Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Grace Elias Mkoma
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. GRACE E. MKOMA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga uwanja mkubwa wa ndege Singida?
Supplementary Question 1
MHE. GRACE E. MKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Je, ni lini mchakato rasmi utakamilika ili uwanja wa ndege wa Mkoa wa Singida uweze kujengwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, nini mkakati wa Serikali kufungua anga ili sasa ndege yetu ya Air Tanzania ili iweze kusafiri mfano katika nchi za Morocco, Uturuki na Vietnam kwa sababu nchi hizo zina fursa za kiuchumi? (Makofi)
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Uchuzi napenda kujibu maswali ya nyongeza mawili ya Mheshimiwa Grace Elias Mkoma, Mbunge wa Viti Maalum kama ambavyo ameulizia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza nampongeza Mheshimiwa Grace Mkoma kwa kutambua umuhimu wa Uwanja wa Ndege wa Mkoa wa Singida na kuendelea kuwa sauti makini ya wanawake na viongozi na wananchi na hii ni kutokana na ukweli kwamba Mheshimiwa Grace anatambua kwamba Mkoa wa Singida kwanza uwanja wake ni mbadala na ni sehemu ya jirani kutoka Dar es Salaam, lakini pia kuna fursa za madini, kilimo, ufungaji pamoja na mambo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Grace Mkoma na wananchi wote wa Mkoa wa Singida kwamba Serikali kwa kutambua umuhimu wa uwanja huu wa Singida imekwishaanza kwanza kwa kutambua eneo kama nilivyosema na hatua inayofuatia sasa ni kukamilisha taratibu za utwaaji wa ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na hivi navyozungumza katika bajeti iliyosomwa hapa Bungeni mwezi huu wa tano na Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Mbarawa Makame Mnyaa amewahakikishia Wana-Singida katika mwaka wa fedha 2026/2027 tunakwenda kuanza taratibu mbalimbali kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi huo. Nimuombe Mheshimiwa Grace awe na uvumilivu wakati Serikali inafanyia kazi jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; pia nampongeza kwa kuendelea kupigania ndege yetu Shirika letu la Air Tanzania ambalo ndiyo shirika kubwa kwa nchi yetu na la Serikali ameuliza ni mkakati gani uliowekwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza kabisa mkakati wa kwanza ni kuingiza kwenye Ilani ya CCM, Serikali ya CCM kupitia aliyekuwa mgombea ambaye ndiye Rais wa nchi, aliwaambia Watanzania anakwenda kuongeza ndege zilizokuwepo na zitakazokuwepo ili ziweze kuwa nyingi zaidi; zaidi ya ndege nane katika kipindi cha miaka mitano hii ijayo hii ni kuongeza uwezo wetu wa kutoa huduma, lakini pia ili kuhakikisha kwamba jambo hili linakwenda kutekelezeka mwaka wa fedha wa 2026/2027 Serikali imejipangia kwenda kuongeza mtandao huo kutoka safari za ndani na nje na za kimataifa 33 zilizopo mpaka kufika 47.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ambapo ukiangalia hadhi iliyokuwepo miaka kumi iliyopita na sasa unaona kabisa vituo vingi vinaongezeka na hapa Bungeni mmesikia matamko ya Wizara jinsi ambavyo tunaongeza ndani ya nchi, tunakwenda Geita tunaunganisha Mwanza na Dodoma na maeneo mengine, pamoja na maeneo mengine ya nje ya nchi ikiwemo visiwa Sychelles na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inayo mpango wa kwenda mahali pengi zaidi ili kuhakikisha kwamba tunanufaika na fursa ambazo ziko kwenye nchi yetu, lakini mwisho tutaendelea kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha kwamba shirika letu linakwenda kuongeza mtandao zaidi ndani na nje ya nchi yetu.
Name
Esther Nicholas Matiko
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Tarime Mjini
Primary Question
MHE. GRACE E. MKOMA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga uwanja mkubwa wa ndege Singida?
Supplementary Question 2
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, ukizingatia Wilaya ya Tarime ina nafasi kubwa kama lango muhimu la shughuli za madini, biashara za mpakani lakini zaidi za utalii wa kaskazini mwa Tanzania.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuendeleza airstrips ya Magena kuwa kituo cha kisasa cha usafiri wa anga kwa kuweza kuboresha njia ya kurukia ndege, kujenga jengo la abiria na huduma nyingine muhimu ili kuongeza ushindani wa kiuchumi na kuvutia wawekezaji wengi katika eneo hili ambapo wataongeza mapato na kuongeza ajira katika Mji wa Tarime na Tanzania kwa ujumla?
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi nipende kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Matiko ambaye ametaka kufahamu airstrips ya Magena.
Kwanza ni mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba inaboresha viwanja vya ndege mbalimbali takribani 235 vinavyomilikiwa na taasisi za umma sambamba na kuhamasisha ambavyo vinamilikiwa na taasisi binafsi na katika hivyo vikiwemo 61 vinavyomilikiwa na TAA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Mbunge tupokee ushauri wa airstrips aliyoisema kwa sababu katika mkoa wake pale Serikali inakwenda kujenga uwanja wa ndege mkubwa wa Serengeti katika mkoa huo huo, Musoma Mjini tunajenga uwanja wa ndege wa Musoma. Kwa hiyo, inawezekana tusifike haraka kwenye hiyo airstrip aliyoisema, lakini awe na subira tutaipokea na kulichakata na kulingana na upatikanaji wa fedha na taratibu Serikalini tutakwenda kufanyia kazi katika muda mwafaka.
Name
Rashid Mohamed Mtima
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Newala Mjni
Primary Question
MHE. GRACE E. MKOMA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga uwanja mkubwa wa ndege Singida?
