Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2025-2030 Session 3 Sitting 19 Works and Transport Wizara ya Uchukuzi 229 2026-04-29

Name

Jasmine Chesco Ng'umbi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JASMINE C. NG’UMBI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia mafunzo ya kitaalamu wahitimu wapya katika sekta ya uchukuzi ili kuongeza ajira?

Name

David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Jasmine Chesco Ng’umbi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi na taasisi zake, inao utaratibu wa kuwapatia vijana wanaohitimu elimu ya juu mafunzo ya vitendo kupitia utaratibu wa ajira za muda mfupi za miezi sita hadi 12 baada ya kuhitimu, yaani (internship).

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kupitia LATRA, Wizara imeanzisha utaratibu wa kusajili mawakala wa kutoa leseni za usafirishaji kwa pikipiki za magurudumu mawili na matatu nchi nzima, ikiwa ni njia mojawapo ya kuongeza ajira kwa vijana. Hadi sasa, jumla ya mawakala 15 wamesajiliwa, wakiwemo vikundi vya kijamii, vyama vya ushirika na makampuni ambayo kwa pamoja yameajiri vijana zaidi ya 315.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, upo utaratibu unaotekelezwa na LATRA tangu mwezi Juni, 2022, kwa ushirikiano na vyuo mbalimbali kama Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Chuo cha Ufundi Arusha, Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na Vyuo vya VETA kutoa mafunzo ya uhudumu wa mabasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kufikia mwezi Februari, 2026 wahudumu 6,123 walishapewa mafunzo ambapo kati yao wanawake walikuwa 3,303 na wanaume walikuwa 2,820. Kati yao, wahudumu 3,722 walishapata usajili wa LATRA kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua hii imewaongezea thamani ya ajira zao waliokuwa kazini, kutoa ajira mpya na kuboresho vipato vyao.