Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
											Name
Ester Amos Bulaya
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ESTER A. BULAYA K.n.y. MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha majengo ya Mradi wa Dege Beach-NSSF Mbweni kwa kuwa ni wa muda mrefu?
Supplementary Question 1
MHE. ESTHER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru. Kwanza ninatoa pongezi kwa Dar Young Africans kwa kuchukua ubingwa bila kipengele chochote na hiyo ndiyo Yanga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya hapo ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. 
Swali la kwanza; kumekuwa na malalamiko ya wastaafu fedha zao kutumika kwenye uwekezaji bila kushirikishwa: -
(a)	Je, Serikali ina kauli gani katika hili?
(b)	Je, kuna miradi mingine aina ya Dege Beach ambayo imeiletea Serikali hasara ambayo mmeifanyia tathmini na hatua gani ambayo mmechukua kwa walioruhusu uwekezaji kama huu?
 
											Name
Paschal Katambi Patrobas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Shinyanga Mjini
Answer
								NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, ahsante na ninaomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Ester Bulaya kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, la kwanza, kuhusu malalamiko ya wastaafu kuhusiana na fedha zao kuwekezwa hilo hatujalipata rasmi kama ofisi. Kimsingi sababu za uwekezaji zinazofanywa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, tunafanya baada ya kufanya tathmini na kushauriwa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT). Kuna mwongozo maalum kuhusiana na maeneo ya uwekezaji na namna ya kuwekeza. Tafiti zinafanyika na wanashauri baada ya kuwa mmefanya utafiti huo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo lengo la kuwekeza ni kwa ajili ya kulinda thamani ya fedha ya mfuko, kwa sababu kuna wakati mwingine inatokea price fluctuation au mfumuko wa bei au kushuka kwa shilingi au thamani ya fedha. Sasa fedha hizi zitakapokuwa zimewekwa tu kama kwenye kibubu halafu baadaye fedha ikashuka thamani maana yake unapeleka athari kwa mwanachama mwenyewe kushindwa kuja kupata fedha au mafao mazuri zaidi. 
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo zinawekezwa ili ziweze kulinda ile thamani ya fedha yenyewe, lakini pia kutengeneza stability ya mfuko. Kila wakati tunafanya actuarial valuation kwa mujibu wa sheria na mwongozo. Kwa hiyo, pia hata hivyo katika hatua hiyo tunaangalia mambo mawili, cost benefit analysis na pia tunafanya profit and loss analysis, ili kujiridhisha kwamba patakapowekezwa basi kuwe kuna tija na faida kwa mfuko, lakini zaidi kwa wanachama wenyewe.
Mheshimiwa Spika, kwa swali la pili linafanana na la kwanza na swali la pili linasema kwa nini tunaweka miradi ambayo inakuwa na hasara. 
Mheshimiwa Spika, miradi yote hii ambayo inafanywa inafanyiwa tafiti na mwongozo wa BOT unaelekeza kwamba kabla ya mradi kuwekezwa kwanza ufanyiwe tafiti, kuwe na andiko la mradi na kisha kwenda BOT kufanyiwa mapitio na hatimaye kupitishwa. 
Mheshimiwa Spika, sasa kinachojitokeza kwa mfano wa Mradi wa Dege anaueleza Mheshimiwa Mbunge kwenye swali, ni kwamba wakati wa uwekezaji, wakati ule, mazingira yaliruhusu na kulikuwa kuna tija na haja ya mradi huo kuwekwa kwa wakati ule, lakini kadri muda ulivyokwenda mambo yalibadilika. Kwa mfano uamuzi wa kuihamisha Serikali kwa kuitoa Dar es Salaam kuja Jijini Dodoma kuliathiri maeneo mengi ambayo ukiacha tu hata kwenye Mradi wa Dege, lakini pia hata miradi kwenye private investment na maeneo mengine yalikuwa na athari. 
Mheshimiwa Spika, vivyo hivyo kuna mambo ya kimkataba na muda ambayo kimsingi yote haya huwa ni mazingatio ya msingi kuweza kuhakikisha na ndiyo maana hatua nzuri ya Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ilikuwa ni kufanya utafiti na assessment kwenye miradi yote…
SPIKA: Haya ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (MHE. PASCAL P. KATAMBI): … kuangalia yenye hasara ili kurudisha faida, kwa maana ya kuweka utaratibu hata huu wa kuuza ili kuweza kulinda ile thamani ya fedha na kuboresha mafao ya wafanyakazi kama jinsi alivyofanya Mheshimiwa Rais kwa sasa. 
							
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved