Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Bazilio Kapunda Mbwilo

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Nkasi Kaskazini

Primary Question

MHE. BAZILIO K. MBWILO aliuliza:- Je, lini Barabara ya Namanyere – Kipili, Nkasi Kaskazini, itajengwa kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 1

MHE. BAZILIO K. MBWILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninaishukuru Serikali kwamba, sasa barabara hii imefikia hatua nzuri. Kwa kuwa, barabara hii ni muhimu sana, hasa kwa mapato ya Serikali, kutokana na mizigo mingi inayokwenda nje ya nchi inapitia Bandari ya Kipili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kitu kimoja katika hizo kilometa 20 au hata ikibidi, pungufu ya hizo zianzie bandarini kwenyewe kwa ajili ya yale malori yanapokuja na mizigo; kwa sasahivi yanahangaika sana kuingia pale bandarini, lakini lami ikianzia bandarini hata kilometa mbili tunaweza kuwa tumevutia wasafirishaji wengi kuendelea kuitumia Bandari hiyo ya Kipili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kama Bandari ya Kipili ilivyo muhimu kwa uchumi wa nchi hii, Bandari ya Kabwe nayo ni hivyohivyo. Ninamuomba Mheshimiwa Waziri, walau kilometa moja tu tuijenge, ianzie bandarini, ili kuwezesha magari baada ya mihangaiko huko mbugani kwenye matope mengi yanapoingia kwenye gati yaweze kupita kirahisi. Ahsante.

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninaomba nijibu maswali mawili ya nyongeza, kwa pamoja, ya Mheshimiwa Mbunge wa Nkasi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakiri kupokea ombi lake, lakini pia, namweleza Mheshimiwa Mbunge kwamba, pamoja na kupokea huo ushauri, lakini lengo letu hasa ni kuhakikisha zile barabara zinapitika na tunajua barabara zinazotoka bandarini zinakuwa ni zenye uzito mkubwa. Kwa hiyo, pamoja na kupokea ushauri, lakini tutakachoshauriana na wataalamu ni hasa yale maeneo ambayo yanaweza kuwa ni kikwazo kwa magari kupita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, linaweza likatoka bandarini, lakini kama litakwama Katikati, hata kama tutakuwa tumeweka lami mwanzoni itakuwa haina maana. Cha msingi ninadhani tutaangalia yale maeneo korofi, ambayo yanaweza yakafanya barabara isipitike tufanye hasa kwa maombi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Kabwe tumeanza kufanya hivyo, maeneo yenye madaraja membamba na kwa maeneo korofi, tumetoa maelekezo yatengenezwe, ili magari yaweze kupita. Kwa hiyo, tutashauriana, lakini pia, wataalamu watashauri nini cha kufanya, hasa kulingana na ombi lako. Ahsante sana.

Name

Arif Suleiman Premji

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtwara Vijijini

Primary Question

MHE. BAZILIO K. MBWILO aliuliza:- Je, lini Barabara ya Namanyere – Kipili, Nkasi Kaskazini, itajengwa kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 2

MHE. ARIF S. PREMJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuzingatia Kanuni ya 56(1) ya Kanuni zetu za Bunge, kwa kuzingatia Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi ya 2025 – 2030, ujenzi wa barabara ya Ziwani kwenda Kilambo na kwa kuzingatia ripoti ya BOT ya mwezi Julai ambayo inaonesha makusanyo ya fedha yamevuka malengo. Je, lini ujenzi wa barabara ya Ziwani kwenda Kilambo utaanza? Ahsante sana.

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba moja, sisi kama Wizara tayari tumeshatenga hata fedha ya kuanzia kufanya upembuzi yakinifu na usanifu kwa lile daraja la Kilambo. Pia, ni mpango kwamba hiyo barabara tumeitengea fedha ya kuanza kuijenga kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama tulivyosema katika bajeti, kipaumbele kwanza kwa sasa ni ile miradi ambayo imesimama lakini pamoja na hiyo miradi ambayo tumeipangia fedha, tuna hakika kwamba ndiyo tunaanza utekelezaji wa bajeti na hasa kwa Ilani yetu ya miaka mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina uhakika kwa umuhimu wa barabara hiyo, nayo itakuwa ni kati ya barabara ambazo katika kipindi hiki zitaanza kujengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante.

Name

Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Primary Question

MHE. BAZILIO K. MBWILO aliuliza:- Je, lini Barabara ya Namanyere – Kipili, Nkasi Kaskazini, itajengwa kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 3

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaipongeza Serikali kwamba Makete tuliomba barabara mbili zipandishwe hadhi, barabara ya Ikuwo – Nkenja mmeipandisha hadhi kwenda TANROADS na inaendelea kujengwa. Pia kuna barabara kutoka Lupila – Kipengere ni barabara ambayo inawasumbua sana wananchi wa eneo la Lupila na eneo la Ipepo. Ni lini Serikali itatoa fedha ili barabara hii ianze kujengwa kwa kiwango cha changarawe, kwa sababu tayari iko kwenye mikono ya TANROADS kutoka mwaka 2024?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba barabara hiyo ya Lupila – Kipengere imeshapandishwa hadhi tangu 2024 na mara tu baada ya kupandishwa hadhi, TANROADS cha kwanza ilianza kuiweka katika hadhi ya barabara za TANROADS kwa sababu viwango vya barabara za TARURA na TANROADS vinatofautiana pakubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachofanya sasa hivi ni kuhakikisha inapitika na hata katika mwaka huu wa fedha, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge, hiyo barabara tutaendelea kuikarabati na imetengewa fedha ili iweze kukarabatiwa, kwa sababu ndiyo kwanza ilikuwa katika hadhi ya TARURA, Meneja ameelekezwa kwanza ahakikishe kwamba maeneo yale ambayo ni korofi ndiyo hasa yanatengenezwa kuhakikisha kwamba inapitika wakati sasa anaiweka katika viwango vya barabara ya TANROADS, hiyo barabara ambayo ina takribani kilometa 50. Kwa hiyo ninamhakikishia, tayari tunayo na tumeshaanza kupata bajeti yake, ahsante.

Name

Jacqueline Ngonyani Msongozi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. BAZILIO K. MBWILO aliuliza:- Je, lini Barabara ya Namanyere – Kipili, Nkasi Kaskazini, itajengwa kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 4

MHE. JACQUELINE K. N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Ninaomba niulize swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 124 kwa kiwango cha lami kutoka Songea Mjini eneo la Likuyufusi kwenda Mkenda, mpakani mwa Tanzania na Mozambique? Ahsante.

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Songea hasa kutokea Likuyufusi kwenda Daraja la Mkenda mpakani na Msumbiji tutaanza kuijenga kwa awamu. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tuna mkandarasi, huyu mkandarasi anasubiri alipwe advance na ndiyo barabara ambazo tulikuwa tunasema tutaanza kuzijenga ikiwa ni pamoja na hiyo barabara. Kwa hiyo, tutaanza Likuyufusi hadi eneo linaloitwa Muhukuru kwa kilometa 60. Kwa hiyo, sasa hivi muda siyo mrefu sana tumeshaanza kupokea fedha, tutamlipa fedha ya awali ili mkandarasi aende site kwa sababu tayari yupo. Ahsante.

Name

Naomy Duncan Mwaipopo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. BAZILIO K. MBWILO aliuliza:- Je, lini Barabara ya Namanyere – Kipili, Nkasi Kaskazini, itajengwa kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 5

MHE. NAOMY D. MWAIPOPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Uvinza – Lukoma mpaka kwenye lango la Mahale National Park yenye kilometa 38 ni mbovu na haipitiki hasa kipindi cha mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nini mpango wa Serikali kuhakikisha barabara hii inajengwa ili kuchochea uchumi wa utalii pale Uvinza? Ahsante. (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichukue swali la Mheshimiwa Mbunge na tutasaidiana na wenzetu wa TARURA kuhakikisha kwamba hii barabara kwa kweli kwa sababu inaenda kwenye mbuga muhimu ya utalii inakarabatiwa na inapitika kipindi chote cha mwaka, ahsante.