Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2025-2030 Session 2 Sitting 1 Livestock , Fisheries, Agriculture, Food Security and Cooperatives Wizara ya Kilimo 13 2026-01-27

Name

Neema Gerald Mwandabila

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza:-

Je, upi mpango wa Serikali wa kuupatia fedha za uendeshaji Mfuko wa Pembejeo za Kilimo ili kuwafikia wananchi wengi?

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Kilimo, na ahadi yangu kwake ni siku zote tu kazi itaendelea na tutaifanya kwa uaminifu.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutenga fedha ili kuuwezesha Mfuko wa Pembejeo za Kilimo kupata fedha za uendeshaji na mitaji kwa wakulima hususan vijana na wanawake.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali iliidhinishiwa na Bunge shilingi bilioni 10 kwa ajili ya utoaji wa mikopo kwa vijana na wanawake. Vilevile, katika mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali imetenga shilingi bilioni sita kwa ajili ya kukopesha wakulima kupitia Mfuko huo. Hadi Desemba 2025, jumla ya mikopo 27 imetolewa yenye thamani ya shilingi bilioni 5.49. Kati ya mikopo hiyo, mkopo wa shilingi bilioni tano ni mkopo uliotolewa kwa Benki ya Ushirika (Coop Bank) ambapo vijana na wanawake wanaojishughulisha na kilimo katika Ushirika wanakopeshwa.

Mheshimiwa Spika, kati ya fedha zinazoidhinishwa kwa ajili ya utoaji wa mikopo, 13% ni kwa ajili ya usimamizi wa mikopo ikiwemo kutembelea wateja na kufanya ukaguzi. Serikali itaendelea kuuwezesha Mfuko wa Pembejeo za Kilimo fedha za uendeshaji kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu kwa vijana na wanawake ili kuhakikisha kilimo kinafanyika kwa tija. Ahsante sana.