Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
| Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
|---|---|---|---|---|---|---|
| 2025-2030 | Session 3 | Sitting 17 | Youth, Disabled, Labor and Employment | Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira na Mahusiano | 191 | 2026-04-27 |
Name
Chacha Mwita Wambura
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita Mjini
Primary Question
MHE. CHACHA M. WAMBURA aliuliza:-
Je, upi mkakati wa kuunda ajira na kukuza uchumi wa vijana kupitia miradi ya uzalishaji na ujasiriamali ili kupunguza utegemezi wa sekta ya madini – Geita?
Name
Rahma Riyadh Kisuo
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA MAHUSIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, ninapenda kujibu swali zuri la Mheshimiwa Engineer Chacha Mwita Wambura, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mkakati wa kuunda ajira na kukuza uchumi wa vijana kwa kuwawezesha kushiriki katika miradi ya uzalishaji na ujasiriamali, sambamba na kupunguza utegemezi wa sekta ya madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Mradi wa Mageuzi katika Sekta ya Madini kwa Maendeleo Jumuishi na Endelevu (MBT), vijana 5,983 wamewezeshwa kwa kupatiwa leseni, mafunzo na mitaji, huku wachimbaji wadogo 658 wakipatiwa mafunzo kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi katika mikoa ya kimadini ya Geita, Mbogwe na Chunya.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali inatekeleza mikakati jumuishi ikiwemo uratibu wa utekelezaji wa Sera ya Ajira ya Mwaka 2008 pamoja na sera nyingine za kisekta. Vilevile, utekelezaji wa programu za kuwawezesha vijana kama BBT na BBT-LIFE, pamoja na utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu kupitia Halmashauri na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia inaendelea kukuza ujuzi wa vijana, kuratibu fursa za ajira ndani na nje ya nchi, na kuhakikisha masuala ya ajira yanajumuishwa katika mipango ya maendeleo, hatua zinazolenga kukuza fursa za ajira na kuimarisha uchumi wa vijana kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved