Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
John Stephano Luhende
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukene
Primary Question
MHE. JOHN S. LUHENDE aliuliza:- Je, lini Kampuni ya Yapi Merkezi wanaojenga Mradi wa SGR Bukene italipa fidia ya shilingi 2,666,666,666.64 inazodaiwa na Halmashauri ya Nzega?
Supplementary Question 1
MHE. JOHN S. LUHENDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza ahsante sana kwa Serikali kwa kulishughulikia suala hili naona kwa sasa tumeanza kupokea fedha zinazotokana na madini ujenzi ndani ya halmashauri yetu. Maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza kumekuwa na changamoto nyingi kwa wakandarasi kutolipa fedha hizi kwa wakati. Kwa nini Serikali isiweke utaratibu wa kuwa inazikata fedha zile moja kwa moja kabla ya kumlipa mkandarasi na kuzielekeza kwenye halmashauri husika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kumekuwa na changamoto ya wakandarasi kuja na wafanyakazi wao hasa wafanyakazi wa kawaida kama wale wanaotumika katika kufyeka, kukata miti na kazi nyingine za ujenzi ndogo ndogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Serikali msiweke msisitizo wa kuhakikisha kwamba wanapokuwa wanatekeleza miradi kwenye vijiji husika watumike wananchi wa vijiji hivyo ili tuweze kutengeneza ajira pamoja na kuinua uchumi wa eneo hilo? Ahsante. (Makofi)
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, napenda kumjibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa John Luhende kama ambavyo ameuliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ametoa kama ushauri kuhusiana na kwa nini tusione umuhimu wa kukata moja kwa moja? Na kabla sikujibu swali lake kwa niaba ya Serikali nipokee pongezi zake ambazo amezitoa kwa hii Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan jinsi inavyosimamia na kuratibu kwa umakini mkubwa mradi mkubwa kwenye nchi yetu wa standard gauge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nimrejeshee pongezi yeye mwenyewe kwa kuthibitisha umakini na ujasiri wa kufuatilia na kusimamia maslahi ya Watanzania, lakini hasa wa jimboni kwake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakubaliana na ushauri wake na Serikalini tumekwishaanza kufanyia kazi ili ikiwezekana wale wakandarasi ambao watakuwa na changamoto pengine za kulipa malipo hayo kwa wahusika au kwa vibarua tuone namna bora ya kulifanyia kazi jambo hilo bila kuathiri sheria, kanuni na taratibu za nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitumie nafasi hii kutoa rai kwa wakandarasi wote waliopo kwenye sekta yetu Mheshimiwa Waziri anatoa maelekezo kwamba ni vyema wakazingatia mikataba wanayoingia na Watanzania ili Watanzania wanaopata fursa ya kufanya kazi kwenye maeneo hayo basi waweze kulipwa stahiki zao kwenye nchi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Mheshimiwa Mbunge anatoa msisitizo kwamba ni vyema vipaumbele vitolewe kwa wananchi waliopo kwenye eneo hilo kabla ya kwenda maeneo mengine; hapa kwanza nikubaliane naye kipaumbele siyo upendeleo ni jambo la muhimu kwamba kama mradi unatekelezwa katika eneo hilo basi ukiwa na vijana wenye sifa kwenye eneo hilo wapewe kipaumbele zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili haimanishi kwamba kukiwa na mradi sehemu “A” basi wananchi wa maeneo mengine wasipate fursa hiyo hiyo kwa sababu tukifanya hivyo sasa nchi yetu tutaiingiza mahali pabaya zaidi. Maana yake kule kusipo na migodi basi Watanzania wasiajiriwe waajiriwe wa hapo hapo, kule kusipo na bandari, kule kusipo na uwanja wa ndege na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunachokisema tutatoa fursa kwa Watanzania wote, lakini ikiwezekana wa eneo hili hususan kwa kazi kama za vibarua waweze kutazamwa zaidi ili waone na wao wananufaikaje katika eneo lao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Name
Paschal Inyasi Chinyele
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Dodoma mjini
Primary Question
MHE. JOHN S. LUHENDE aliuliza:- Je, lini Kampuni ya Yapi Merkezi wanaojenga Mradi wa SGR Bukene italipa fidia ya shilingi 2,666,666,666.64 inazodaiwa na Halmashauri ya Nzega?
Supplementary Question 2
MHE. PASCHAL I. CHINYELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, wakazi wa Kata za Kikuyu Kusini, Mkonze pamoja na Zuzu ni miongoni mwa Watanzania waliopata bahati ya kupitiwa na reli ya SGR. Hata hivyo, iko changamoto kubwa ambayo imepelekea wakazi hawa kushindwa kuvuka kutoka upande mmoja kwenda mwingine kujitafutia riziki hasa maeneo ya mjini.
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga madaraja ya juu hasa zinaitwa overpass ili wakazi hawa waweze kuvuka kirahisi na hususan eneo la Michese katika Jimbo la Dodoma Mjini ambalo lina wakazi wengi sana walau wajengewe overpass moja tu waweze kupita maana sasa wanajua kutembea hadi kilometa nne ili kuvuka upande wa pili.
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chinyele, Mbunge wa Dodoma Mjini ambaye ametaka kufahamu mpango wa Serikali katika kujenga madaraja ya juu, vivuko vya juu katika maeneo mbalimbali ili kusaidia wananchi wake wa Kikuyu Kusini, Michese, Mkonze, Zuzu na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza, ni Mbunge ambaye ndiyo ameingia kwa mara ya kwanza, lakini unaweza kuona jinsi ambavyo anakesha kupambana na kupigania wananchi wa jimbo lake. Kweli nampongeza sana kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wetu na hata Waziri pale huwa anamsumbua sana kila wakati anaenda pale, mara amemwambia habari za Kizota mara Zuzu na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili nataka pia kumjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwanza uwekaji wa madaraja au vivuko vya chini na juu vinafanywa kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni na kwa kawaida vinapangwa kabla mradi haujaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi tunapozungumza, kuanzia Dar es Salaam mpaka Kigoma na mpaka Mwanza tayari Serikali ilikwishatambua maeneo ambayo yanapaswa kuwekewa vivuko hivyo. Kwa kuwa ameleta hoja hii mpya, ninawaelekeza Shirika la Reli waende wakaangalie maeneo hayo na kutazama, kulinganisha na mipango iliyopo Serikalini ili kama linawezekana basi tuone namna bora ya kuweza kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu pia ni changamoto, ni vigumu kusema kwamba kila palipo na watu tukaweke daraja la juu, kwa sababu ni gharama kubwa sana, lakini ushauri wake tumeupokea na ninaamini Mkurugenzi wa Shirika la Reli atakwenda kulitazama eneo hilo, na baada ya hapo chini ya maelekezo ya Mheshimiwa Waziri tutaona namna bora ya kuweza kufanyia kazi. (Makofi)
Name
Juma Ramadhani Mustafa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Igalula
Primary Question
MHE. JOHN S. LUHENDE aliuliza:- Je, lini Kampuni ya Yapi Merkezi wanaojenga Mradi wa SGR Bukene italipa fidia ya shilingi 2,666,666,666.64 inazodaiwa na Halmashauri ya Nzega?
Supplementary Question 3
MHE. JUMA M. KAWAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi niulize swali la nyongeza kwenye Wizara hii ya Uchukuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninapenda kuipongeza Serikali kwa kuanza kujenga kipande cha Lot 3 kutoka Makutupora kwenda Tabora na mikoa mingine, chenye kilometa 368.
