Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Fadhili Ally Liwaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nachingwea

Primary Question

MHE. FADHILI A. LIWAKA aliuliza:- Je, lini huduma za fedha kupitia mitandao ya simu zitapelekwa kwa wananchi Kilimarondo na Kiegei ambao hufuata huduma hiyo umbali wa kilometa 120?

Supplementary Question 1

MHE. FADHILI A. LIWAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na majibu mazuri na ya kutia moyo ya Serikali, ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Kwa kuwa maeneo ya Kiegei na Kilimarondo yamekuwa na mwamko mkubwa wa uzalishaji wa madini, hususan madini ya dhahabu na kumekuwa na mwingiliano mkubwa wa watu na uhitaji wa huduma za kifedha na kufanya miamala mbalimbali ya simu. Je, Serikali ina mkakati gani wa haraka wa kushawishi na kusukuma kampuni mbalimbali za simu za mkononi ili ziweze kwenda kujenga minara na kuwezesha huduma hizi muhimu za upatikanaji wa fedha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa majibu na jitihada hizi za kuhakikisha kwamba tunapata mawasiliano yenye huduma za kifedha ni za muda mrefu. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri ana utayari wa kuongozana na mimi japo kwenda kutembelea kwa siku nzima ili ajionee mazingira ya mawasiliano na masuala ya miamala katika maeneo ya Kilimarondo na Kiegei? (Makofi)

Name

Switbert Zacharia Mkama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ukerewe

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninaanza kwa kumpongeza, Mheshimiwa Liwaka amekuwa mfuatiliaji mzuri wa huduma hizi za kidijitali katika Jimbo lake na ni msumbufu kwelikweli. Amekuja Wizarani zaidi ya mara kumi, kwenye simu yangu nina meseji zake zaidi ya 30 na watu wasiomfahamu kama ni Mheshimiwa Mbunge wanaweza kudhani kwamba ni mtumishi wa Wizara yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninampongeza sana kwa kuwapigania wananchi wake. Hakika wananchi wa Nachingwea wamepata Mbunge jembe, jembe ulaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaanza kujibu swali la pili kuhusu kutembelea Jimbo la Mheshimiwa Liwaka. Ninamhakikishia Mheshimiwa Liwaka kwamba niko tayari, baada ya Bunge hili, tutapanga mimi na yeye ni lini nitakwenda kutembelea ili nikajionee hali halisi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la kwanza, Wizara yetu inaendelea na mazungumzo na watoa huduma mbalimbali ili kuhakikisha kwamba wanafikisha huduma katika eneo hilo kwa sababu amesema ni eneo la uzalishaji na lina mwingiliano mkubwa wa watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia umuhimu wa eneo hili, ninamwelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano kupitia taasisi zake kuratibu haya mashauriano yanayoendelea na watoa huduma ili kuhakikisha kwamba wanapeleka huduma za minara katika eneo alilolitaja Mheshimiwa Liwaka la Kiegei mapema iwezekanavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia kwamba Dira yetu ya 2050 inaitaka sekta binafsi iwe mstari wa mbele katika kuleta maendeleo ya nchi yetu na sisi hilo tumelizingatia, tunawasiliana na watoa huduma wetu ili kutekeleza pia dira yetu hii. Ninakushukuru. (Makofi)

Name

Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FADHILI A. LIWAKA aliuliza:- Je, lini huduma za fedha kupitia mitandao ya simu zitapelekwa kwa wananchi Kilimarondo na Kiegei ambao hufuata huduma hiyo umbali wa kilometa 120?

Supplementary Question 2

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Dunia iko kiganjani, huwezi ukapata fursa mbalimbali kama hauna mawasiliano, huwezi ukafanya huduma za kipesa kama hauna mawasiliano. Mheshimiwa Naibu Waziri ulikuja Bunda, hukuamini kama Jimbo la Bunda Mjini kuna maeneo hakuna mawasiliano, nikakupeleka Kabasa, nikakupeleka Guta, nikakupeleka Wariku, nikakupeleka Sazira, nikakupeleka Mcharo, nikakupeleka Bunda Stoo, Mgaya Ngogo hakuna mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini sasa ahadi yako uliyosema utatujengea minara ili wananchi wa Jimbo la Bunda Mjini wapate mawasiliano na waweze kufanya huduma mbalimbali za kifedha kupitia mawasiliano itatimia? (Makofi)

Name

Switbert Zacharia Mkama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ukerewe

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nilikuwa Jimboni kwake, ni Mbunge imara kabisa, alinipokea vizuri, tulitembelea maeneo yote aliyoyataja. Hakika Bunda wana Mbunge imara, Mbunge mchapazi, bado kijana, wanaweza kumuongeza miaka mingine 10. Hata hivyo, ninamhakikishia kwamba tutajenga minara katika Jimbo lake mwaka huu wa fedha ulioanza. Kwa hiyo, awe na amani, akawaambie wapigakura wake kwamba minara inakuja katika mwaka huu wa fedha. (Makofi/Kicheko)