Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Question to Prime Minister

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2025-2030 Session 3 Sitting 43 Livestock , Fisheries, Agriculture, Food Security and Cooperatives Maswali kwa Waziri Mkuu 5 2026-06-04

Name

Dickson Nathan Lutevele

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Primary Question

MHE. DICKSON N. LUTEVELE: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi na mimi ya kuuliza swali kwa Serikali, lakini kabla sijauliza, ninaomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Waziri wetu Mkuu, kwa kazi kubwa anayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri Mkuu, kimsingi ziara unazozifanya siyo tu zinaweka ukaribu kati ya wananchi na Serikali yao, lakini zinaongeza mahaba sana kwa wananchi kwa Serikali yao, hasa pale yanapotatuliwa papo kwa papo matatizo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ninaomba nimuulize Mheshimiwa Waziri Mkuu, swali; sekta ya kilimo imekuwa na mchango mkubwa sana katika kuongeza pato la wakulima, lakini pia katika kuongeza pato la Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na utaratibu wa malipo baadaye hasa kwenye mazao ya kilimo cha biashara kama chai na hii imepelekea sana wananchi hawa baada ya kupeleka mazao yao viwandani wanacheleweshewa sana malipo na wakati mwingine hawalipwi kabisa. Nimetoa mfano kwenye zao la chai.
Mheshimiwa Spika, sasa nini mpango wa Serikali katika kuhakikisha kwamba wananchi hawa wanakuwa wanalipwa kwa wakati na hivyo kuendeleza mashamba yale ambayo mazao yanatoka na kuongeza pato lao? Ahsante sana. (Makofi)

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge wetu wa Mafinga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Lutevele, ameleta jambo ambalo linajitokeza siyo tu kwa zao la chai, linajitokeza pia kwa mazao mengine.

Mheshimiwa Spika, nimefanya vikao na wadau wakiwemo Waheshimiwa Wabunge na hata yeye mwenyewe Mheshimiwa Lutevele, pamoja na Wabunge wenzake wanaotokea ukanda wa chai, tumeshakaa vikao takribani viwili/vitatu tukiwa pia na Waziri wa Kilimo pamoja na wataalam wake.

Mheshimiwa Spika, tumekaa pia na Wabunge wanaotokea upande wa zao la tumbaku, tumekaa na Wabunge wanaotokea eneo la zao la pamba na mazao mengine; korosho na mazao mchanganyiko.

Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na tatizo hilo na hasa hasa katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na kupanda na kushuka kwa bei hizi na wakati mwingine ucheleweshaji wa malipo kwa sababu kule sokoni tunapotegemea maeneo mengi kumekuwa kukitokeza na kuharibika kwa mnyororo huu wa ugavi.

Mheshimiwa Spika, utakumbuka hapajatulia huko kwenye masoko yetu kwa mfululizo linatoka hili linaingia lingine. Imekuja UVIKO-19 kukawa na lockdown; kukishakuwa na lockdown mnyororo wa ugavi unaharibika kule duniani. Baada ya hapo kukatokea mzozo wa Ulaya ya Mashariki, baada ya hapo kukatokea tatizo lile lililokumba uhaba wa fedha za kigeni katika mataifa mengi na sasa ukatokea tena huu mzozo wa Mashariki ya Mbali/Mashariki ya Kati.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Serikali imeendelea kujitahidi kuhakikisha kwamba wakulima wanapata masoko, lakini pia wanapata bei zinazostahili katika masoko yake.

Mheshimiwa Spika, baadhi ya hatua ambazo Serikali imeendelea kuchukua ni kufanya mahusiano ya nchi na nchi zile ambazo tunashirikiana katika ununuzi wa mazao husika ili kuweza kuhakikisha kwamba kampuni zinayotoka katika nchi hizo ambazo zinanunua mazao yale ambayo wakulima wetu wanayalima ikiwemo chai, wanaendelea kupata faida kutokana na kilimo chao.

Mheshimiwa Spika, Serikali pia inachukua hatua kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, kuhamasisha upatikanaji ama kuanzishwa kwa viwanda vya kuchakata mazao haya ndani ya nchi yetu, kwa sababu mazao yenyewe kama chai yana muda mfupi sana kabla hayajaharibika yasipochakatwa. Hatua hiyo imeshachukuliwa kwa upande wa mazao ya Kaskazini, Mashariki kule Tanga, kuna kiwanda kinafungwa siku siyo nyingi kwa jitihada za Serikali ili kuweza kuhakikisha kwamba unapunguza uharibifu lakini pia unatengeneza uchakatajwi wa zao la chai katika eneo husika.

Mheshimiwa Spika, hivyo hivyo na kwa upande wa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, ikiwemo Mafinga hatua zinaendelea kuchukuliwa za kufufua viwanda vile; majadiliano yanaendelea na wawekezaji waliopo na wanunuzi wale ambao wamekuwa wakinunua ili kuweza kuhakikisha tunashughulikia tatizo hilo.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge pamoja na Wananchi wake wa Mafinga, Mungu akitupa uhai weekend hii tutakuwa kwake Mafinga kule na tutakuwa na timu nzima ya Serikali ikiwemo Wizara inayoshughulikia suala hilo. Tutaendelea kutoa mrejesho kwa wananchi wake ili kuweza kuhakikisha kwamba wananchi hao wanapata faida kutokana na nguvu kubwa wanayoweka kwenye zao hilo, ambalo ni zao lao la msingi la kuwaletea maendeleo.

Additional Question(s) to Prime Minister