Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Jasmine Chesco Ng'umbi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JASMINE C. NG’UMBI aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia mafunzo ya kitaalamu wahitimu wapya katika sekta ya uchukuzi ili kuongeza ajira?

Supplementary Question 1

MHE. JASMINE C. NG’UMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, kumekuwa na tatizo kubwa la ajali za bodaboda kutokana na hawa vijana wetu. Sasa ningependa kujua, Serikali haioni haja ya kutenga dawati maalum au kitengo maalum katika hospitali zetu, kuwasaidia hawa vijana wanaopata ajali za bodaboda ili wawe wanapewa kipaumbele au wanapata huduma za haraka wanapopata ajali hizi, kwani hawa vijana vifo vyao vimekuwa ni vingi sana? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Tunaelewa kama sasa Tanzania yetu imekumbwa na teknolojia, na vyuo vyetu vinavyotoa elimu juu ya udereva vimekumbwa na teknolojia. Sasa kutokana na ukuaji wa teknolojia, ningetamani kujua, je, Serikali haioni haja ya kuwasaidia hawa wahitimu wanaomaliza kila siku kwenye vyuo vyetu, kuwapatia elimu ya kisasa zaidi ili wanapopata ajira baada ya kuhitimu katika vyuo vyao, kuweza kuwa madereva mahiri na kuweza kuutumia ujuzi huo walioupata kwa umahiri zaidi? Ahsante. (Makofi)

Name

David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Jasmine Chesco Ng’umbi kwa jinsi ambavyo amejitoa kuamua kuwasemea vijana wenzake wa nchi hii haswa kundi la bodaboda. Ninakubaliana na ushauri wake kuhusu umuhimu wa kuweza kuwa na mkakati maalum wa kuwatazama hawa vijana wanaopata ajali, kwa sababu ni nguvu kazi ya Taifa. Wanapata ajali wakiwa wanakwenda kuhangaika kutafuta riziki za familia zao na kujenga nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli kupitia Wizara yetu ya Afya, ninaamini jambo hili wamelipokea, wataona namna bora ya kuweza kulifanikisha, na sisi kama Sekta ya Uchukuzi tutakuwa tupo tayari kwa ajili ya kulifanikisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Mheshimiwa Mbunge amezungumza kuhusiana na teknolojia namna gani ambavyo tunaweza kushiriki kikamilifu kuhakikisha kwamba vijina wetu mafunzo tunayowapatia, yanakuwa yanakidhi teknolojia ya sasa. Ni kweli hata hivi karibuni tumeshuhudia baadhi ya madereva wakipelekwa nje ya nchi. Teknolojia waliyojifunzia hapa kwetu wakienda huko inakuwa ni changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapokea ushauri huu, tunauingiza Serikalini kuanza kuuchakata. Nitumie nafasi hii kutoa maelekezo kwa Chuo chetu cha Taifa cha Usafirishaji ili waendelee kutoa mafunzo ambayo dereva au kijana akipata mafunzo huku kwetu, akienda mahali pengine popote duniani, aweze kufiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitoe rai na maombi kwa vyuo vingine na taasisi nyingine ambazo zinatoa mafunzo ya namna hiyo, ili kuweza kutazama mabadiliko ya teknolojia. Wahitimu mnaowatoa hapa waweze kuwa competitive mahali popote wanapokwenda duniani.

Name

Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Primary Question

MHE. JASMINE C. NG’UMBI aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia mafunzo ya kitaalamu wahitimu wapya katika sekta ya uchukuzi ili kuongeza ajira?

Supplementary Question 2

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili la udereva ni taaluma kama zilivyo taaluma nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, madereva wengi wanapata mafunzo kabla ya kupata leseni, lakini sasa hivi kumekuwa na usumbufu sana kwamba, madereva wa magari ya mizigo, lakini pia na magari ya abiria wanapokwenda ku-renew leseni zao wanalazimika tena kurudi darasani.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka kujua, Serikali haioni kwamba hii taaluma ya udereva ni kama inapata changamoto ya unyanyasaji hasa wakati wanapo-renew leseni? (Makofi)

Name

David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, mwenzangu wa Wizara ya Mambo ya Ndani atalielezea kwa kina, pengine jambo la leseni, lakini sisi kwetu Sekta ya Uchukuzi tunathibitisha madereva. Tumeweka utaratibu kufuatia ajali nyingi nchini ambapo Watanzania wengi wanakufa pia wakiwa hawana makosa. Tumeamua kufanya utaratibu wa kuthibitisha madereva.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge hili limepitisha Sheria Sura ya 413 ya Kifungu cha 5(1)(d) kuhakikisha kwamba LATRA imepewa mamlaka, dereva anarudi anafanya mtihani na kisha akithibitishwa anakwenda kuendelea kufanya kazi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo ni kuhakikisha kwamba wale madereva wanakuwa competitive, tunawapima. Utaratibu huu kwa wanaotoa huduma mbalimbali kwenye nchi yetu, hufanya hivyo. Kwa mfano, madaktari pamoja na kusomea kwa miaka mitano, bado wanapata leseni.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda hata kwa wanasheria, wanasimama Mahakamani, pamoja na kusoma vizuri, bado wakienda Mahakamani kule kila mwaka wanapata leseni ili waweze kuthibitishwa. Hata ukienda kwa Wahandisi, pamoja na kusoma, lakini bado wanapata vyeti vyao vile vya kutambulika rasmi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, lengo letu ni jema ili kuona yule dereva je, kweli taaluma hiyo anayo? Alipata leseni kwa namna ambayo iko sahihi?

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa madereva wanapokuja wameshawekewa LATRA imejenga mfumo, imeweka maswali karibu 1,000 wanayasoma mara kwa mara, kisha anapewa masaa matatu anafanya. Akipata 70% automatically sasa anaweza kuthibitishwa na kuendelea na kazi yake. Akifeli mara tatu, huyo dereva anarudishwa kwenda kujifunza upya.

Mheshimiwa Naibu Spika, tangu tumeanza mfumo huu takribani madereva 7,599 wamefanya mitihani na 54% wamefaulu, wale ambao hawakufanya vizuri tayari wanaelekezwa namna ya kufanya. Sasa wanaweza kufanya mitihani hii nchi nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, lengo kubwa ni kuhakikisha kwamba taaluma hii ya madereva wanaobeba abiria 60 wanakuwa ni watu wenye weledi, wenye uwezo ili kulinda uhai wa watu wetu kama ambavyo Serikali ya Awamu ya Sita ilikuwa imeahidi kulinda raia na mali zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.