Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

John Francisco Nzilanyingi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Primary Question

MHE. JOHN F. NZILANYINGI aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kushirikiana na Sekta Binafsi kufufua Viwanda vya kuchakata samaki ili kuongeza ajira na mapato?

Supplementary Question 1

MHE. JOHN F. NZILANYINGI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi nyingine ili niweze kupata kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je, ni nini mpango wa Serikali wa kupambana na uvuvi haramu ambao unatajwa ndicho chanzo cha uhaba wa samaki na hivyo kupelekea viwanda vingi vifungwe?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; katika majibu ya Serikali, pamoja na jitihada ambazo inafanya za kuhamasisha ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba, Serikali bado haioni kwamba tutaendelea kuwa na changamoto ya upungufu wa samaki kwa sababu viwanda vyetu havitumii samaki aina ya sato ambaye ndiye hasa anafugwa kwenye vizimba vya samaki?

Name

Ng'wasi Damas Kamani

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa maswali mazuri. Katika swali la kwanza, Serikali inatambua uzito wa changamoto ya uvuvi usiozingatia sheria na athari kubwa ambazo uvuvi huu umeleta katika uchumi wetu na ndiyo maana mpaka sasa tunaendelea na jitihada mbalimbali na mipango ya kupambana na uvuvi huu haramu ikiwemo kuunda Mamlaka ya Uvuvi ambayo iko katika hatua mbalimbali na Mamlaka hii itapewa nguvu ya kisheria na kikanuni ya kupambana na uvuvi huu haramu.

Mheshimiwa Spika, Serikali pia inaendelea na doria mbalimbali za ulinzi kwa kushirikiana na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ikiwemo Jeshi la Polisi na Jeshi letu la Ulinzi wa Wananchi ili kuhakikisha tunaendelea kupambana na uvuvi huu usiozingatia sheria. Serikali pia inaendelea kushirikisha jamii zetu katika kulinda rasilimali hizi za uvuvi kupitia BMU zetu ambazo tunazo katika mialo yote nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, tunaendelea kutoa elimu kwa wavuvi wetu lakini pia tunaendelea kudhibiti uingizwaji na uuzwaji wa zana mbalimbali ambazo zinachochea au kuchangia katika uvuvi haramu.

Mheshimiwa Spika, katika swali la pili, tunatambua pamoja na kwamba Serikali na kwa jitihada za Mheshimiwa Rais, tunaendeleza programu mbalimbali za kuwezesha Watanzania yakiwemo makundi mbalimbali ya vijana, wanawake na vyama vya ushirika kushiriki katika uvuvi kupitia uvuvi wa vizimba. Hata hivyo bado tunatambua kwamba uvuvi huu hauwezi kuwa mbadala wa uvuvi wa asili.

Mheshimiwa Spika, kwa misingi hiyo, ndiyo maana tunaendelea na jitihada mbalimbali za kupambana na uvuvi usiozingatia sheria, kuu zaidi ikiwa ni uundwaji wa Mamlaka hii ya Uvuvi ambayo utaratibu wake katika Mpango wetu wa Serikali unaendelea vizuri. Tunawaomba tu Waheshimiwa Wabunge kwamba pindi tutakapokamilisha taratibu zetu za kiserikali na kuleta mpango huu wa uundwaji wa Mamlaka hii, basi watuunge mkono ili tuweze kuipa nguvu hii ya kisheria na kikanuni kupambana na uvuvi huu usiozingatia sheria. Ninashukuru sana. (Makofi)

Name

Yannick Ikayo Ndoinyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Primary Question

MHE. JOHN F. NZILANYINGI aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kushirikiana na Sekta Binafsi kufufua Viwanda vya kuchakata samaki ili kuongeza ajira na mapato?

Supplementary Question 2

MHE. YANNICK I. NDOINYO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kabla sijauliza kwa kweli ninatoa shukrani nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza ile ahadi yake ya kutujengea Barabara ya Gamba Gumu kutoka Ngorongoro kwenda kule mbugani Serengeti kwa kuwa ile barabara imeanza. Kwa kweli tunamshukuru sana.

Mheshimiwa Spika, swali langu la nyongeza kwa Wizara hii ya Mifugo, kama ambavyo tunatambua, viwanda ni nyenzo muhimu sana ya kuongeza thamani ya mifugo na kuongeza masoko na kipato cha wananchi wafugaji. Wilaya yangu ya Ngorongoro wananchi wakazi karibu 98%…

SPIKA: Mheshimiwa nenda kwenye swali moja kwa moja.

MHE. YANNICK I. NDOINYO: Mheshimiwa Spika, je, Wizara hii ina mpango gani wa kutujengea kiwanda cha nyama cha kusindika mazao ya mifugo ili kuongeza kipato kama vile inafanya kwa samaki?

Name

Ng'wasi Damas Kamani

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, Serikali iko katika utaratibu wa kufanya mambo yafuatayo ili kuhakikisha tunaongeza uwekezaji wa viwanda vya nyama na kuongeza tija kwa wafugaji wetu. Kwanza ni kuendelea kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ili waweze kuwekeza katika sekta hii ambayo kwa kiasi kikubwa ina uwezo wa kuchangia katika pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, pili, tunaendelea kuwahamasisha wafugaji wetu ili kuendelea kufanya ufugaji wa kisasa kuongeza tija na ubora wa mifugo yao ili pindi tunapofanya uwekezaji huu, basi mazao haya tunayoyapata katika mifugo yetu yaweze kuwa na ubora mzuri ili kukidhi soko la ndani na nje katika nchi yetu. Ninakushukuru sana.

Name

Kangi Alphaxard Lugola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwibara

Primary Question

MHE. JOHN F. NZILANYINGI aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kushirikiana na Sekta Binafsi kufufua Viwanda vya kuchakata samaki ili kuongeza ajira na mapato?

Supplementary Question 3

MHE. KANGI A. LUGOLA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Serikali ilikuja na mpango mzuri sana wa kuwakopesha wavuvi vizimba vya kufuga samaki ndani ya Ziwa Victoria. Tatizo limekuwa usambazaji wa vifaranga pamoja na chakula kwa wale wazabuni ambao wanatakiwa kufanya hivyo. Mfano mzuri wa kuchelewesha usambazaji wa vifaranga na chakula, ni kwa huyu mvuvi anaitwa Japhet Moya Rogombero Ngeresi Nyamuguru ambaye alipata vifaranga baada ya miezi tisa wakati vizimba vilikuwa ndani ya maji.

Mheshimiwa Spika, je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba hizo kero zinaondolewa ili mikopo hii iwe na tija kwa ajili ya Taifa letu? (Makofi)

Name

Ng'wasi Damas Kamani

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana. Serikali pamoja na kutoa uwezeshaji huu, tunaendelea kufanya tathmini ya karibu sana kuona changamoto zote tulizonazo katika uvuvi huu wa vizimba. Moja ya changamoto ambayo wavuvi wetu wamekutana nayo ni ucheleweshwaji wa vifaranga pindi wanapolipia kwa wale wazalishaji. Tayari tumeshaanza kufanyia kazi changamoto hii, moja ikiwepo sisi wenyewe kuanzisha na kuendeleza vituo mbalimbali vya uzalishaji wa vifaranga bora ili pale ambapo wavuvi wetu wanavihitaji, waweze kuvipata kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, hata kwa wale ambao wanazalisha kama sekta binafsi, tunaendelea kuwafuatilia na kufanya nao kazi kwa karibu ikiwepo kuwaratibu ili pale mfugaji au mvuvi anapolipia vifaranga vyake, kwanza aweze kuvipata kwa wakati, lakini pili aweze kupata idadi sahihi aliyolipia.