Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
											Name
Condester Michael Sichalwe
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Momba
Primary Question
MHE. CONDESTER M. SICHALWE K.n.y. MHE. JACKSON G. KISWAGA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga bweni la wasichana na wavulana katika Shule ya Sekondari ya Kimaiga, Kata ya Kihanga?
Supplementary Question 1
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali kwa Jimbo la Mheshimiwa Jackson Kiswaga. Nina maswali mawili ya nyongeza ninayaelekeza kwenye Jimbo la Momba.
Mheshimiwa Spika, kwenye Jimbo la Momba tuna sekondari 16 na sekondari zote hizi kuna changamoto ya mabweni. Je, ni upi mkakati wa Serikali kuanza kutusaidia kutujengea mabweni angalau kwa kuanzia kwa shule tano kisha kuendelea na shule zingine?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa watoto wengi wanatembea mwendo mrefu na watoto wa kike wengi huahirisha masomo katika Jimbo la Momba kutokana kushindwa kuwatunza kwenye mabweni kwa sababu hakuna mabweni kabisa. 
Je, ni upi mkakati wa Serikali wa haraka na wa dharura angalau kuzisaidia shule kongwe kama Msangano, Chikanamlilo, Kapele, Momba, Uwanda na Ivuna ili zile ambazo zimechukua watoto wengi waweze kusaidika wasiendelee kutoroka kwenye shule? (Makofi)
 
											Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
								NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali inafanya uwekezaji mkubwa sana katika sekta yetu hii ya elimu msingi na sekondari na ni dhahiri kutokana na utekelezaji wa Sera ya Elimu bila Malipo udahili wa wanafunzi umeongezeka maradufu na mazingira ya uhitaji miundombinu ya madarasa na shule zetu hizi umeongezeka; na ndio maana katika majibu ya msingi nimeeleza kwamba kipaumbele cha Serikali kwa wakati huu ni ujenzi wa shule mpya za kutwa pia ni ujenzi wa miundombinu itakayowezesha baadhi ya shule zetu hizi za kutwa ziweze kupokea wanafunzi wa kidato cha tano na sita.
Mheshimiwa Spika, sasa Mheshimiwa Condester Sichalwe katika Jimbo lake la Momba anasema kwamba ana shule za sekondari 16 na kwamba anahitaji shule angalau tano zijengewe mabweni ili ziweze kuwa ni shule za bweni. Sasa mpango wa Serikali kwa sasa shule zenye kuanzia kidato cha kwanza mpaka kidato cha nne ni shule za kutwa ni shule za kata, kwa hiyo ndiyo maana hazijengewi miundombinu ya mabweni. 
Mheshimiwa Spika, kwenye uhitaji kwa kukubaliana na wazazi pamoja na walimu wanakaa pamoja wanajadili na wanaweza kushirikisha wadau kwa ajili ya kujenga hosteli, lakini kipaumbele cha Serikali kwa wakati huu ni kuhakikisha shule za kata nyingi zinajengwa ili ziweze kupokea wanafunzi wengi zaidi ambao wamejitokeza. 
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili kwamba anahitaji mabweni kwenye shule hizi ili ziweze kuwasaidia wanafunzi wasichana wasikatize masomo yao kutokana na changamoto mbalimbali; jibu ni lilelile kwamba Serikali inaweka kipaumbele zaidi kujenga miundombinu ya shule ili shule hizi za kata za kutwa ziweze kupokea wanafunzi wengi ambao wamejitokeza, wanataka kupata elimu. Kwa mipango ambayo inakubalika Serikali, shule pamoja na wazazi wanaweza wakakaa wakakubaliana ili waweze kushirikisha wadau kujenga hosteli. 
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea…
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): ... kufanya uwekezaji mkubwa wa kuhakikisha kwamba wanafunzi wetu wanapata miundombinu ya kusomea.
							