Supplementary Question 3
MHE. RASHID M. MTIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.
Ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kujenga uwanja wa ndege eneo la Luchingu, Newala Mjini baada ya kuruhusu kiwanja cha zamani pale Nangwala kupima viwanja? (Makofi)
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inayo dhamira ya kuujenga uwanja husika mara tutakapokamilisha taratibu za utwaaji wa ardhi kwa maana ya vifaa vya fidia basi tutakwenda kuanza mchakato huo wa ujenzi wa uwanja ili wananchi waweze kunufaika na fursa zilizopo. (Makofi)
Name
Neema William Mgaya
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. GRACE E. MKOMA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga uwanja mkubwa wa ndege Singida?
Supplementary Question 4
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, takribani miaka kumi na tano sasa ndani ya Bunge hili nimekuwa nikiuliza lini Serikali itajenga Uwanja wa Ndege wa Njombe?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini? Kwanza Mkoa wa Njombe ndiyo mkoa ambao unalima parachichi kwa wingi na kila siku tunasisitiza, tuna hamasisha wawekezaji waje kuwekeza ndani ya mkoa wetu. Je, tunawezaje tukahamasisha wawekezaji waje kuwekeza ndani ya mkoa wetu ili hali hatuna uwanja wa ndege wa Njombe je, Serikali lini mtajenga uwanja huu wa Njombe? (Makofi)
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema Mgaya kuhusiana na Uwanja wa Ndege wa Njombe, nimhakikishie Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Mbarawa amenituma niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba uwanja wa ndege ni uwanja muhimu na mara kadhaa hapa Bungeni limekuwa likiulizwa swali hilo sambamba na Uwanja wa Ndege wa Tiabajwa, Serengeti na wa Mwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2026/2027 zimetengwa fedha kwa ajili maendelezo mbalimbali. Kwa sasa tupo kwenye hatua ya kutwaa ardhi tutakapokamilisha tutakwenda kwenye hatua ya pili kwa ajili ya kuanza kuujenga uwanja huo ambao ni muhimu siyo tu kwa ajili ya kilimo cha parachichi na kusafirisha mazao ya mboga mboga, lakini ninyi mnafahamu Njombe ni center, Njombe tuna mradi mkubwa sana wa Liganga na Mchuchuma ambao tunategemea kwamba wananchi pamoja na wawekezaji mbalimbali wanahitaji kuutumia.
Name
Josephine Joseph Kapoma
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. GRACE E. MKOMA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga uwanja mkubwa wa ndege Singida?
Supplementary Question 5
MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kati ya vipaumbele vikubwa vya kuongeza uchumi Mkoa wa Morogoro ikiwa kimoja wapo ni kuongeza idadi ya watalii wa ndani kutoka watalii 60,000 mpaka 300,000 na wa nje kutoka 400,000 mpaka 750,000 na Serikali ilishatuahidi kutujengea kiwanja cha ndege kwenye Hifadhi ya Mbuga ya Mikumi; je, ni lini Serikali itaanza kutekeleza suala hili? Ahsante. (Makofi)
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Josephine kwa swali lake ambalo kimsingi ameliuliza. Ni kweli Serikali inayo dhamira ya dhati ya kuendeleza sekta ya utalii na uwanja wa ndege pale Mikumi ni moja ya vipaumbele vyetu kwenye ilani yetu. Nimhakikishie kwa kuwa ndiyo tunaanza utekelezaji wa ilani hiyo, aipe muda Serikali iendelee na mchakato wa ndani, tutakapokuwa tayari basi tutakwenda kuanza taratibu za kuujenga uwanja huo.
Name
Zainab Rashid Kawawa
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. GRACE E. MKOMA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga uwanja mkubwa wa ndege Singida?
Supplementary Question 6
MHE. ZAINAB R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona. Ukisoma ile investment guide inaonesha namna gani Mkoa wetu wa Lindi ni mkoa wa kimkakati hasa kiuchumi, lakini pia una historia nzuri ya kutafuta kupambania uhuru wa nchi mbalimbali za Kiafrika, ina vivutio vya bahari, ina ardhi nzuri ya uwekezaji, inavutia kwenye kilimo pamoja na vivutio vya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafahamu kwamba Sera ya Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kujenga viwanja vikubwa katika kila mkoa wa nchi yetu ya Tanzania.
Sasa je, kwa vivutio hivi ambavyo vipo katika mkoa wetu wa Lindi; ni lini Serikali itajenga kiwanja kikubwa cha ndege katika Mkoa wa Lindi? Ahsante. (Makofi)
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi napenda kumjibu Mheshimiwa Zainab Kawawa ambaye anataka kufahamu ni lini Uwanja wa Ndege wa Lindi utajengwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakubaliana naye na kumpongeza Uwanja wa Ndege wa Lindi ni uwanja umuhimu kiuchumi kama alivyosema kutokana na uzalishaji wa mazao ya kibiashara kama vile korosho, mazao ya chakula na kadhalika, lakini pia pale Lindi Serikali inayo ajenda ya Mradi wa LNG. Hivyo uwanja huu ni muhimu sana acha utalii pamoja na mambo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua hilo Serikali hii ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imeamua kuujenga uwanja huu na hatua zifuatazo zimekamilika; kwanza kukamilisha usanifu, lakini pili tulikwishatangaza na kumpata mkandarasi lengo ni kujenga uwanja mkubwa wenye hadhi na wa kisasa utakaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 120 na kwa sasa tunachokizungumza ni kutafuta fedha za malipo ya awali ili mkandarasi alipwe na aanze kujenga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Mbunge awe na subira kipindi ambacho michakato ya ndani inakamilika na hatimaye tuweze kuanza ujenzi wa uwanja huu.