Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Neema Gerald Mwandabila
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza:- Je, upi mpango wa Serikali wa kuupatia fedha za uendeshaji Mfuko wa Pembejeo za Kilimo ili kuwafikia wananchi wengi?
Supplementary Question 1
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Niseme tu, kutokana na kwamba Benki ya Ushirika kuweza kupata shilingi bilioni tano kutoka kwenye Mfuko wa Pembejeo, ni wazi inaonyesha yenyewe kama yenyewe haina mtaji. Swali la kwanza; ninataka kufahamu, kitendo cha Mfuko wa Pembejeo kutoa shilingi bilioni tano kwa Benki ya Ushirika, hawaoni kwamba Mfuko umepoteza mantiki ya kuwafikia wananchi wanyonge?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; 13% ya shilingi bilioni sita ni shilingi milioni 780, hii inaenda kwa ajili ya uendeshaji wa Mfuko. Sasa ninataka kufahamu, kitendo cha kuweka shilingi milioni 780 kufuatilia madeni ambayo yameenda kwenye mikopo 27 tu, hawaoni kama haya yatakuwa ni matumizi mabaya ya rasilimali za Taifa?
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ninamshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake na ninamthibitishia tu kwamba Serikali ambayo ni Wizara ya Kilimo kutumia Benki yake ya Ushirika (Coop Bank) na Serikali kutoa fedha kutoka AGITF kupeleka Coop, lengo ni kuongeza wigo mpana kwa ajili ya kuwafikia wakulima na hicho ndicho ambacho tumekifanya kwa sababu Ushirika inawagusa wakulima moja kwa moja kupitia maeneo ya Vyama vya Ushirika (AMCOS) pamoja na SACCOSS zake.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tumefanya hivyo kwa lengo la kuboresha ili tuweze kuwafikia wakulima wengi na mikopo yote hii inayotolewa, inatolewa kwa asilimia saba, asilimia ambayo haiko katika benki nyingine yoyote inayotolewa.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, suala la usimamizi. Fedha yoyote inahitaji usimamizi na ni lazima tufuate sheria za nchi na sheria zinazohusiana na usimamizi wa fedha ili kuhakikisha kwamba kila kinachotolewa lazima kifikie malengo yake. Hili lililowekwa ni lengo na siyo kwamba fedha zote ambazo zimetajwa hapa zinatumika kwa 100% kama ambavyo tumeainisha. Kwa hiyo ni kama target tu katika mwaka, lakini kiukweli katika matumizi inakuwa ni pungufu na hicho ambacho Mheshimiwa Mbunge amekiainisha. Ahsante sana.
Name
Salma Rashid Kikwete
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Mchinga
Primary Question
MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza:- Je, upi mpango wa Serikali wa kuupatia fedha za uendeshaji Mfuko wa Pembejeo za Kilimo ili kuwafikia wananchi wengi?
Supplementary Question 2
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninaomba kukupongeza na kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa na nzuri ambazo amezifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa leo tuko kwenye Wizara ya Kilimo, Mheshimiwa Rais wetu amejipambanua vyema kabisa katika eneo la kilimo kuhakikisha kwamba anaongeza bajeti kubwa na ya kutosha ili Tanzania iweze kujilisha yenyewe hatimaye Afrika na tuweze kuilisha dunia.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba tunazungumzia suala la pembejeo, pembejeo hizi ni muhimu sana kwa kuwa bila pembejeo uzalishaji unakuwa ni chini. Sasa swali langu ni kwamba, Wizara tuliomba na walitupangia kutupatia pesa shilingi bilioni 31.3 kwa ajili ya bonde letu la Kinyope. Je, Serikali lini mtatupatia hizi pesa shilingi bilioni 31.3 ili tuendeleze kilimo na kilimo hiki kitaleta manufaa kwa vijana pamoja na wanawake?
Mheshimiwa Spika, ninaomba jibu la Serikali. Ahsante sana. (Makofi)
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge mama Salma Kikwete, Mbunge wa Mchinga, anafanya kazi nzuri sana katika jimbo lake.
Mheshimiwa Spika, ninamthibitishia tu kwamba maelekezo ambayo Serikali imeshatoa katika hili bonde ambalo ameliainisha na maombi ya fedha ya shilingi bilioni 31.3, tayari Wizara ya Kilimo tumeshayapeleka Wizara ya Fedha na tunasubiri tu taratibu zikamilike ili tuhakikishe bonde lile linakamilishwa na linaanza utekelezaji wake kama tulivyoainisha. Ahsante sana.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved