Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2025-2030 Session 2 Sitting 1 Livestock , Fisheries, Agriculture, Food Security and Cooperatives Waziri wa Mifugo na Uvuvi 14 2026-01-27

Name

John Francisco Nzilanyingi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Primary Question

MHE. JOHN F. NZILANYINGI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kushirikiana na Sekta Binafsi kufufua Viwanda vya kuchakata samaki ili kuongeza ajira na mapato?

Name

Ng'wasi Damas Kamani

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa vile ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu, ninaomba kutumia fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini na kuniteua kumsaidia kama Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi. Ninamuahidi kwamba nitafanya kazi hii kwa weledi, nguvu, bidii kadri Mwenyezi Mungu atakavyonijaalia.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa John Fransisco Nzilanyingi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mpango kabambe wa kuendeleza Sekta ya Uvuvi wa mwaka 2021 – 2037 ambapo kipaumbele ni kuendeleza, kuanzisha, kuimarisha na kufufua viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi nchini ili kufikia kwenye uchumi wa viwanda unaoongozwa na sekta binafsi kwa maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha viwanda vyetu vinafanya kazi kulingana na matarajio ya Serikali, Wizara ipo katika hatua za maamuzi kulingana na taratibu za Serikali kuanzisha Mamlaka ya Uvuvi kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa rasilimali za uvuvi na kupambana na uvuvi usiozingatia sheria ili kuongeza upatikanaji wa samaki na hivyo kuwezesha viwanda vyetu kupata malighafi za kutosha. Kwa hatua za awali Wizara imeweka maboya 32 yenye thamani ya shilingi milioni 224 kwa ajili ya kulinda mazalia ya samaki katika eneo la Luchelele - Ziwa Victoria, Mkoani Mwanza.

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha ushirikiano na Sekta Binafsi, Wizara imeanzisha Dawati la Mitaji na Uwekezaji kwa lengo la kufuatilia kwa ukaribu changamoto zinazoikabili Sekta Binafsi (vikiwemo viwanda hivi vya samaki), kuzitafutia ufumbuzi na kuongeza uwekezaji na uchangiaji kwenye pato la Taifa ili kufikia azma ya Serikali ya kuelekea kwenye Uchumi wa Viwanda. Aidha, mipango mingine ya Wizara ni pamoja na kuhamasisha ufugaji wa samaki kwa vizimba ili kuwezesha upatikanaji wa samaki kwa wingi. Mpango huu utasaidia kuchochea uwekezaji wa sekta binafsi katika viwanda. Ninashukuru sana.