Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Deodatus Philip Mwanyika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Njombe Mjini

Primary Question

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa mradi wa maji kwenye Mji Mdogo wa Kifanya katika Kata ya Kifanya?

Supplementary Question 1

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, na ninashukuru kwa majibu ambayo nimeyapata. Hata hivyo, ninasikitika kwamba mradi huu ni wa siku nyingi sana. Mradi huu ni ahadi ya Marehemu Mheshimiwa Rais Magufuli; ni ahadi ya Mheshimiwa Makamu wa Rais, alipopita na Mawaziri wawili wa Maji waliopita, Mheshimiwa Mbarawa akiwepo. Je, ni lini mradi huu utatekelezwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Tuna mradi mwingine wa Igongwi ambao nao ni wa muda mrefu. Ni mradi ambao umekamilika kwa 90% lakini hakuna maji. Je, ni lini mradi huu wa Igongwi unaokwenda kwenye kata zaidi ya nne utakamilishwa?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninamshukuru sana Mheshimiwa Deodatus Philip Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini kwa kazi kubwa ya kuendelea kuwasemea Wananjombe Mjini na kwa kazi kubwa ya kutoa ushirikiano kwa Wizara ya Maji. Hivi karibuni Mheshimiwa Mbunge ameongelea miradi hii, na amefanya mazungumzo na Mheshimiwa Waziri wa Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kama Serikali mradi huu wa kifanya ni ahadi za viongozi wa Kitaifa; na ahadi za viongozi wa Kitaifa ni lazima zitekelezwe. Sisi kama Serikali kupitia Wizara ya Maji ninamwahidi Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu feasibility study imekamilika, usanifu wa kina umefanyika na sasa tumesha-establish gharama ambazo ni shilingi bilioni 4.6.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba mradi huu tutaanza kutekeleza kwa awamu na kwa kufanya rescoping ili kuhakikisha kwamba usisimame kama ambavyo amesema kwamba ni ahadi ya zamani ya viongozi wa Kitaifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali la pili, kuhusu mradi wa Igongwi, ni kweli kabisa mradi huu ambao una gharama ya shilingi bilioni 4.8 umefikia takribani 90% ya utekelezaji wake. Tunatambua kwamba bado kuna mahitaji ya fedha. Kazi kubwa iliyokuwa imefanyika zaidi ni kuweka mabomba takribani kilomita 60 na sasa tuko katika hatua za mwisho. Kinachohitajika ni shilingi 200,000,000 ili mradi huu uweze kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba ndani ya miezi hii tutapeleka fedha milioni 200 ili kwenda kuhakikisha kwamba mradi huu unakamilika kwa sababu umefikia hatua nzuri za utekelezaji. Lengo ni kwamba uanze kutoa matokeo na wananchi wapate huduma ya maji safi na salama.

Name

Sylivia Francis Sigula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa mradi wa maji kwenye Mji Mdogo wa Kifanya katika Kata ya Kifanya?

Supplementary Question 2

MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira ya Mheshimiwa Rais ni kuwatua ndoo wanawake wa Tanzania na kuwapa tabasamu, lakini hali ya upatikanaji wa maji katika Mji Mdogo wa Namanyere ulioko Wilaya ya Nkansi, Mkoa wa Rukwa ni duni sana na kumekuwa na ahadi za viongozi wengi lakini mpaka sasa changamoto ni kubwa. Kwa kuwa tumepitisha bajeti, je, ni lini tatizo hilo litatatuliwa?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na nimshukuru sana dada yangu Mheshimiwa Sylvia kwa kuendelea kuwasemea wananchi wa Katavi na Rukwa, kwa sababu ni eneo ambalo linapitiwa na Ziwa Tanganyika; pia tunatambua kuna maeneo ambayo bado yana changamoto, hasa Mji Mdogo wa Namanyere ambapo pia tulikuwa na miradi iliyokuwa inaendelea, lakini haikukamilika vizuri na hasa kwenye hili suala la Mji Mdogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imepanga mpango wa kuhakikisha kwamba tunaenda kutatua, na Mheshimiwa Mbunge ameshiriki kutupitishia bajeti yetu ya maji ya shilingi trilioni 1.102, na ya maendeleo ambayo imeongezeka kwa takribani shilingi 205,000,000,000. Hii ni ishara kwamba Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kwenda kuhakikisha kwamba tunaenda kutatua changamoto za maji, hasa katika Mji wa Namanyere. Nimtoe hofu, tunaenda kulipa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, alisema kwamba kipaumbele cha Wizara kwa sasa ni kwenda kuhakikisha kwamba miradi viporo vyote tunaenda kuvimaliza, ahsante sana.