Swali langu linajielekeza hapa, je, ni lini treni yetu ya gari moshi ambayo inabeba mizigo pamoja na abiria itaanzisha safari zake za kutoka Dar es Salaam – Morogoro – Dodoma mpaka kufika Tabora ili wakazi wa Vijiji vya Tura, Mayongwe, Nyahua, Goweko na Igalula waweze kunufaika kusafirisha abiria pamoja na mizigo ndani ya Jimbo la Igalula? Ahsante. (Makofi)
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mustafa, Mbunge wa Igalula kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini anamaanisha treni ya kisasa kwenye reli ya kisasa, kwa sababu kama ni treni ya metre-gauge inafanya kazi japo kwa kusuasua. Kwa sababu hiyo, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba nchi yetu inaendelea kunufaika kupitia sekta yetu ya uchukuzi kwa kuboresha njia ambapo kwa sasa njia ya treni ya metre-gauge njia yake inaendelea kuboreshwa kutokana na kwamba uwezo ulishuka sana, awali ilikuwa ni kubeba mzigo tani milioni tano, ukashuka mpaka tukafikia asilimia tano. Kwa hiyo, kwenye vipande mbalimbali Serikali inaendelea kufanya maboresho hayo makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kwenye upande wa reli ya kisasa ya SGR, Serikali imekwishaweka wakandarasi. Wote wako kazini, kutoka Dar es Salaam mpaka Kigoma, kutoka Tabora mpaka Mwanza. Mradi huu wote utaigharimu Serikali takribani dola bilioni 11.2.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa habari njema zaidi, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan mpaka ninapozungumza amekwishalipa zaidi dola bilioni 4.8 na wakandarasi hao wanadai kiasi kidogo cha fedha na wengine wanaendelea kutekeleza majukumu yao, watakapokamilisha wataendelea kulipwa, ninaamini kwamba mara baada ya mradi huu kukamilika basi wananchi wa Igalula, Mkoa wa Tabora pamoja na maeneo mengine nao wataanza kunufaika moja kwa moja na reli yetu au na treni yetu ya kisasa kama vile ambavyo kutoka Dar es Salaam mpaka Morgoro, Morogoro mpaka Dodoma tunavyonufaika.
Name
Kenneth Ernest Nollo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bahi
Primary Question
MHE. JOHN S. LUHENDE aliuliza:- Je, lini Kampuni ya Yapi Merkezi wanaojenga Mradi wa SGR Bukene italipa fidia ya shilingi 2,666,666,666.64 inazodaiwa na Halmashauri ya Nzega?
Supplementary Question 4
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona Serikali ikiweka Bandari Kavu sambamba na SGR na tumeona imefanya vizuri kuanzia Bahi na Isaka, lakini ukiangalia mizigo mingi inayoenda nje ya nchi inapita njia ya Tunduma.
Je, Serikali haioni kwamba iweke Bandari Kavu Morogoro ili mizigo mingi inayoenda corridor ya Tunduma kwenda Zambia na Kusini mwa DRC iweze kuchukuliwa kiurahisi katika sehemu ya Morogoro? Ahsante sana.
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Kenneth Nollo, Mbunge wa Bahi ambaye ninampongeza kwa jinsi anavyotazama umuhimu wa kuboresha sekta yetu hii ya Uchukuzi kwa sababu ndugu Waheshimiwa Wabunge, tukikubaliana sisi sote kwamba tukiboresha sekta yetu hii ya uafirishaji, kwa maana ya kujenga uwezo wa kibandari sambamba na miundombinu yake, basi nchi yetu ina nafasi ya kufanya vizuri zaidi katika ukanda wetu huu wa Kusini mwa Afrika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali inatambua umuhimu wa eneo la Morogoro na ninamhakikishia, wenzetu wa TRC (Shirika la Reli) wanayo maeneo ambayo walikuwa wameshayatenga. Ninaamini kwa ushauri huu tunaupokea na kuanza kuuchakata ili ama kushirikisha sekta binafsi kuhakikisha ya kwamba tunajenga bandari kavu kubwa. Kwa kweli kama anavyosema, mzigo mkubwa unakwenda Kusini mwa Afrika kuanzia na nchi zetu za jirani. Kwa hiyo, ukiwa na Bandari Kavu kubwa pale Morogoro, ni kweli itarahisisha mzigo wa SGR ukaja mpaka Morogoro, halafu pengine magari yakachukulia pale kwenda kwenye mikoa hii ya Kusini sambamba na nchi jirani ikiwemo Zambia, Malawi na nchi nyingine. Kwa hiyo, ni ushauri mzuri ambao Serikali tunaupokea.