 
											Name
Esther Nicholus Matiko
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. CONDESTER M. SICHALWE K.n.y. MHE. JACKSON G. KISWAGA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga bweni la wasichana na wavulana katika Shule ya Sekondari ya Kimaiga, Kata ya Kihanga?
Supplementary Question 2
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Mji wa Tarime waliomba fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa bweni na bwalo kwenye Shule ya Msingi Magufuli ambayo ni maalum kwa watoto wenye uhitaji maalum. Je, lini Serikali italeta fedha hizi ili tuweze kujenga bweni hilo?
 
											Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikiendelea kuimarisha miundombinu katika sekta hii muhimu ya elimu ya msingi na sekondari na imekuwa ikifanya uwekezaji maalum kabisa katika shule za watoto wenye mahitaji maalum. Kwa hiyo, ninaomba nikuhakikishie Mheshimiwa Esther Matiko kwamba Serikali itaendelea kutenga fedha kwa awamu kupitia mapato ya ndani ya halmashauri, lakini kupitia Serikali Kuu kwa ajili ya kuhakikisha na kuja kujenga bweni na bwalo katika shule hii ya wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Jimbo la Tarime.
 
											Name
Kasalali Emmanuel Mageni
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sumve
Primary Question
MHE. CONDESTER M. SICHALWE K.n.y. MHE. JACKSON G. KISWAGA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga bweni la wasichana na wavulana katika Shule ya Sekondari ya Kimaiga, Kata ya Kihanga?
Supplementary Question 3
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, ninashukuru, Shule ya Sekondari ya Mantare katika Jimbo la Sumve ina jiografia ambayo imezungukwa na milima hivyo kusababisha ugumu wa watoto kuwahi shuleni kwa muda muafaka na kusababisha utoro. Je, Serikali haioni kuna umuhimu wa kujenga bweni katika shule hii ili kurahisisha usomaji na ujifunzaji wa watoto hawa?
 
											Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
								NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kipaumbele cha Serikali kwa wakati huu ni kuhakikisha Serikali inaendelea kujenga shule mpya za kutwa ili ziweze kupokea wanafunzi wengi ambao wamejitokeza kwa ajili ya kupata elimu. Shule nyingi hizi za kata ni shule za kutwa, lakini kwa mpango maalum wazazi wakishirikiana na uongozi wa shule wanakaa na kushirikisha wadau na kuamua kujenga hosteli. Serikali inapeleka fedha katika baadhi ya shule hizi za kata ili ziweze kujengewa miundombinu ikiwemo mabweni kwa ajili sasa ya kuanza kupokea wanafunzi wa kidato cha tano na sita.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaomba nitumie nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Kasalali katika Jimbo lake hili la Sumve kuwa Serikali kupitia mapato ya ndani pia kupitia utaratibu huu unaofanywa, fedha kutoka Serikali Kuu itaweka kipaumbele katika shule hii uliyoomba ijengewe miundombinu hii ili iweze kuwa na mabweni, hatimaye iweze kupokea wanafunzi pia wa kidato cha tano na sita.
							
 
											Name
Samweli Xaday Hhayuma
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hanang'
Primary Question
MHE. CONDESTER M. SICHALWE K.n.y. MHE. JACKSON G. KISWAGA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga bweni la wasichana na wavulana katika Shule ya Sekondari ya Kimaiga, Kata ya Kihanga?
Supplementary Question 4
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Spika, ni lini fedha zitapelekwa Shule ya Bassodesh ambayo ni shule maalum kwa ajili ya watoto wa wafugaji na miundombinu yake imechakaa sana?
 
											Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
								NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikiendelea kuimarisha miundombinu katika sekta hii muhimu kabisa ya elimu msingi na sekondari na Serikali imekuwa ikitumia fedha za mapato ya ndani ikiwemo pia fedha za Serikali Kuu kwa ajili ya kuendelea kuimarisha miundombinu ya shule zetu. 
Mheshimiwa Spika, katika shule hii ya Bassodesh ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Hhayuma kwamba Serikali kupitia mapato ya ndani itafika katika shule hii kwa ajili ya kuhakikisha kwamba inaikarabati iwe ina miundombinu mizuri ili iweze kuwanufaisha wanafunzi katika jimbo lako.