Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2025-2030 Session 3 Sitting 12 Planning and Investment Ofisi ya Rais: Mipango na Uwekezaji 135 2026-04-20

Name

Haran Nyakisa Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Primary Question

MHE. HARAN N. SANGA aliuliza:-
Je, lini Serikali itakuja na mpango wa pamoja ili kutoa suluhu ya mageuzi ya sekta binafsi katika kukuza uchumi?

Name

Dr. Pius Stephen Chaya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Haran Nyakisa Sanga, Mbunge kutoka Jimbo la Kigamboni, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari imekamilisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambapo sekta binafsi inatarajiwa kuchangia takribani 70% ya ukuaji wa uchumi. Ili kufanikisha azma hiyo, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji inaendelea kukamilisha Mpango wa Pili wa Maboresho ya Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI II). Pia, inaandaa sera mpya ya uwekezaji na mkakati wake wa utekelezaji, kwa lengo la kuhakikisha mazingira ya uwekezaji yanakuwa rafiki zaidi kwa wawekezaji wa ndani na nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2026/2027 imepanga kuandaa sera, sheria na mkakati wa kukuza sekta binafsi, pamoja na kuandaa mwongozo wa kupima utendaji wa sekta binafsi, mwongozo wa upimaji wa mchango wa sekta binafsi kwenye 70% ya uchumi na mfumo wa kitaifa wa usimamizi wa takwimu za biashara na uwekezaji. Ofisi pia itaendelea kuimarisha majukwaa ya sekta binafsi kupitia Tanzania Private Sector Foundation (TPSF), Vitengo vya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ngazi za mikoa na Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, Serikali inapanga kufungua One Stop Facilitation Centres katika kila Mkoa na Wilaya ili kurahisisha mazingira ya biashara na uwekezaji ngazi ya Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla, Serikali inaichukulia sekta binafsi kama mshirika mkuu wa maendeleo ya Taifa na itaendelea kuweka mazingira rafiki, thabiti na yenye kutabirika ili sekta hiyo ikue, izalishe zaidi, iongeze ajira, ipanue wigo wa kodi na hatimaye kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.