Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Haran Nyakisa Sanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigamboni
Primary Question
MHE. HARAN N. SANGA aliuliza:- Je, lini Serikali itakuja na mpango wa pamoja ili kutoa suluhu ya mageuzi ya sekta binafsi katika kukuza uchumi?
Supplementary Question 1
MHE. HARAN N. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ninashukuru kwa majibu mazuri sana ya Serikali, lakini ninaomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa kuwa, uchumi jumuishi ni mfumo wa uchumi unaohakikisha kila mtu ananufaika na maendeleo ya kiuchumi. Je, wananchi wa Kigamboni wananufaika vipi na uchumi jumuishi kama Serikali haijaweka kwenye mpango ujenzi wa Barabara ya BRT kutoka Kongowe - Mji Mwema - Feri na barabara ya lami kutoka Feri kwenda Pemba Mnazi ili vijana wa bodaboda, vijana wa mamalishe, machinga wa Kivukoni pamoja na Pemba Mnazi, Wavuvi wa Gezaulole, Wakulima wa Mbogamboga Mtaa wa Sala na Kibada waweze kunufaika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ninataka kujua ni lini Serikali itaanza kutekeleza mpango wa kuboresha mazingira bora ya biashara MKUMBI II kwa maana ya kutoa utitiri wa leseni za biashara kwa wafanyabiashara hususani wa Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla? (Makofi)
Name
Dr. Pius Stephen Chaya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manyoni
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Haran Nyakisa Sanga, Mbunge kutoka Jimbo la Kigamboni kwa maswali yake mazuri mawili, pia Mheshimiwa Haran ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti na amekuwa akichangia sana suala la uwekezaji hususani Kigamboni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo ninaomba nijibu maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza, ni kweli Dira yetu ya 2050 na mpango wetu wa miaka mitano wa 2026 - 2030 umezingatia kwamba tunahitaji kuja na uchumi jumuishi. Katika hili ninatambua kwamba Kigamboni ni eneo ambalo ni very potential kwa uwekezaji na tuna wawekezaji wengi sana wameweka viwanda Kigamboni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kupitia hili sisi kama Serikali na ndiyo maana kwenye mpango wa miaka mitano tumwekea kipaumbele kuboresha mazingira rafiki hususani miundombinu ya barabara, vilevile BRT kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunapovutia wawekezaji katika maeneo yale, wawe tayari kwenda kwa ajili ya kuwekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimhakikishie Mbunge tumepokea hoja yake na sisi kama Serikali tutaiingiza kwenye mpango yetu tuhakikishe kwamba wale wawekezaji ambao wanataka kwenda kule waweze kwenda na tuweze kupata manufaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, ni kuhusu MKUMBI II ni kweli kama Serikali tayari tupo mbioni kukamilisha utengenezaji wa mpango wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini na tayari huu mpango ulishapitia katika uhakiki Mheshimiwa Rais kutoka Zanzibar alikuja kwa ajili ya mapitio na tunategemea mwezi ujao tutazindua huu mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kwa kupitia huu mpango tunaenda kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji hususani kupunguza utitiri wa kodi, tozo, lakini urasimu ambao unaendelea katika kukuza sekta binafsi. Ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
Name
Ibrahim Mohamed Shayo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Mjini
Primary Question
MHE. HARAN N. SANGA aliuliza:- Je, lini Serikali itakuja na mpango wa pamoja ili kutoa suluhu ya mageuzi ya sekta binafsi katika kukuza uchumi?
Supplementary Question 2
MHE. IBRAHIM M. SHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa kuuliza swali dogo. Mheshimiwa Naibu Waziri, Moshi ulikuwa ni Mji mwenye viwanda vingi sana, lakini kwa sasa viwanda vyetu Moshi vimekufa na vilivyokuwa vimebinafsishwa waliobinafsisha wameingia mitini. Je, ni lini Serikali itahakikisha kwamba tunakwenda kuanzisha viwanda vipya na kufufua vile ambavyo vimekufa? (Makofi)
Name
Dr. Pius Stephen Chaya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manyoni
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru Mbunge kutoka Moshi Mjini kwa maswali yake mazuri na nilifanya ziara na Mheshimiwa Waziri Mkuu, Moshi Mjini, mojawapo ya changamoto ambayo alii-raise Mheshimiwa Mbunge ni suala la viwanda ambavyo vilikuwepo kule ambavyo kimsingi havifanyi kazi, lakini vilevile mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba tunakuja na viwanda vipya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Moshi ni mojawapo ya maeneo yetu ambayo tumeya-target kwa ajili ya kukuza viwanda hususani kwenye upande wa kilimo, vilevile kwenye viwanda mbalimbali vya manufacturing. Ninaomba nimhakikishie kwamba hoja yake tumeichukua na katika mipango yetu tutaipa kipaumbele. Ninashukuru sana.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved