotokea maeneo mbalimbali. Ni jambo linaloweza kutokea katika nchi yoyote.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutambua hilo tumeendelea kuchukua hatua za kutoa elimu na nitumie Bunge lako Tukufu, kuendelea kupaza sauti kwa Watanzania wote kuendelea kuchukua tahadhari kama ambavyo tumekuwa tukichukua tahadhari yanapotokea mambo ya magonjwa ya aina hii ambalo hili siyo la kwanza na hata hili hili la aina hii la ebola siyo la kwanza kutokea katika mataifa haya ambayo yameripotiwa kuwa na tatizo hilo.
Mheshimiwa Spika, tuendelee kuchukua hatua za tahadhari, tuendelee kuelimishana, lakini pia tuwe na utayari, mtu anapotoka nje ya nchi, anapotoka nje ya mipaka; awe mtanzania, awe mgeni tuwe na utayari wa kufanya vipimo na tuwe na utayari wa kutokuficha tetesi hizo, lakini pia na kutokuficha dalili hizo ili kuweza kupata huduma ya kwanza ambayo itasaidia kutokuruhusu ugonjwa kusambaa endapo kuna mgeni ama dalili zozote ama tetesi zitakazojitokeza katika eneo lolote lile. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa undani zaidi, Waziri wa Afya, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, pamoja na timu yake ya wataalam wanajipanga kuendelea kutoa elimu hii, lakini pia na kutoa taarifa kuhusu hali halisi ya jambo hilo ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mungu ni mwema bado tupo salama, tuendelee kumuomba Mungu, hajawahi kushindwa, tumewahi kuvuka mambo mengi magumu ya aina hii na hata hili tutavuka salama. Tuendelee kuzingatia yale ambayo wataalam wetu wa afya watatushauri, tuyazingatie na tuyafanyie kazi ili kuweza kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved