Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2025-2030 Session 3 Sitting 27 Natural Resources and Tourism Wizara ya Maliasili na Utalii 319 2026-05-12

Name

Edibily Kinyoma Kazala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Vijijini

Primary Question

MHE. EDIBILY K. KINYOMA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza mgogoro wa ardhi kati ya TFS na TAWA dhidi ya wananchi wa Jimbo la Kasulu Vijijini?

Name

Hamad Hassan Chande

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kojani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Edibily Kazala Kinyoma, Mbunge wa Kasulu Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Kasulu Vijijini kuna Kitalu cha Uwindaji cha Makere - Uvinza ambacho kimetengwa na kusimamiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu. Baada ya kutengwa kwa kitalu hicho ulijitokeza migogoro kwa baadhi ya wananchi kuanzisha shughuli za kibinadamu kama vile makazi na kilimo ndani ya eneo la kitalu ikiwemo Kitongoji cha Katoto kilichoanzishwa ndani ya kitalu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Kamati ya Mawaziri nane wa kisekta ilitoa maelekezo kuwa kitongoji hicho kihamishwe baada ya kubaini kuwa kimeanzishwa nje ya mipaka ya Kijiji mama cha Kagerankanda. Serikali ya Mkoa wa Kigoma ilitekeleza maelekezo hayo na kusimamia zoezi la kuwahamisha wananchi hao kwenda kwenye Kijiji cha Kagerankanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia mwezi Oktoba, 2025 uongozi wa Mkoa wa Kigoma kwa kushirikiana na uongozi wa Wilaya ya Kasulu ulifanikiwa kuhamisha wananchi wote kutoka Kitongoji cha Katoto na kwenda Kitongoji cha Nyantuku katika Kijiji cha Kagerankanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muktadha huo, endapo kuna changamoto nyingine zinazotokana na mwingiliano wa matumizi ya ardhi kati ya wananchi na kitalu hicho, Wizara ipo tayari kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge na Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kutafuta ufumbuzi na kuondoa changamoto hizo. Ahsante sana.