Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
 
											Name
Tarimba Gulam Abbas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kinondoni
Primary Question
MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza:- Je, Serikali haioni haja ya kutafuta fedha kama mikopo kuliko kutegemea Bajeti ya Serikali katika kuweka lami, taa na mifereji barabara za ndani Dar es Salaam?
Supplementary Question 1
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, ahsante, nimesikia majibu ya Serikali ni kwamba pale Dar es Salaam barabara muhimu ambazo zilifanyiwa utafiti kwamba zijengwe ni kilometa 759 na kilometa ambazo Mheshimiwa Naibu Waziri anazizungumza ni kama ni kama 30% tu na kwangu kwenye jimbo langu tutapata kilometa nne tu katika zote hizo anazozizungumzia. 
Mheshimiwa Spika, swali langu, nini mipango ya Serikali kutafuta fedha nje ya Mradi wa DMDP II na fedha za bajeti ili kuweza kumaliza ujenzi wa barabara za ndani pale Dar es Salaam?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, wewe ni shahidi kwamba pamoja na kwamba Serikali inajitahidi sana kujenga barabara, suala la ukarabati limekuwa ni sugu, mashimo ni mengi kila mahali na hata wakandarasi waotumika hawafanyi kazi vizuri. 
Je, Serikali iko tayari kufanya utafiti ili sasa kubaini jukumu la utengenezaji na ukarabati wa barabara lipelekwe kwa halmashauri za miji yetu ili barabara zetu ziweze kuwa salama wakati wote?  (Makofi)
 
											Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
								NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Serikali ya Awamu ya Sita imefanya jitihada za makusudi kabisa kupata mradi mahususi ambao utaendeleza miundombinu ya barabara katika Mkoa wa Dar es Salaam. Mradi huu wa DMDP II ni mradi ambao una gharama za jumla ya dola za Kimarekani 438 ikiwa ina lengo la kujenga kilometa 250 za barabara za lami, lakini mifereji ya maji ya mvua kilometa 90, vituo vya mabasi tisa, masoko 18 na ujenzi wa madampo matatu. 
Mheshimiwa Spika, sasa pamoja na hoja ya Mheshimiwa Abbas Tarimba ninaomba nimfahamishe kwamba kupitia bajeti ya TARURA ambayo inaendelea kuimarika katika kila mwaka wa bajeti ukitazama tu katika kipindi cha miaka minne ya Awamu ya Sita zaidi ya shilingi bilioni 32.2 zimetumika katika Wilaya ya Kinondoni kwa ajili ya kuendelea kuimarisha miundombinu ya barabara zetu hizi.
Mheshimiwa Spika, mpango uliowekwa na Serikali ni kwamba kila wilaya katika nchi hii kwa maana ya Tanzania Bara kila mwaka wa fedha angalau ijengewe kilometa moja ya lami. Haitoshi hivyo, pia kupitia mapato ya ndani ya halmashauri Serikali imekuwa ikitenga fedha mahsusi kabisa kwa ajili ya kwenda kuimarisha miundombinu ya barabara zetu hizi za wilaya. Mathalani, nitoe pongezi kwa halmashauri hii ya Manispaa ya Kinondoni ambayo kupitia mapato ya ndani imeweza kununua mitambo ya kuchongea barabara. Pongezi kubwa sana kwako Mheshimiwa Mbunge, lakini pongezi kwa Manispaa ya Kinondoni kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Spika, unatazama katika mwaka wa bajeti 2024/2025 ambayo Manispaa ya Kinondoni ina jumla ya mapato ya ndani shilingi bilioni 74; shilingi bilioni 5.6 zimeenda katika ujenzi wa kilometa 5.6 za barabara za lami ambazo tayari zimeshaanza kutekelezwa na zinakaribia kukamilika. Kuna kilometa 2.5 za lami ambazo bado zinaendelea kujengwa na zikikamilika jumla unaona hapo ni zaidi ya kilometa 7.5 ya lami zinakuwa zimejengwa kutokana na mapato ya ndani. Kwa hiyo, Serikali itaendelea na mikakati hii ya kuhakikisha kwamba kupitia miradi mahususi kama hii ya DMDP, bajeti ya TARURA, lakini mapato ya ndani inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya barabara hizi muhimu za wilaya.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusiana na kutenga fedha…
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri fupisha majibu ya swali la pili tafadhali.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali la pili la ukarabati wa barabara, Serikali inatenga fedha kila mwaka wa bajeti kupitia bajeti ile ya TARURA kuhakikisha inakarabati barabara zetu hizi, lakini kuna maelekezo mahsusi kabisa na hasa kwenye Halmashauri za Manispaa na Majiji kutenga fedha kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya kuhakikisha inakarabati barabara hizi za wilaya. 
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba niendelee kusisitiza maelekezo haya kuwa Wakurugenzi waweze kutenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha na wenyewe kwenye mapato ya ndani wanakarabati barabara zetu hizi za wilaya. (Makofi)
							
 
											Name
Dorothy George Kilave
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Temeke
Primary Question
MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza:- Je, Serikali haioni haja ya kutafuta fedha kama mikopo kuliko kutegemea Bajeti ya Serikali katika kuweka lami, taa na mifereji barabara za ndani Dar es Salaam?
Supplementary Question 2
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante, je, kuna mkakati gani kati ya TARURA na TANROADS kuhakikisha wanashirikiana kufanya hizi barabara za ndani ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam hasa Jimbo la Temeke?
 
											Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
								NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikifanya jukumu la pamoja la kushirikiana kwa maana ya Serikali nzima kama alivyoainisha Mheshimiwa Mbunge kwamba ushirikiano kati ya TARURA na TANROADS, Serikali imekuwa ikifanya hivyo ikishirikiana kuhakikisha kwamba inaendelea kuimarisha miundombinu ya barabara zetu hizi za wilaya, lakini pia barabara zetu hizi zenye hadhi ya kimkoa. Kwa maana TANROADS inahudumia mtandao wa barabara zenye hadhi mkoa na TARURA inahudumia barabara zenye hadhi ya wilaya.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuhakikisha inaimarisha ushirikiano ili kwa pamoja kama Serikali kujenga barabara hizi na kuhakikisha miundombinu ya barabara inakuwa imara, wananchi wetu waweze kufanya shughuli zao za kiuchumi, lakini pia waweze kufikia huduma za msingi kabisa za kijamii.
							
 
											Name
Abubakar Damian Asenga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilombero
Primary Question
MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza:- Je, Serikali haioni haja ya kutafuta fedha kama mikopo kuliko kutegemea Bajeti ya Serikali katika kuweka lami, taa na mifereji barabara za ndani Dar es Salaam?
Supplementary Question 3
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, je, ni lini taa za barabarani zitafungwa katika Barabara ya Mwaya na ya Kidatu? Naishukuru Serikali kwa taa za Kibaoni Stendi.
 
											Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
								NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali ina mkakati maalum kabisa wa kuhakikisha katika barabara zinazojengwa hizi za lami zinajengwa pamoja na mifereji ya kutoa maji ya mvua, lakini pia zinajengwa na taa juu na Serikali imeanza kufanya hivyo katika ujenzi wa barabara zake kwa wakati huu na Serikali itaendelea na jitihada za kufikia barabara zetu hizi na kuhakikisha kwamba zinawekewa taa juu. 
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Abubakari Asenga kwamba kwenye barabara alizozitaja za Mwaya za Kidatu, Serikali itafika kwa ajili ya kuhakikisha inaweka taa ili kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara zetu hizi muhimu kabisa.